Monday 13 February 2017

NUKUU ZA RAIS MAGUFULI KUHUSU DAWA ZA KULEVYA




“Wale wote waliohukumiwa nje ya nchi, wawe wamehukumiwa kunyongwa au kufungwa maisha, Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi wetu msijihusishe katika kitu chochote. Waacheni wapate wanachostahili. Kama amefungwa kwa dawa za kulenya na akahukumiwa kunyongwa, mwache anyongwe.”

“Pamoja na kwamba sheria ilipitishwa, Waziri Mkuu hakujua kama yeye ni mwenyekiti, alifichwa. Waziri Mkuu kama amejua. basi amejua jana au juzi, kwamba yeye ni mwenyekiti wa baraza linalohusika katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.” 

“Hata mimi sikuletewa mapendekezo ya kumteua Kamishina Jenerali, mpaka nikaamua kumteua. Ni lazima tuzungumze ukweli kwani tukificha, tutajifanya malaika. Sijaletewa na niliamua kuteua mwenyewe. Kwa hiyo mnaweza kujua kwa namna gani vita hii ilivyokuwa kubwa.”

“Tusishabikie shabikie kwa wepesi suala hili la dawa za kulevya. Nimekuwa nikiangalia maneno kwenye mitandao, mengine yanasikitisha sana. Hii ni vita kama zilivyo vita zingine, tusilichukue kimzaha, madhara yake ni makubwa.”

“Sheria namba 5 ya mwaka 2015 tumepewa mamlaka sisi serikali ya kupambana na dawa za kulevya, hatutojali mtu yeyote. Awe mbunge, waziri, mwanasiasa, polisi, mwanajeshi, mtoto, mkubwa, mchungaji, padre au sheikh tutadeal naye. Hili nataka kusema kwa dhati.”

“Nawapongeza wabunge waliopita chini ya Spika mama Anna Makinda. Walikaa bila kujali vyama vyao na kupitisha Sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya. Vilevile nampongeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kupata uchungu kwa Watanzania waliokuwa wakiumia kwa kuweka saini ya matumizi ya sheria hii Mei 11,  2015. Sisi tuna wajibu wa kusimamia, hatutorudi nyuma.”

“Majeshi ya ulinzi na usalama, Jeshi la Wananchi, Polisi, Uhamiaji, TISS, Magereza na Zimamoto, wote mkasimamie kazi hii.”

“Mtu anakwenda kuripoti polisi halafu wengine wanapiga deki gari, kwani mliambiwa hapo ni kwa kusafisha magari? Na polisi mpo hapo! Shika wote na gari ikiwezekana weka rock up. Mtu anapeleka kwaya, mliambiwa mnakwenda kuimbiwa mapambio. I wish I could be IGP. Sasa sitaki kitokee kitu cha namna hiyo. Mambo ya msingi tunaweka mzaha, mbona hawakwenda Lugalo kuimba. Tunataka vyombo vya ulinzi viheshimiwe. Tukileta mzaha tutakuja kujuta.”

No comments:

Post a Comment