Monday 13 February 2017

JPM: VITA IMENZA, ITAENDELEA, HAITAISHA


NA MUSSA YUSUPH
RAIS Dk. John Magufuli amekoleza moto dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya, ambapo amesisitiza kuwa, vita hivyo vilivyoanza ni endelevu, havitosimama kamwe na havitoangalia sura wala wadhifa wa mtu.
Aidha, amewataka mabalozi wanaoliwakilisha taifa nje ya nchi, kutojiingiza kuwasaidia Watanzania waliokamatwa kisha kuhukumiwa kifungo au kunyongwa kwenye mataifa hayo, kwani wanastahili adhabu hizo kwa sababu nguvu kazi ya taifa imekuwa ikiangamia kwa vijana wengi kujihusisha kwenye matumizi ya dawa hizo.
Katika kuonyesha namna ambavyo mapambano hayo yalivyoshika kasi, Rais Dk. Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kuendeleza moto wa mapambano hayo kwa kuwadhibiti wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.
Pia, amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, kufanya mageuzi makubwa kwenye idara hiyo, hususan kitengo cha fedha kutokana na kuwepo kwa vitendo vya ubadhirifu.
Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam, jana, Rais Dk. Magufuli alisema mapambano hayo hayataangalia cheo wala jina, hivyo Watanzania wanapaswa kuiunga mkono serikali, ambayo imepewa mamlaka ya kuongoza vita hivyo kupitia Sheria namba tano ya mwaka 2015 kifungu cha 10.
“Sheria namba 5 ya mwaka 2015, tumepewa mamlaka sisi serikali ya kupambana na dawa za kulevya, hatutojali mtu yeyote. Awe mbunge, waziri, mwanasiasa, polisi, mwanajeshi, mtoto, mkubwa, mchungaji, padre au sheikh tupambana naye. Hili nataka kusema kwa dhati.
“Nawapongeza wabunge waliopita chini ya Spika Mama Anna Makinda. Walikaa bila kujali vyama vyao na kupitisha sheria namba 5 ya mwaka 2015, ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya. Vilevile nampongeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwa kupata uchungu kwa Watanzania waliokuwa wakiumia kwa kuweka saini ya matumizi ya sheria hii Mei 11 mwaka 2015. Sisi tunawajibu wa kusimamia, hatutorudi nyuma,” alisema.
Alisema madhara kwa taifa yamekuwa makubwa kwani hadi sasa zaidi ya Watanzania 1,000, wameshafungwa kwenye magereza ya nchi mbalimbali duniani kwa makosa ya kukutwa na dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa na Rais, Watanzania waliofungwa Msumbiji 20, Nepal wanne, India 26, Uturuki 38, Ugiriki 98, Malaysia 16, India mmoja, Comoro watatu, Pakistani 13, Japan sita, Nigeria mmoja na Ghana mmoja.
Zingine ni Uingereza 24, Kenya 66, Misri wawili, Uganda 15, Ethiopia saba, Iran 63, Brazil 12, Afrika Kusini 296 na China zaidi ya 200 huku 68 wakiwa wamehukumiwa kunyongwa.
“Wale wote waliohukumiwa nje ya nchi, wawe wamehukumiwa kunyongwa au kufungwa maisha, Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi wetu msijihusishe katika kitu chochote. Waacheni wapate wanachostahili. Kama amefungwa kwa dawa za kulenya na akahukumiwa kunyongwa, mwache anyongwe,” alisisitiza.
Rais Dk. Magufuli alisema kwa takwimu zilizopo, zinaonyesha kuwa, Dar es Salaam kuna kesi zaidi ya 50, zinazohusu dawa za kulevya, hivyo hakuna mzaha kwenye vita hiyo na yeyote mwenye kulipenda taifa hawezi kunyamaza.
“Mtu anakwenda kuripoti polisi halafu wengine wanapiga deki gari, kwani mliambiwa hapo ni mahali kwa kusafisha magari? Na polisi mpo hapo tu. Shika wote na gari likiwezeka weka rock up. Mtu anapeleka kwaya, mliambiwa mnakwenda kuimbiwa mapambio. I wish I could be IGP.
“Sasa sitaki kitokee cha namna hiyo. Mambo ya msingi tunaweka mzaha, mbona hawakwenda Lugalo kuimba. Tunataka vyombo vya ulinzi viheshimiwe. Tukileta mzaha tutakuja kujuta,” alisisitiza.
Pia, Rais Dk. Magufuli alieleza namna yeye na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walivyofichwa kuhusu majukumu yao kwenye Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na mamlaka hiyo, rais anajukumu la kumtea Kamishna Mkuu huku Waziri Mkuu atakuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.
“Pamoja na kwamba sheria ilipitishwa, Waziri Mkuu hakujua kama yeye ni mwenyekiti, alifichwa. Waziri Mkuu kama amejua, basi amejua jana au juzi, kwamba yeye ni Mwenyekiti wa baraza linalohusika katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.
“Lakini hata mimi sikuletewa mapendekezo ya kumteua Kamishina Jenerali, mpaka nikaamua kumteua. Ni lazima tuzungumze ukweli kwani tukificha, tutajifanya malaika. Sijaletewa na niliamua kuteua mwenyewe. Kwa hiyo mnaweza kujua kwa namna gani vita hii ilivyokuwa kubwa,” aliweka bayana Dk. Magufuli.
Rais pia alimpongeza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na wakuu wengine wa mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya na Shinyanga kwa kuanza kupambana dhidi ya wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa hizo.

MAJALIWA ALONGA
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa alisema endapo matumizi ya dawa hizo yakiachwa, kutasababisha athari kubwa kwa wananchi, hivyo vita hiyo itaendelea na haitosimama kamwe.
Alisema katika kuongeza nguvu ya mapambano hayo, mawaziri wa Mambo ya Ndani, Nje, Ulinzi, Elimu, Afya, Fedha, Habari pamoja na wakuu wote wa mikoa watashiriki.
“Vita hivi lazima viendelee ndani hadi nje ya nchi. Hatoachwa mtu yeyote bila kujali uwezo, cheo au rangi yake,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kwa mwaka jana, zilikamatwa bangi kilo 3,798, mirungi kilo 1,814, heroin kilo 50.4 pamoja na cocaine kilo 5.4.
GWAJIMA AIBUKA, ADAI  MSAFI
Wakati huo huo, Emmanuel Muhamed anaripoti kuwa, baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kutoka rumande kwa masharti, ameibuka na kudai kuwa yeye ni mtu msafi.
Aidha, ametangaza kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli katika vita dhidi ya dawa za kulevya na kwamba, ameingia rasmi kwenye vita hivyo katika kusaidia juhudi za serikali.
Mbali na hilo, Gwajima leo anatarajia kuripoti kituo cha Polisi Kati,saa tatu asubuhi.
Askofu huyo alisema hayo jana, Dar es Saalam, kabla ya kuanza ibada ya Jumapili katika kanisa lake, liloko Ubungo, ambapo alieleza kuwa, hapingi juhudi za kuendelea kwa vita hivyo, bali utaratibu wa kutaja majina ubadilishwe. 
“Baada ya kwenda kituoni hapo, nilichukuliwa kwenda kupimwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali na majibu yalionesha kuwa sijawahi kutumia na ndipo tukaaenda nyumbani kwangu kunipekua, pia hawakukuta kitu na ndipo wakanipa cheti ya kuwa ni msafi,”alisema.
Alisema baada ya polisi kubaini kuwa ni msafi, bado walifanya ukaguzi kwenye akaunti za benki zake zote kwa ajili ya kujiridhisha zaidi katika sakata hilo.
“Niseme kuwa vyombo vya dola na ofisi ya Rais vimefanya kazi kubwa kwa uaminifu na weledi katika kufahamu ukweli kuhusu suala hili la madawa ya kulevya dhidi yangu,”alisema.
Alisema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda, hakuwa na nia njema katika kutaja majina ya watu wanaohusishwa na dawa za kulevya na kwamba, hafai katika nafasi za utendaji.
Gwajima alisema kutokana na jina lake kutajwa kuwa ni miongoni mwa watu wanaohusishwa na dawa hizo, atajua cha kufanya na kwamba, atamshtaki kwa Rais Magufuli.
“Nimetumiwa ujumbe wa pole kutoka kwa baadhi ya watu, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Wilbroad Slaa na kwamba katika maelezo yake, amesema kuwa licha ya mambo mengine kwa hilo wamekuonea na endapo nikiitwa mahakamani, nitatoa ushahidi,”alisema. 
Aliongeza kuwa hakuna wa kumlaumu kwa jambo hilo kutokana na kuwa hata baadhi ya askari wamo ndani wameshikiliwa, hivyo hao ni watumishi wa serikali kama walivyo wengine na bado hawajatoka.
Askofu Gwajima alisema hana imani na Makonda kama ana uwezo wa utendaji kazi wa nafasi hiyo na kwamba, iwapo itawezekana apangiwe nafasi nyingine.
“Mimi bado sina imani kabisa na kamati aliyoiunda mkuu huyu wa mkoa kutokana na kuwa, yeye ndiye ametaja majina hayo, je kesi ya nyani ukampe ngedele kweli mimi bado sijaona maana,”alisema.
Askofu huyo alishikiliwa na polisi tangu Alhamisi iliyopita, ambapo alifika katika kituo hicho cha kati baada ya kutajwa na Makonda kwenye orodha ya watu 65, kuhusiana na vita dhidi ya dawa za kulevya.

0000

No comments:

Post a Comment