Sunday, 26 February 2017
VIGOGO WANNE SHIRIKA LA POSTA WATUMBULIWA
BODI ya Shirika la Posta Tanzania, imewasimamisha kazi watendaji wakuu wanne wa shirika hilo kwa tuhuma za ubadhilifu, wizi na kufanya kazi kwa mazoea.
Imedaiwa kuwa baadhi ya watendaji wakuu kutoka makao makuu ya shirika hilo, Dar es Salaam, wamekuwa kikwazo katika dhana ya uwajibikaji, weledi na kujituma wakati wa kutekeleza wajibu na majukumu yao ili kuwa mfano bora katika kutoa huduma.
Watendaji waliosimamishwa kazi ni pamoja na Meneja Mkuu Rasilimali za Shirika, James Sando. Nafasi yake imechukuliwa na Macrice Mbodo.
Bodi hiyo pia imemsimamisha kazi Meneja Mkuu Uendeshaji Bishara, Janeth Msofe, ambapo nafasi yake kwa sasa itakaimiwa na Hassan Mwang’ombe.
Wengine waliosimamishwa ni Meneja Msaidizi wa Mali na Logistic, Jasson Kalile na Msimamizi wa Usafirishaji, Ambrose John, wote kutoka makao makuu ya posta.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Luteni Kanali mstaafu Harun Kondo, alisema hivi sasa shirika linao wafanyakazi 1,082, kwa takwimu za hadi Desemba, mwaka jana, lakini baadhi yao wanafanya kazi kwa mazoea na kusema ni lazima wabadilike ili lirudi katika hali yake.
Alisema hatua hiyo inatokana na ufatiti wa muda mrefu uliofanywa juu ya shirika hilo na kubaini kuwa madai ya ubadhirifu na wizi unaofanywa na watendaji hao ni kweli.
"Bodi ilikaa juzi na kupitia kwa umakini utendaji, uwajibikaji, nidhamu na uwezo wa watendaji wakuu wa shirika, ambao wanatakiwa kuwa mfano bora wa uongozi na utendaji,"alisema.
Pia, aliitaka menejimenti kuendelea kusimamia uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa kada zote ndani ya shirika hilo ili kujenga nidhamu ya kazi, kujituma, kuheshimu kanuni na utaratibu uliowekwa.
Luteni Kanali Kondo alisema hivi sasa wanahitaji zaidi wafanyakazi wenye kuongeza ubunifu na kufanyakazi kwa ufanisi wenye tija kwa shirika.
Aidha, alisema hivi sasa shirika limeanza kuwapima wafanyakazi wake kwa kutumia mfumo wa wazi wa kazi (OPRAS), kuanzia mwaka huu wa fedha na wafanyakazi watakaobainika kufanya kazi chini ya viwango, lazima wawajibishwe.
“Hatuwezi kufanya kazi na mtumishi asiyefuata utaratibu na sheria za kazi, yeyote atakayekiuka sheria za shirika la posta, atasimamishwa kazi kwa mujibu wa sheria,”alisema Kondo.
Wakati huo huo, shirika hilo limesema limechukua hatua mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kudhibiti dawa za kulevya.
Kondo alisema hivi sasa wamedhamiria kuongeza msukumo na kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu, ambao una madhara makubwa kwa jamii hususan vijana.
Alisema shirika limeamua kusimika mfumo wa kisasa wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa shirika.
Kondo alisema mfumo huo unagharimu zaidi ya sh. milioni 200 na kujumuisha ufungaji wa kamera za usalama (CCTV), makao makuu, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment