Friday, 17 February 2017

MANJI KIZIMBANI


MFANYABIASHARA  maarufu nchini, Yussuf Manji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

Manji alifikishwa mahakamani hapo jana saa 7.58 mchana, chini ya ulinzi wa polisi akitokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, alikokuwa amelazwa siku tatu.

Alilazwa akitokea mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Kati, Dar es Salaam.

Manji ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya mpira ya Yanga, alipandishwa kizimbani ikiwa ni siku ya saba tangu ashikiliwe na polisi baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa wanaohusika na dawa za kulevya.

Alipofikishwa mahakamani hapo, aliwekwa katika chumba cha mahabusu hadi ilipofika saa 8.58 mchana, alipopandishwa kizimbani  mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka nchini, Oswald Tibabyekomya, aliongoza jopo la mawakili wa serikali waandamizi, Shadrack Kimaro na Mutalemwa Kishenyi katika shauri hilo, ambapo Karani Sarah Mlokozi alimsomea Manji shitaka.

Karani Sarah alidai Manji anakabiliwa na shitaka la kutumia dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 17(1)(a) cha sheria ya dawa za kulevya.

Alidai tarehe tofauti Februari 6 na 9, mwaka huu, maeneo ya Upanga Sea View, wilayani Ilala, Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alitumia dawa za kulevya  aina ya heroin.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Mkeha alimtaka mshitakiwa huyo kujibu kama si kweli au hapana, ambapo Manji alijibu ‘no umekosea, siyo kweli’.

Wakili Tibabyekomya alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Jopo  la mawakili linalomtetea Manji likiongozwa na Alex Mgongolwa akishirikiana na Hudson Ndusyepo na Jeremiah Ntobesya, waliomba mshitakiwa apewe dhamana kwa kuwa kosa linalomkabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria.

“Ukiangalia kwa uzito wake, tunaomba mshitakiwa apatiwe masharti nafuu, ikizingatiwa mshitakiwa ana dhamana ya watu kwa kuwa ni diwani na mfanyabiashara, hivyo ikiwezekana hata ajidhamini mwenyewe kwa sababu dhamira ya dhamana ni kuhakikisha anafika mahakamani pindi kesi itakapotajwa,” aliomba.

Hakimu Mkeha alisema upande huo kwa kufanya hivyo, unakuwa unajiwekea masharti ya dhamana, ambapo Mgongolwa alidai wanasisitiza tu.

Wakili Tibabyekomya alidai shitaka linalomkabili Manji linadhaminika. Hakimu Mkeha alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka mfanyabiashara huyo kutia saini dhamana ya sh. milioni 10 na kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayetia saini kiasi hicho cha dhamana.

Baada ya hakimu kutoa masharti hayo, Katibu Mkuu wa Yanga African, Charles Mkwasa, alijitokeza kumdhamini kiongozi wake na kukabidhi barua na kitambulisho chake. Hakimu  alisema Mkwasa anakubaliwa kumdhamini Manji na kuahirisha shauri hilo hadi Machi 16, mwaka huu kesi itakapotajwa.

Manji aliondolewa katika chumba cha mahakama saa 9.17 alasiri na kupelekwa mahabusu kusubiri kukamilisha utaratibu wa dhamana.

ARUDISHWA MUHIMBILI


Saa 9.23 alasiri, Manji alikamilisha utaratibu wa dhamana kwa kutia saini, karatasi za dhamana.

Baada ya kukamilisha utaratibu huo, mawakili wake walisikika wakisema kwamba anatakiwa arudishwe hospitali kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

“Gari lipo huku,  anatakiwa arudishwe hospitali kwa matibabu,” alisema wakili Ntobesya, huku mashabiki na wapenzi wa Yanga waliokuwa wamefurika mahakamani hapo wanaume kwa wanawake wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kiongozi wao huyo kuachiwa kwa dhamana.

Manji aliondolewa mahakamani hapo kupelekwa hospitali kwa kutumia gari aina ya Hummer, lenye namba za usajili T 670 BBX, ambalo lilikuwa ni miongoni mwa magari matatu yaliyokuwa yamefuatana, likiwemo la polisi wakati akifikishwa mahakamani hapo.

Kuachiwa kwa dhamana kwa mfanyabiashara huyo, kuliamsha shangwe kwa mashabiki na wapenzi wa Yanga, ambao walikuwa wakiondoka, huku wakiimba.

Mfanyabiashara huyo alifikishwa mahakamani hapo baada ya kuwa miongoni mwa watu 65 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakihusishwa na dawa za kulevya.

Februari 8, mwaka huu, Makonda alitaja awamu ya pili ya watuhumiwa wanaohusika na dawa za kulevya, akiwemo Manji ambao aliwataka wafike polisi Februari 10, mwaka huu.

Hata hivyo, siku hiyo hiyo baada ya Manji kutajwa jina lake, aliitisha mkutano na waandishi wa habari saa tisa alasiri na kuzungumzia tuhuma hizo na kudai hausiki kwa namna yoyote.

Akizungumza katika mkutano huo, Manji alidai hausiki na dawa za kulevya kwa namna yoyote si kwa kutumia au kuuza.

Alidai kutokana na kutajwa yuko tayari kupimwa au kupekuliwa ili kubaini iwapo anahusika na dawa hizo na endapo akikutwa hana chochote, mamlaka husika zitangaze hadharani kama ilivyomtangaza.

Mbali na hayo, Manji alitishia kumfikisha mahakamani Makonda kwa kile alichodai  amemdhalilisha kwa kumtaja katika orodha ya watu wanahusishwa na dawa za kulevya.

Manji alisema yeye ni mtu mwenye heshima kubwa kwenye jamii, ambapo kwa muda mrefu amekuwa akiisaidia jamii kwa mambo mbalimbali.

"Mimi nina nafasi mbili kwenye jamii, mimi ni mwenyekiti wa klabu kubwa ya soka nchini, Yanga pia ni diwani, kunihusisha na tuhuma ambazo bado hazijathibitishwa ni kunikosea heshima,'' alisema na kuahidi kufika kituoni hapo siku iliyofuata.

Februari 9, mwaka huu, Manji alitimiza ahadi yake na kwenda kuripoti polisi asubuhi ambapo baadaye alionekana anatoka kituoni hapo lakini ghafla aizuiwa na polisi.

Tangu siku hiyo, Manji alikuwa mahabusu, ambapo Jumapili iliyopita, alionekana akiondolewa katika gari la wagonjwa na kupelekwa Muhimbili katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa matibabu.

Manji aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo jana, hata hivyo taarifa zilizopatikana zilieleza kwamba asubuhi kabla ya kufikishwa mahakamani hapo hali yake ilibadilika, hivyo alirudishwa hospitali, ndipo mchana akapandishwa kizimbani na kurudishwa tena hospitali baada ya kuachiwa kwa dhamana.

Mfanyabiashara huyo akiwa anashikiliwa na polisi, Jumanne wiki hii, Idara ya Uhamiaji, mkoa wa Dar es Salaam, ilimtaka mmiliki huyo wa Quality Plaza, kuripoti uhamiaji mara baada ya kutoka hospitali kutokana na kubainika ameajiri raia wa kigeni 25 bila ya kuwa na vibali vya kufanyia kazi nchini.

No comments:

Post a Comment