WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, kupeleka wakaguzi wilayani Mlele na kubaini watu waliokula fedha za Chama cha Ushirika cha Ukonongo na kuwachukulia hatua.
“Watakaobainika watiwe hatiani. Licha ya bodi ya ushirika huo kuvunjwa, hatuwezi kuacha suala hili limalizike kwa kuvunja bodi kwa sababu walioingia wanaweza kuiba kwa mategemeo ya kuvunjwa bodi," alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kiwanja cha Inyonga, wilayani Mlele.
Alisema kila mtumishi afanye kazi na awajibike kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa mujibu wa taaluma yake ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, kwani hilo ndilo lengo la kuajiriwa kwake.
“Haiwezekani hapa kuna ofisa ushirika halafu Waziri Mkuu analetewa mabango ya kumtaka atatue tatizo la chama cha ushirika. Hali hii inaonyesha hapa hakuna kazi inayofanyika,“ alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema wanahitaji watumishi watakaosikiliza maelekezo yanayotolewa na serikali na kuyafanyia kazi kwa sababu malengo ya Rais Dk. John Magufuli ni kuona nchi inabadilika, hivyo wasioweza ni vyema wakaandika barua za kuacha kazi.
“Msikubali kuhamasishwa kufanya mambo yatakayowaletea madhara. Fanyeni kazi ili tupate maendeleo. Hatuwezi kufananishwa na nchi ndogo ndogo, wenzetu wanafanya kazi nasi tupunguze maneno tufanye kazi,“ alisema.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini, ambapo imetenga zaidi ya sh. trilioni moja, kwa ajili ya kumalizia kazi ya usambazaji umeme nchi nzima, ikiwemo wilaya ya Mlele.
Alisema watapeleka jenereta kubwa mbili, zitakazofungwa katika kijiji cha Utende, ambazo zitasambaza na kuwasha umeme katika kata ya Inyonga na maeneo mengine.
“Novemba, mwaka huu, umeme utakuwa umewaka wilayani Mlele. Mkakati ni kuunganisha mkoa wa Katavi na gridi ya taifa kutoka Tabora kupita Sikonge hadi Inyonga,“alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na mbunge wa Katavi, Mhandisi Isack Kamwelwe, alimwomba Waziri Mkuu, Majaliwa kuwasaidia kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya cha Inyonga na kuwa hospitali ya wilaya kwa sababu wilaya yao haina hospitali.
Pia, aliomba wilaya hiyo ipatiwe umeme wa TANESCO ili kupunguza gharama kubwa za kununua umeme kutoka kwa mfanyabiashara, ambaye amefunga jenereta na anawauzia uniti moja sh. 1,000, wakati shirika hilo linauza sh. 100 kwa uniti moja.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda, alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto, ikiwemo ya ukosefu wa nyumba za watumishi, hali inayosababisha mkuu wa wilaya na katibu tawala wa wilaya kuishi kwenye nyumba za kupanga.
No comments:
Post a Comment