Monday, 20 February 2017

MAJALIWA AZINDUA BARAZA LA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NA KUTOA ONYO KALI



MAMLAKA zitakazogundulika zinachukua rushwa na kuwasamehe wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya, zitachukuliwa hatua kali.

Onyo hilo lilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akizindua na kufungua kikao cha Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya, kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali na baraza hilo, hazitahiji kuona mtu yeyote, ambaye ana mamlaka ya kufanyakazi hiyo, kushiriki kwa namna yoyote ili kupokea rushwa kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

"Ikigundulika, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote mwenye mamlaka, ambaye atashiriki kupokea rushwa na kuwasamehe wauzaji wa dawa za kulevya,"alionya.

Alisema watendaji wa mamlaka kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa ameaminiwa, hivyo wawe waadilifu kwani wamekabidhiwa majukumu makubwa yanayohitaji uangalifu wa hali ya juu.

Majaliwa alisema mamlaka itashirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama katika ngazi zote katika vita hiyo. "Vyombo vyetu vya usalama vyote vipo katika ngazi zote, hivyo vina wajibu mkubwa wa kutimiza," alisema.

Aidha, alisema sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya inatakiwa kusimamiwa kikamilifu na masharti yote yaliyotajwa yatekelezwe bila kumwonea mtu yeyote.

Waziri Mkuu alisema uanzishwaji wa taasisi zote zilizotajwa na sheria, ukamilishwe mapema ili kukiwezesha chombo hicho kufanyakazi zake ipasavyo hadi ngazi ya chini na kuleta ufanisi.

Alisema wakuu wa mikoa wanayo kazi kubwa katika vita hiyo, wakiwa kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama.

"Mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu," alisema.

Waziri Mkuu alisema wakuu wa wilaya, watendaji wa kata na vijiji, wanahusika moja kwa moja kushiriki kuwakamata watumiaji wa dawa za kulevya.

Pia, aliwataka wakuu wa mikoa na watendaji wote, kuwahamasisha wananchi ili waweze kutoa  ushirikiano katika kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili uchunguzi ufanywe na kuwatia hatiani wahusika.

"Jiepusheni kuwatangaza watuhumiwa kabla hatujafanya uchunguzi," alisema.

Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa baraza hilo, alisema limeanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na 5 ya mwaka 2015.

Majaliwa alisema wajumbe wa baraza hilo kwa mujibu wa sheria husika ni Waziri Mkuu, ambaye anakuwa mwenyekiti na katibu, ambaye ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Wajumbe waliomo kwenye baraza hilo ni Waziri wa Sheria na Katiba; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje; Waziri wa Fedha; Waziri wa Elimu; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Ulinzi.

Wengine ni makatibu wakuu, wakuu wa mikoa waliopo kwenye mikoa, ambayo ni miji na wale ambao mikoa yao ipo mipakani.

"Mawaziri wengine wanaweza kukaribishwa kutegemeana na ajenda ya kikao," alisema.

Aidha, alisema baraza linaweza kumkaribisha mtu yeyote mwingine aliye mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Akizungumzia kuhusu kukamatwa kwa dawa za kulevya, alisema kuanzia Januari 2015 hadi Desemba 2016, vyombo vya dola vilikamata kilo 77 za heroine, zikihusisha kesi 703 na kilo 32.3 za cocaine, zikihusisha kesi 259.

Pia, alisema juma ya kilo 78,656.179, za bangi zilikamatwa zikihusisha kesi 14,323 na ekari 71 za mashamba ya bangi ziliteketezwa kwa kipindi hicho.

"Vilevile, katika kipindi hicho, mirungi kilo 31,463.615 ilikamatwa ikihusisha kesi 2,362," alisema.

Alisema vifaa vya utambuzi vimetolewa katika mipaka ya Tunduma, Kasumulu, Namanga, Horohoro na Mtukula kwa ajili ya kukabiliana na dawa hizo.

Aliongeza kuwa, serikali imeendelea kutoa matibabu kwa kutumia dawa ya methadone kwa watumiaji wa dawa za kulevya aina ya heroine.

"Taarifa zinaonyesha kuwa, watumiaji zaidi ya 2,223, wanapata huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke," alisema.

Aidha, alisema huduma za nyumba za upataji nafuu zipatazo 11, kwa Tanzania Bara zinatolewa na hadi sasa zimehudumia waathirika 2,325.

"Kwa upande wa Zanzibar, kuna nyumba 12, ambazo hadi sasa zimehudumia waathirika wapatao 7,953," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, chini ya Ibara ya 155, inaitaka serikali kuongeza jitihada za kupambana na dawa za kulevya kwa kuanzisha Mamlaka ya Kuzuia Dawa za Kulevya.

No comments:

Post a Comment