Monday 24 October 2016

SMZ YAPIGA MARUFUKU SIASA KWENYE NYUMBA ZA IBADA


NA JUMA MOHAMMED, MAELEZO-Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imepiga marufuku wanasiasa kutumia nyumba za ibada kwa shughuli za kisiasa visiwani Zanzibar.

Akitoa tamko hilo jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema serikali inawaagiza wakuu wa mikoa yote ya Zanzibar, kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao.

“Kwa taarifa hii, serikali inawaagiza wakuu wa mikoa kupitia kamati zao za ulinzi na usalama, kusimamia utekelezaji wa agizo hili katika mikoa yao,”alisema Waziri Aboud.

Aidha, serikali imewaagiza wakuu hao wa mikoa kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayekiuka agizo hilo.

Waziri Aboud alisema viongozi wa dini na kamati zao katika nyumba za ibada, watakaoruhusu wanasiasa kuendesha shughuli za kisiasa, watawajibika kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema hivi karibuni kwenye misikiti  ya Mbuyuni, Kihibnani na Kwabiziredi, Mkoa wa Kusini Unguja, kumetokea tabia kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa kupita na kutoa hotuba za kisiasa.

Waziri huyo alisema shughuli za vyama vya siasa zinaendeshwa chini ya sheria N0 5 ya mwaka 1992, ambayo imeeleza wazi mipaka na shughuli za kisiasa zinavyopaswa kuendeshwa chini ya sheria hiyo.

“Vitendo vinavyofanywa na viongozi hao wa kisiasa wanaotumia nyumba za ibada kama majukwaa ya kisiasa, wanakwenda kinyume na dhamira ya katiba na sheria za nchi, ikiwemo sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992,”alisisitiza waziri huyo.

Waziri Aboud alisema shughuli zote za  dini ya kiislamu Zanzibar, zinasimamiwa kupitia sheria namba 9, ya mwaka 2001, namba 2 ya mwaka 2007 na namba 3 ya mwaka 1985, zinazoongoza taasisi mahsusi kama vile ofisi ya Mufti, Mahakama ya Kadhi na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.

Alisema kupitia katiba na sheria, uhuru wa mtu kuabudu dini anayoitaka umetolewa bila kuingiliwa na itikadi za vyama vya siasa, kama inavyobainishwa na katiba zote mbili, ibara ya 19, ambazo zinaeleza umuhimu wa uhuru wa mtu kuamini dini aitakayo kwa misingi ya kukuza usalama na amani katika jamii.

Waziri Aboud alisisitiza wananchi kuzitumia nyumba za ibada kwa shughuli za kidini kama ilivyokusudiwa na kuachana kabisa kushirikiana na viongozi au wananchi wengine, ambao wanatumia nyumba za ibada kujinufaisha kwa maslahi binafsi ya kisiasa.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, amekuwa akipita kwenye baadhi ya misikiti, hususan baada ya swala ya Ijumaa na kuhubiri siasa kupitia misikitini.

Kutokana na tabia hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCC, Shaka Hamdu Shaka, aliitaka Serikali ya Mapinduzi Zanziba (SMZ), kumdhibiti Maalim kwa kuwa anakiuka katiba na sheria za nchi.

Shaka alitahadharisha kwamba endapo SMZ haitafanya hivyo, vijana wa CCM watalazimika kuchukua hatua kuhakikisha Maalim Seif anafuata sheria za ikiwemo kutoendesha siasa misikitini.

No comments:

Post a Comment