Monday 20 February 2017

MAOFISA WAWILI TRA WANASWA



VITA dhidi ya dawa za kulevya sasa vimeibukia kwa maofisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao wamekamatwa kwa kuingiza kemikali bashirifu aina ya ephedrine, zinazotumika kutengenezea heroine.

Aidha, watumishi wengine wawili wanaendelea kuchunguzwa kwa madai ya kujihusisha na uingizwaji wa kemikali hizo, ambapo kwa sasa wanafuatiliwa kwa umakini.

Maofisa hao wawili wa TRA, ambao wamekamatwa kwa kujihusisha na upitishwaji wa kemikali hizo, watafikishwa mahakamani muda wote kuanzia sasa.

Hata hivyo, taarifa ya Mamlaka ya Kazuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema endapo itabainika kuwa vituo vya kuhudumia watu wenye uraibu wa dawa hizo, ambavyo vinaendelea kutumia dawa hizo, vitachukuliwa hatua kutokana na kukiuka sheria ya uanzishwaji wa vituo hivyo.

Akizungumza jana, mjini Dar es Saalam, kuhusu mwenendo wa operesheni ya kukamata dawa za kulevya nchini, Kamishna wa Operesheni Mamlaka ya Kazuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Mskhela, alisema imefanikiwa kubaini maeneo yanayopatikana dawa hizo katika mikoa mbalimbali.

Kamishna Mihayo alisema katika operesheni hizo, Morogoro wamekamata kete tatu za heroine, Lindi kete 50, Singida kete moja na Songwe kete 274.

“Operesheni hii imefanyika kwa juhudi kubwa huku mkoa wa Simiyu, Tarime na Rorya, zikiongoza kwa dawa za kulevya za mashambani, ambapo tumeteketeza ekari 40 hadi 36 za bangi,”alisema.

Mihayo aliongeza kuwa, katika operesheni hiyo, mikoa na maeneo ambayo wamekamata dawa hizo ni Tanga, Morogoro, Shinyanga, Kagera, Njombe, Songwe, Tabora, Singida, Rukwa, Mbeya, Kigoma, Lindi, Simiyu, Ruvuma, Tarime na Rorya.

Kamishna Mihayo alisema kasi bado inaendelea kuwasaka watu wanaojihusisha na baishara ya dawa hizo za kulevya, wakiwemo wasafirishaji,wasambazaji na watumiaji.

Alisema katika orodha ya majina yaliyotajwa kujihusisha na dawa hizo za kulevya, hatapona mtu iwe mtoto wa kigogo, wafanyabiashara au yeyote na kwamba, katika vita hiyo, hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe lingine.

“Nipongeze kazi nzuri zilizofanywa na wakuu wa mikoa na kamati za ulinzi na usalama kwa jitihada kubwa walizoonesha katika kupambana na kupiga vita dawa za kulevya. Ninawaomba wananchi watoe taarifa za kufanikisha vita hii, ”alisema.

Hata hivyo, alisema hatoweza kutaja majina ya maofisa hao wa TRA, kutokana na kuwa upelelezi bado unaendelea na kwamba, utaratibu wa kuingiza kemikali unahusisha ofisi ya Mkemia Mkuu na TRA.

Kamishna huyo aliendelea kusema kuwa, operesheni hiyo imefanikiwa kuyabaini mashamba yanayolima dawa hizo za kulevya za mashambani aina ya bangi na mirungi na kuyaharibu.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo la kushughulikia orodha ya majina ya mahakimu na majaji, ambao walikuwa wakichelewesha kesi za dawa za kulevya, alisema upo katika hatua nzuri na kwamba, muda wowote yatawasilishwa mahala husika.

Mihayo alisema kitendo cha kutaja majina na kutotaja majina kwa watu ambao wanadaiwa kujihusisha na dawa hizo, ni mifumo tu ya kujiridhisha katika makosa, ambayo mengine yako wazi na upande mwingine yamejificha.

No comments:

Post a Comment