Friday 10 June 2016

ASKARI JKU ATOSWA BAHARINI PEMBA



ASKARI wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kutoka ofisi kuu Pemba (jina linahifadhiwa), amenusurika kufa maji baada ya kushushwa kwenye chombo alichokuwa akisafiria kutoka Bandari ya Wete kwenda Fundo na kutoswa baharini.

Akizungumza na Uhuru, jana, askari huyo alisema, tukio hilo lilitokea Juni 4, mwaka huu, alipokuwa akisafiri ndani ya boti ndogo, iitwayo Upepo, kwenda kazini.

Alisema ghafla akiwa kwenye boti hiyo, iliyokuwa ikienda Fundo,
aliona ikigeuza mwelekeo na kuanza kwenda kisiwa cha Ukunjwi, kabla ya nahodha na watu wengine waliokuwemo ndani kumuamuru ashuke.

Kwa mujibu wa askari huyo, baada ya kushushwa baharini, alijitahidi kuogelea na kufanikiwa kufika nchi kavu na kutembea kwa miguu kurudi mjini.

“Nikiwa ndani ya chombo hicho tukiendelea na safari, katikati ya bahari wakaanza kunihoji.

"Nikawaambia nakwenda kwa sheha, ndipo chombo kikageuzwa na kuelekea Ukunjwi na baadaye wakaniamuru nishuke majini. Nikatapatapa hadi kufika juu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa ilikuwa mara yangu ya kwanza kuogelea,”alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Utawala wa JKU Pemba, Meja Juma Nassor, alisema tukio hilo limewashitua na kuviomba vyombo husika kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya wahusika waliotenda unyama huo.

Meja Nassor aliwataka wamiliki na manahodha wa vyombo vya usafiri wa nchi kavu na baharini, kufanyakazi bila ya ubaguzi kwa kuwachukua abiria wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid, alisema katika hatua ya kwanza, tayari serikali imekiagiza kikosi cha KMKM pamoja na Jeshi la Polisi, kukizuia chombo hicho kuendelea na kazi.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ameagiza kukamatwa na kufikishwa makahamani manahodha waliohusika na kitendo cha kumshusha askari huyo majini kwa kuwa kilihatarisha maisha yake.

“Tumeviagiza vyombo vya ulinzi kukikamata na kukizuia chombo hicho pamoja na kuwatafuta wahusika wa tukio hilo ili wafikishwe mahakamani. Serikali haiwezi kukaa kimya wakati raia wake wanahatarishiwa usalama wa maisha yao,”alisema.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi kwa serikali juu ya watu wanaowabagua wenzao katika kutoa huduma mbalimbali.

Tukio hilo linahusishwa na masuala ya kisiasa, kutokana na watu waliomshusha askari huyo majini, kabla ya kufanya hivyo, walimuhoji ili kujua ni mtu wa aina gani, ambapo baada ya kubaini ni mtumishi wa serikali, waliamua kumfanyia unyama huo.

No comments:

Post a Comment