SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema imeanza rasmi safari ya kuimarisha uchumi kupitia nishati ya mafuta na gesi asilia.
Imesema hatua hiyo inachukuliwa na kuwaziba mdomo wale wote waliokuwa wakisema hakuna jambo lolote litakalofanyika katika jitihada za kuchimba mafuta na gesi asilia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alisema hayo jana, wakati akizindua ndege maalumu ya Kampuni ya Bell Geospace ya kufanya utafiti wa awali ili kubaini kama kuna nishati hiyo ya mafuta na gesi asilia au la.
Balozi Idd alisema ndege hiyo inaanza kufanya utafiti wake kwenye eneo la Zanzibar na baada ya muda majibu yatapatikana, hivyo kuwasihi wananchi kutoa ushirikiano.
“Wengi walitubeza hadi kudharau ile saini ya Rais wa Zanzibar Dk. Shein ya kuanzisha Sheria ya Mafuta na Gesi Zanzibar, wakisema haina mpango wowote kwani hatuna ubavu wa kuchimba nishati hiyo. Hatukuvunjika moyo wala kukata tamaa, kwani tulikuwa tunafanya jambo ambalo tuna uhakika nalo," alisema.
Akitoa historia ya kuanza kwa maandalizi ya mchakato huo, alisema ulianza miaka mingi iliyopita, lakini miaka ya hivi karibuni, SMZ kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), zilikaa na kujadili jambo hilo chini ya Dk. Shein na Rais mstaafu Jakaya Kikwete hadi kulipatia ufumbuzi.
Balozi Idd alisema vuongozi hao walitumia busara za kuhakikisha unapelekwa muswada wa sheria bungeni ili upitishwe na Zanzibar ianze kuchimba yenyewe rasilimali hizo.
Alisema kazi ya utafiti wa mafuta na gesi asilia itafanywa na Kampuni ya RakGas kutoka Dubai, ambapo shughuli za utafti zitasimamiwa na Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, ikitumia ndege kukagua miamba iliyoko chini ya ardhi, ambapo kwa kitaalamu kazi hii inajulikana 'Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey (FTG)'.
Kampuni hiyo ya kigeni, inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya Brunswick Zanzibar Limited, ambayo inahusika na shughuli za uombaji wa vibali kutoka serikalini kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Aidha, alifafanua kuwa kuna kampuni nyingi za kimataifa kutoka Canada, China na Marekani, zilikuwa zinawania zabuni hiyo, lakini RakGas ambayo imeajiri kampuni ya kufanya utafiti wa awali ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, ilifanikiwa kuipata.
Hata hivyo, Balozi Idd alisema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuondoa dhana kuwa, kupatikana kwa nishati ya mafuta na gesi kutamaliza changamoto na matatizo yote ya kiuchumi, badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha uchumi wa nchi, na kama nishati hiyo ipo, iwe nyongeza ya kuisogeza nchi mbele kimaendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Maji Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alifafanua kuwa ndege hiyo inavyo vifaa vya kitaalamu vitakavyokusanya taarifa zinazohusiana na masuala ya mafuta na gesi.
“Nawaomba wananchi wasiwe na hofu pindi ndege hii itakapokuwa inafanya kazi zake kwani itaruka karibu na makazi ya watu, hivyo itakuwa inazunguka sehemu mbalimbali Pemba na Unguja.
“Ndege hii itaruka karibu na mgongo wa dunia kwa wastani wa mita 80 hadi 120, kutoka usawa wa bahari kwa maeneo ya nchi kavu na baharini,”alisema Waziri Salama.
Kwa mara ya kwanza, kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ulifanyika Zanzibar mwaka 1952, ambapo utafiti huo ulionyesha kuwepo kwa dalili za mafuta.
No comments:
Post a Comment