Friday, 17 February 2017

DAR YAONGOZA KWA MAPENZI YA JINSIA MOJA


MKOA wa Dar es Salaam unaongoza kwa idadi kubwa ya wapenzi wa jinsia moja, vitendo vya ukahaba na maambukizi ya virusi vya ukimwi vinavyochangiwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, serikali imevifungia vituo vyote vinavyojihusisha na utoaji huduma kwa makundi maalum na waathirika wa ukimwi kwa sababu vimebainika kuchochea mapenzi ya jinsia moja.

Takwimu hizo zimeifanya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kusema itahakikisha inahamasisha wananchi kuzingatia maadili kwa sababu mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha katiba na sheria za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema katika kukabiliana na vitendo wizara hiyo itashirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kudhibiti vitendo hivyo.

Waziri Ummy alisema maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa makundi maalum nchini yameongezeka kwa kasi ikilinganishwa na wastani wa kiwango cha maambuzi kwa nchi nzima.

“Ili kupunguza maambukizi ya ukimwi nchini na kutokomeza ukimwi duniani ifikapo mwaka 2030 ni dhahiri kuwa tuna wajibu wa kuweka mipango na mikakati ya kupambana ukimwi kwa makundi hayo.

“Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya ukimwi na malaria wa mwaka 2011/12, wastani wa kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi miongoni mwa watu wenye umri kati ya miaka 15 - 49 ni asilimia 5.1 (5.1%). Hii inamaanisha kuwa katika kila watu 100, watu 5 wanaishi na maambukizi ukimwi,”alisema.

Aidha, alieleza kuwa watu milioni 1. 3 wanaishi na ukimwi. Kati yao, watu 839,574 wanapata dawa za kudumaza virusi hivyo katika vituo 4,737 vinavyotoa huduma katika halmashauri mbalimbali nchini, kwa mujibu wa takwimu kwa kipindi kinachoishia Juni mwaka jana.

Kwa mujibu wa utafiti uliopo, unaonyesha hali ya maambukizi ya virusi hivyo kwa makundi maalum yaliyopo kwenye hatari zaidi ya maambukizi iko juu ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 5.1.

“Maambukizi hayo yanaonyesha kuwa, miongoni mwa watu wanaotumia dawa ya kulevya kwa kujidunga sindano ni asilimia 36, ambapo Dar es Salaam inaongoza, huku Mwanza ikiwa chini ya matukio hayo, wanawake wanaofanya biashara ya ngono ni asilimia 26 huku Dar es Salaam, Mwanza na Shinyanga zikiongoza.

“Wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao ni asilimia 25, huku Dar es Salaam, Dodoma na Tanga zikiongoza,” alisisitiza.

Alisema uchunguzi uliofanywa na kikosi kazi maalumu cha serikali cha kufuatilia uwezekano wa kuwepo kwa shughuli za kuhamasisha uhusiano wa kingono wa jinsia moja ulibaini kuwa mbali na kufanya shughuli za mapambano dhidi ya ukimwi, baadhi ya wabia walikuwa wakifanya shughuli za kuhamasisha vitendo hivyo.

“Ninaagiza mamlaka zote za utoaji huduma za afya kuhakikisha kuwa huduma za ukimwi zinapatikana kwa mtu yeyote nchini bila ubaguzi wa aina yoyote kwa kuwa ubaguzi katika utoaji wa huduma za afya nchini ni kinyume cha sheria, sera na utaratibu wa nchi.

“Serikali inasisitiza kuwa huduma za afya, ikiwemo huduma za ukimwi kwa makundi maalumu bado zinaendelea kutolewa bila malipo kwa wahitaji wote bila ubaguzi au unyanyapaa na endapo mtu yeyote, hususan katika makundi maalum atakosa huduma, asisite kutoa taarifa kwa mganga mkuu wa halmashauri husika,” alieleza.

Waziri huyo alisema utaratibu wa awali wa kutoa huduma hizo kwa makundi maalum kutumia vituo maalum  hautatumika tena na wizara haitatambua vituo hivyo maalum.

No comments:

Post a Comment