Monday 24 October 2016

CCM YASHINDA UMEYA KINONDONI, CHADEMA, CUF WASUSIA UCHAGUZI


NA MUSSA YUSUPH

MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamini Sitta, amefanikiwa kuivunja ngome ya wapinzani, baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Aidha, George Manyama (CCM), amechaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo, ambayo awali ilikuwa ikiongozwa na CHADEMA.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika jana, katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni, wagombea hao walipata ushindi wa kura zote 18, huku madiwani kutoka CHADEMA na CUF, wakigomea kushiriki kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni hofu ya kushindwa.

Hofu hiyo ilidaiwa kuwaingia CHADEMA na CUF, kutokana na akidi ya madiwani wa CCM kuwa kubwa kuliko ile ya wanaotokana kwenye vyama hivyo ndani ya Manispaa ya Kinondoni.

Orodha ya idadi ya madiwani wa CCM kwenye halmashauri hiyo ni 18, CUF wanne na CHADEMA ikiwa na madiwani 12, hivyo upande wa wapinzani ulijikuta ukiwa na madiwani 16, ikizidiwa madiwani wawili na CCM.

Akitoa ufafanuzi wa uchaguzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Aron Kagurumjuli, alisema taarifa ya kufanyika kwa uchaguzi huo ilitolewa kwa mujibu wa sheria kwa wahusika kupokea barua za kufahamishwa.

Alisema kwa sababu hiyo, kujitoa kwa madiwani wa CHADEMA na CUF hakutoathiri kuendelea kwa uchaguzi huo kwani unafanyika kihalali.

“Wajumbe wote walipata barua ya wito na kuzipokea kupitia 'dispatch', lakini baadhi yao wamefika na kugoma kuingia ukumbini.

“Kukaa kwao nje hakutuzuii kuendelea na uchaguzi kwa sababu utaratibu wote umezingatiwa na kufuatwa,”alieleza mkurugenzi huyo.

Alisema madai kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), ni mkazi wa Kinondoni, hayana ukweli kwani mbunge huyo anaishi eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivyo ni mkazi wa Ubungo na anapaswa kushiriki kwenye vikao vya baraza la madiwani kwenye wilaya hiyo mpya.

Pia, uamuzi huo ulimgusa Mbunge wa Viti Maalumu, Salma Mwasa (CUF), ambaye ni mkazi wa Kimara na kwa sababu hiyo, alipaswa kushiriki vikao hivyo kupitia Manispaa ya Ubungo.

Aidha, Kagurumjuli alilazimika kutoa ufafanuzi kuhusu wabunge wateule wa Rais Dk. John Magufuli, ambao wanaitumikia manispaa hiyo kama madiwani.

Alibainisha kuwa wabunge hao wanachaguliwa na Rais kwa majukumu maalumu na hawana mchakato kwani mchakato wao hufanywa na Rais mwenyewe.

Alisema endapo madiwani wa upinzani wasipohudhuria vikao vitatu mfululizo vya baraza hilo, watakuwa wamejiondoa kwenye nafasi hizo na kwa mamlaka aliyonayo, ataitisha uchaguzi mwingine kwenye kata zao.

Aliagiza kusomwa barua iliyoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, ikifafanua kuhusu makazi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Barua hiyo ilieleza kuwa, Profesa Ndalichako ni mkazi wa Manispaa ya Kinondoni na anawajibu wa kuitumikia manispaa hiyo.

Kutokana na uthibitisho huo, Katibu Tawala wa manispaa hiyo, Gift Msuya, alitoa nafasi ya kula kiapo kwa Profesa Ndalichako, kuitumikia manispaa hiyo kama diwani.

Kiapo hicho kilimwezesha waziri huyo kushiriki shughuli zote za manispaa ya Kinondoni kwa nafasi yake ya udiwani, ikiwemo kushiriki kwenye uchaguzi huo.

UPIGAJI KURA

Baada ya kutolewa kwa ufafanuzi huo, saa 4.41 asubuhi, utaratibu wa upigaji kura ulianza kwa wagombea kutakiwa kuelezea sera zao.

Kwa mujibu wa orodha ya wagombea, CHADEMA iliwasilisha jina la Mustapha Murro, kuwania nafasi ya Meya, CUF ilimpendekeza Bunju Amri, kugombea nafasi ya Naibu Meya na CCM iliwasilisha jina la Sitta kuwania nafasi ya Meya na Manyama kugombea nafasi ya Naibu Meya.

Kutokana na wagombea wa CHADEMA na CUF kususia uchaguzi huo, wagombea wa CCM walikosa wapinzani, hivyo wao pekee ndio walipewa nafasi ya kuelezea mikakati yao.

Baada ya hapo, utaratibu wa upigajikura ulifanyika kwa kila mjumbe kutumia haki hiyo muhimu ya kidemokrasia.

Utaratibu huo ulipokamilika na kura kuhesabiwa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo aliwatangaza wagombea wa CCM kuibuka na ushindi wa kishindo kwa wote kupata kura zote 18.

Nderemo na vifijo vilitawala kwenye ukumbi huo, vikiashiria kufika ukiongoni kwa safari ya muda mfupi ya upinzani kuongoza Kinondoni.

Sitta, ambaye ni meya mpya wa manispaa ya hiyo, alitoa shukrani kwa madiwani, viongozi na wanachama wa CCM kwa kushirikiana na kuhakikisha ushindi unapatikana.

Aliahidi kuifanya halmashauri hiyo kuwa ya mfano Afrika, kwa kuiletea maendeleo kwa ushirikiano na watumishi waliopo.

Naye Manyama alisema atashirikiana na madiwani kufikia malengo yaliyowekwa kwani hajawahi kushindwa tangu alipoanza nafasi ya kutumikia umma.

Meya huyo alilazimika kuahirisha mkutano huo kwa zaidi ya nusu saa ili kuandaa kamati za maendeleo, baada ya ombi la kuundwa kwa kamati hizo kwenye kikao kijacho cha baraza, kugonga mwamba.

Uamuzi huo aliuchukua baada ya Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge, kutaka kuundwa kwa kamati hizo kabla ya kikao hicho kuahirishwa.

“Wakati tulipojitoa kwenye uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Ilala, wapinzani hawakusubiri, siku ile ile waliunda kamati za maendeleo kwa kuwajumuisha madiwani wa CCM, licha ya kususia uchaguzi huo.

“Hapa hakuna cha kusubiri, ni vyema baraza likaahirishwa, meya, naibu pamoja na mkurugenzi mkaunde kamati,”alisisitiza.

Kutokana na hoja hiyo, Sitta aliwahoji madiwani endapo wanakubali hoja hiyo.

Madiwani wote waliunga mkono hoja hiyo, hivyo aliahirisha kikao hicho kwa muda wa nusu saa ili aweze kuunda kamati.

NJE YA UKUMBI

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, ulinzi uliimarishwa nje na ndani ya ofisi za halmashauri hizo huku idadi kubwa ya wafuasi wa CHADEMA wakijikusanya kwenye vikundi.

Kama ilivyo kawaida yao, wafuasi hao walikuwa wakibishana na polisi waliokuwa wakiwataka kukaa nje ya uzio maalumu uliowekwa kwa ajili ya usalama.

Licha ya ukaidi huo, polisi walitumia busara zaidi kukabiliana nao ili wasiweze kuzua tafrani.

Wafuasi hao waliokuwa wamevalia sare za CHADEMA, mara kadhaa walijaribu kutaka kuwazuia baadhi ya madiwani wa CCM, waliokuwa wakiingia kwenye mkutano huo, hivyo kuwapa wakati mgumu polisi kuwadhibiti.

No comments:

Post a Comment