Sunday, 26 February 2017
DC HAPI AWATANGAZIA VITA WAVAMIZI WA MAENEO YA WAZI
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, ametangaza vita dhidi dhidi ya wavamizi wa maeneo ya wazi na wale wanaojimilikishia viwanja kinyume na taratibu kwenye manispaa hiyo.
Amesema atahakikisha maeneo yaliyovamiwa, yanarudishwa na wavamizi hao kuchukuliwa hatua.
Hapi alitangaza vita hiyo jana, wakati alipokuwa kwenye ziara katika kata ya Wazo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya siku 10, kwenye baadhi ya kata zilizoko ndani ya manispaa hiyo, kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Alisema katika wilaya yake, kuna tatizo kubwa la uvamizi wa maeneo ya wazi na kujimilikisha bila kufuata taratibu na kusababisha kuibuka kwa migogoro.
"Yaani katika wilaya yangu, tatizo la uvamizi wa maeneo ya wazi limekuwa kubwa sana. Majambazi wanatoka kona mbalimbali za Dar es Salaam, wanakuja kuvamia Kinondoni, hususan kata ya Wazo na kusababisha migogoro ya ardhi. Nasema sitokubali," alisema.
Hapi alisema atatumia nguvu zote kuhakikisha maeneo hayo yanarudishwa sehemu husika.
Aidha, aliviagiza vyombo vya ulinzi pamoja na watumishi wa ardhi kuhakikisha wanawakamata watu hao na kuwafikisha mahakamani.
Hapi alisema ameiagisha halmashauri hiyo kufuta hati za mashamba na kuyapima ili yawe viwanja.
Alisema mashamba mengi huwa yanasababisha migogoro kutokana na wananchi wengi kushindwa kuyaendeleza.
"Nawaomba watendaji wa manispaa, mpo hapa mnanisikiliza, sitaki kuona umiliki wa shamba kwenye halmashauri yangu. Yote muyapime na viwanja tutagawana nao, ikiwa ni pamoja na kufidia gharama ya upimaji,"alisema.
Kuhusu dampo la uchafu, Hapi alimuagiza mkugurenzi wa manispaa hiyo, kutafuta eneo la dampo ili wananchi wanaokaa maeneo ya Bunju, Wazo na Mabwepande kulitumia.
"Dampo likiwa karibu, litasaidia sana kupambana na uchafu, kuliko ilivyo sasa dampo lipo Pugu,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment