Wednesday 24 August 2016
MKE WA BILIONEA MSUYA KORTINI MAUAJI YA WIFIYE
MKE wa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, bilionea marehemu Erasto Msuya, Miriam Msuya, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa tuhuma za mauaji ya dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya, yaliyotokea Kibada, Kigamboni.
Miriam (41), mfanyabiashara na mkazi wa Sakina kwa Idd, Arusha, alikamatwa jijini Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kwa ajili ya kusomewa tuhuma hizo za mauaji ya wifi yake.
Mke huyo wa bilionea Msuya, alifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Bankika.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo, ulimsomea mshitakiwa huyo shitaka la mauaji.
Diana alidai Miriam, Mei 25, mwaka huu, eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, alimuua Aneth.
Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mauaji kwani husikilizwa na Mahakama Kuu.
Wakili Diana alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 6, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande hadi tarehe hiyo, shauri litakapotajwa.
Agosti 9, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kumtia mbaroni mke wa bilionea huyo, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Aneth.
Aneth, ambaye alikuwa Mtumishi wa Wizara ya Fedha na mdogo wa bilionea Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment