Friday 17 February 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA ONYO KALI KWA WANAHARAKATI WACHOCHEZI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haitakubali kuona watu wachache wanachochea vurugu na kusababisha watu wengine wapoteze maisha ilhali wao hawadhuriki.

Alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa mjini Kibaya, wilayani Kiteto, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu, ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani Manyara, alisema: “Hatutakubaliana na wachochezi. Hatutakubaliana na yeyote atakayesababisha kifo. Tukibaini kuna uchochezi, tutawasaka wahusika na kuwashughulikia.”

“Hapa kulikuwa na majina ya ajabuajabu, hatutakubali Kiteto iitwe Soweto au Kossovo, hapa ni Tanzania. Hatuwezi kuishi kwa kubaguana, ni lazima tuheshimu maamuzi ya wazee wetu wa kimila, ambao wamesimamia zoezi hili ili kurejesha amani ya Kiteto,” alisema.

Alisema zamani Kiteto kulikuwa hakuna lugha ya amani, lakini hali kwa sasa imebadilika na kuwa nzuri na akasisitiza kwamba, hakuna kurudi nyuma.

Alisema anamshukuru Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kwa kufuatilia suala hilo na kuunda tume ya kutafuta amani wilayani Kiteto.

“Nilipoingia madarakani, nami nilianza kufuatilia suala hilo ili nijue chanzo hasa ni nini. Nikabaini kuwa mgogoro mzima umechangiwa na chokochoko tu za watu wachache,” alisema.

Mapema, viongozi wa kimila walimkabidhi Waziri Mkuu rungu, jembe dogo na jani la mti wa asili (kimasai unaitwa elisibie), ikiwa ni ishara ya amani ya kukomesha mapigano baina ya wafugaji na wakulima. Pia alishiriki dua ya kuombea amani, ambayo iliongozwa na viongozi wa dini.

Mzee Mbambile Oloi Kurkur (65), ambaye amejiita ni msimamizi wa mila za Kimasai, alisema Mungu yuko na anaweza kusimamia na kudumisha amani ambayo wameiombea.

Alisema Mungu ameumba mti wa ajabu, ambao haukauki kwa mwaka mzima na majani hubaki ya kijani hata wakati wa kiangazi kikali. “Jani hili tunakukabidhi ikiwa ni ishara ya makubaliano yetu kuwa ya kudumu,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Amani la Wilaya ya Kiteto, Mzee Abubakar Mrisho, alisema kamati hiyo iliundwa na wazee 70, ambao walipita katika tarafa saba za wilaya hiyo na kutoa elimu kwa wakazi wa vijiji vyote 23, juu ya umuhimu wa kudumisha amani.

Ili kuhitimisha kazi yao, Mzee Mrisho alimweleza Waziri Mkuu kwamba, juzi asubuhi, waliwachagua wazee kutoka makabila manne ya Wamasai, Wanguu, Wakamba na Wagogo ili wawakilishe makabila yote ya wilaya hiyo kwenye tambiko la kuoza ardhi.

“Baada ya tambiko, tulitoa tamko la Baraza la Amani kwamba, mauaji hapa Kiteto sasa basi.Yeyote atakayeona anabanwa, Kiteto haina nafasi naye tena,” alisema.

Kwa upande wao, viongozi wa dini walitumia mkutano huo wa Waziri Mkuu kuomba dua kwa ajili ya kuombea amani, haki, vita dhidi ya rushwa, ufisadi na dawa za kulevya na pia kuombea mvua ya kiasi na yenye kuleta neema.

Askofu Isaiah Chambala wa CCT, alimuomba Mungu awashe moyo wa upendo, amani na udugu miongoni mwa wakazi wa Kiteto, mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla.

Padre Filbert Moita wa Kanisa Katoliki, aliombea kuwe na haki na amani kwa watu wote na Mungu awasaidie watu wake ili waheshimiane kidugu katika wilaya hiyo na mkoa mzima.

Mwalimu Juma Hicha wa BAKWATA mbali ya kuombea amani wilayani humo, aliwaombea viongozi wa kitaifa wapewe hekima ya kuongoza nchi na Mungu awajalie nguvu ya kupambana na ufisadi, dhuluma na dawa za kulevya na zaidi ya yote Mungu awatie nguvu ya kuikamilisha vita hiyo.

No comments:

Post a Comment