Friday, 17 February 2017

MASOGANGE APELEKWA KWA MKEMIA MKUU KUPIMWA


MWANAMITINDO maarufu, Agnes Gerald (Masogange) na wenzake 17 watafikishwa mahakamani leo, endapo vipimo vikibainisha wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha askari tisa kati ya 12 wanaokabiliwa na tuhuma za dawa za kulevya wamekabidhiwa  kwa  Kamishna Mkuu wa mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za Kulevya nchini, kwa ajili ya kuhojiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Saimon Sirro, alisema mwana mitindo huyo na wenzake 17, jana  walipelekwa  kwa mkemia mkuu wa serikali, kufanyiwa vipimo.

Sirro alisema baada ya kuchukuliwa vipimo hivyo, kisha kubainika wanajihusisha na matumizi ya dawa hizo, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Alisema watu hao tayari walishahojiwa na kupekuliwa kwenye makazi yao.

“Tumewapeleka  Masogange na wenzake 17 kwa  mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya vipimo na tunatarajiwa kuwafikisha mahakamani kesho (leo) haraka iwezekanavyo pindi  vipimo vitakapobaini wanajihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya,” alisema Sirro, lakini alikataa kutaja majina ya watuhumiwa wengine hao.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paulo Makonda  katika vita dhidi ya dawa za kulevya aliwataja baadhi ya watu, wakiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Hata hivyo, Askofu Gwajima aliachiwa na polisi huku Mbowe akigoma kwenda kuripoti.

Pia, Sirro alisema hadi sasa tayari wameshawakabidhi askari tisa kwa kamishna mkuu  wa mamlaka inayohusika kupambana na dawa za kulevya kwa ajili ya kuhojiwa.

Askari hao ni PF. 14473 SACP  Christopher Fuime, PF .17041 Inspekta Jacob Hashimu Swai, D.3499 D/SGT Steven Apelesi Ndasha, E.8431 D/SGT 8431 Mohamed Juma Haima, E.5204 D/SGT Steven John Shaga, E.5860 D/CPL Dotto Steven Mwandambo, E.1090 D/CPL Tausen Lameck Mwambalangani.

Wengine ni E.9652 D/CPL Benatus Simon Luhaza, D.8278 D/CPL James Salala, E.9503 D/CPL Noel Masheula Mwalukuta,WP.5103 D/C Groria Mallya Masawe na F.5885 DC Fadhili Ndahani Mazengo.

Katika tukio lingine, kamshina huyo alitangaza kukamatwa kinara wa kusamabaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii, Omary Bakari (23), ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mkazi wa JKT, Mgulani.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Februari 15, mwaka huu baada ya askari kumweka mtegoni ambapo alisambaza taarifa za uongo kwenye mitandao wa facebook kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametaja majina mengine ya watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Katika orodha hiyo, mtuhumiwa huyo alisema wapo wanasiasa na viongozi wa dini ambapo alikiri kuwa taarifa hizo aliziona kwenye kundi la mtandao wa mashabiki wa yanga, hivyo alimua kuzisambaza.

“Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kosa la kutoa taarifa za uongo kama ilivyoainishwa kwenye kifungo cha sheria namba 16 cha mitandao ya mwaka 2015,’ alieleza.

Kamanda Sirro alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na tabia hizo waache kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

No comments:

Post a Comment