Friday 17 February 2017

JELA MAISHA KWA DAWA ZA KULEVYA


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi imewahukumu kifungo cha maisha jela watuhumiwa sita waliokuwa wakikabiliwa na shitaka la kusafirisha dawa za kulevya.

Kati ya watuhumiwa hao, wanne ni raia wa kigeni.

Aidha, mtuhumiwa mmoja amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Raia wa kigeni waliohukumiwa kwenda jela maisha ni Vivian Edigin, raia wa Italia ambaye ni ni mzaliwa wa Nigeria, Joachimu Ikechukwu Ike (Nigeria), Josiani Creppy (Togo) pamoja na Josephine Waithera (Kenya).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Benard Mpepo, alisema katika kipindi cha mwaka 2015, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ilitoa hukumu ya kesi mbili za kusafirisha dawa za kulevya.

Mpepo alisema kesi ya kwanza ilikuwa ikimuhusu Edigin dhidi ya jamhuri, ambapo mtuhumiwa alitiwa hatiani na kosa la kusafirisha dawa za kulevya na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela, ambapo hukumu hiyo ilitolewa Juni 29, mwaka 2015.

Naibu Msajili huyo alisema kesi ya pili ilikuwa ikiwahusu watuhumiwa watatu dhidi ya Jamhuri, ambapo wawili waliachiliwa huru kutokana na kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani, huku mtuhumiwa mmoja aitwaye Mussa Mgonja ambaye ni Mtanzania akitiwa hatiani na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela, Januari 27, mwaka jana.

“Katika kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa pande zote, kesi nyingine ya kusafirisha dawa za kulevya tuliyoisikiliza mwaka jana ilikuwa ni ya Slahi Jumanne dhidi ya jamhuri, ambapo naye alihukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela Machi 17, mwaka jana,”alisema.

Katika kesi nyingine ya kusafirisha dawa za kulevya iliyohukumiwa Januari 27, mwaka jana, alisema raia wa Kenya, Josephine Waithera alihukumiwa kifungo cha maisha jela, huku raia wa Togo, Creppy naye akihukumiwa kutumikia kifungo kama hicho Juni 8, mwaka huo.

Mpepo alibainisha kuwa, raia mwingine wa Nigeria, Ike, alihukumiwa kifungo cha maisha jela Juni 10, mwaka jana, huku Mtanzania Sofia Seif Kingazi akihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, Juni 15, mwaka jana.

Alisema kesi nyingine ya kusafirisha dawa za kulevya iliyokuwa ikimkabili Salimu Mohamedi Salimu ilifutwa Juni 29, mwaka 2015, chini ya kifungu cha sheria namba 91, ambacho kinaruhusu mtuhumiwa kukamatwa na kurejesha mahakamani kuendelea na kesi kama kunaumuhimu ambapo Jamuhuri ilifanya hivyo na kesi yake inaendelea kusikilizwa.

Naibu Msajili huyo alibainisha kuwa kwa sasa zipo kesi sita za dawa za kulevya na nne za mauaji zinazoendelea kusikilizwa ambapo inatarajiwa ifikapo Machi 2, mwaka huu, zitakuwa zimeshatolewa hukumu.

Akizungumzia pia kesi za dawa za kulevya zilizopokelewa mahakamani hapo katika kipindi cha mwaka huu, Mpepo alisema kuwa hakuna hata kesi moja iliyosajili.

No comments:

Post a Comment