Wednesday 24 August 2016

MAJAMBAZI WALIOFUNGA MTAA JELA MIAKA 30



WASHITAKIWA wawili wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, waliokuwa wakidaiwa kufanya tukio hilo Kariakoo, Dar es Salaam, kwa kufunga mtaa, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja, sambamba na kuchapwa viboko 12.

Washitakiwa hao ni Ali Juma au Mpemba (40) na Ali Ramadhan, maarufu Dodo (38), walipewa adhabu hiyo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage.

Hata hivyo, Hakimu Mwijage alisema washitakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka 21, kila mmoja kwa kuzingatia walishatumikia kifungo cha miaka tisa jela, walipotiwa hatiani mahakamani hapo kwa tuhuma hizo kabla ya Mahakama ya Rufani Tanzania, kukubaliana na rufani yao ya kupinga adhabu na shauri kuanza upya.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwijage alisema hakuna ubishi kwamba washitakiwa hao walishiriki katika tukio la unyang’anyi lililotokea Juni 11, 2004, katika mtaa wa Uhuru, Kariakoo, ambapo kwa kutumia nguvu na silaha za moto, waliiba simu na saa mbalimbali zenye thamani ya sh. 8,675,000, mali ya Said Suleiman.

Hakimu Mwijage alisema suala hilo halina ubishi kutokana na ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri, akiwemo mlalamikaji Suleiman na mwenzake, ambao walikuwepo dukani wakati watuhumiwa hao wanavamia mchana kweupe, huku mwenzao aliyekuwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), akirusha risasi ovyo hewani.

Alisema mashahidi wa pili (Suleiman) na wa tatu, waliweza kuwatambua washitakiwa hao katika gwaride la utambulisho na kutambua simu na saa zilizokuwa zimeibwa, ambazo simu sita alikutwa nazo mshitakiwa (Mpemba) na saa na gari dogo alilokutwa nalo mshitakiwa Dogo, ambalo lilitumiwa siku ya tukio.

Akichambua ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri, mashahidi hao waliieleza mahakama kwamba, mtuhumiwa Mpemba alikuwa anakwenda dukani hapo kabla ya tukio na siku hiyo ya tukio, aliambatana na mshitakiwa mwenzake (Dogo), ambaye alikuwa na bastola.

Hakimu Mwijage alisema mashahidi hao walieleza mahakama kwamba, baada ya watuhumiwa hao kufika dukani, waliamuru watu waliokuwepo kulala chini, huku Dogo akiwaonyesha bastola na nje kulikuwa na mtuhumiwa mwingine, aliyekuwa amevalia sare za JWTZ, akifyatua risasi hewani kuwatawanya watu.

Alisema baada ya hapo, mlalamikaji Suleiman alitoa taarifa polisi huku mashahidi wengine wakieleza kuwa, Mpemba alikamatwa Zanzibar, akiwa na simu sita na saa zilizoibwa dukani, ambazo mlalamikaji alizitambua na baadaye aliwapeleka polisi kuonyesha aliko Dogo.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, hakuna ubishi washitakiwa hawa wakati wa kufanya tukio, walikuwa na silaha za moto, hivyo upande wa Jamhuri umethibitisha kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kwa kiwango kinachohitajika. Hivyo mahakama inawaona washitakiwa wana hatia ya kufanya kosa hilo,” alisema hakimu huyo.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Komba, aliiomba mahakama iwapatie washitakiwa hao adhabu kwa mujibu wa sheria, huku washitakiwa wakiiomba mahakama kuangalia adhabu kwa kuwa wameshatumikia kifungo cha miaka tisa jela kabla ya kesi kuanza upya.

Akitoa adhabu, Hakimu Mwijage alisema amezingatia kwamba washitakiwa hao walishatiwa hatiani mahakamani hapo katika kesi namba 198 ya mwaka 2004 na walikuwa watumikie kifungo cha miaka 30 jela bila ya viboko.

Alisema washitakiwa hao walitumikia kifungo kwa muda wa miaka tisa wakati Mahakama ya Rufani inafuta mwenendo wa shauri Julai 15, mwaka jana na kuamuru Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa busara zake, iwapo anaweza kuamua kuwaachia huru au kuwafungulia mashitaka upya.

“Sheria iko wazi, mtatumikia kifungo cha miaka 30, lakini nitawaondolea miaka tisa mliyoitumikia, hivyo itabaki miaka 21.


Sambamba na hilo, mtachapwa viboko sita wakati adhabu inaanza na viboko sita baada ya miezi sita tangu muanze kutumikia adhabu,” alisema.

Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, washitakiwa hao waliomba kupatiwa nakala za hukumu kwa kuwa wana nia ya kukata rufani.

No comments:

Post a Comment