Sunday 30 July 2017

RAIS MAGUFULI AMTOLEA UVIVU MBUNGE WA CCM MORO MJINI

RAIS Dk. John Magufuli amewataka watu wote waliobinafsishiwa viwanda mbalimbali katika mkoa wa Morogoro, kuvirejesha serikalini endapo wameshindwa kuviendeleza ili wapewe wawekezaji wanaoweza kuviendeleza na kuzalisha ajira.

 Agizo hilo alilitoa jana, baada ya msafara wake uliokuwa ukitokea Dodoma kuelekea Jijini Dar es Salaam, kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu.

“Ninarudia wito wangu niliokwishakuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro, ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nawataja, akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wavirejeshe.

"Narudia tena, akiwemo Mbunge wa hapa wa CCM, ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha, avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu," alisisitiza.

Aliwapongeza wakulima wa mazao mkoani humo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na amewapongeza wakulima wa wilaya ya Kilosa, kwa kuongeza uzalishaji kutoka asilimia 42, msimu uliopita hadi kufikia asilimia 82 katika msimu huu.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi, lakini amewataka waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa mkoa huo, kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa mji huo kuendelea kufanyabiashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.

Wananchi hao walimueleza Rais Magufuli kero yao ya kunyanyaswa na manispaa, ambao wamekuwa wakiwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara, hasa baada kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.

Pia, Rais Magufuli alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Onesphory Matei, kuhakikisha askari mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo.

Vilevile, aliwataka wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.

Mbali na Morogoro, Rais Magufuli pia alizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake eneo la Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Rais Magufuli aliwahakikishia kuwa, serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na kero na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Tegeta, nianze kwa kuwashukuru sana kwa kura nyingi mlizonipa ili niwe Rais wa awamu ya tano. Nawashukuru CCM, nawashukuru CHADEMA, nawashukuru CUF, na ACT na hata wale, ambao hawana chama kwani wote kwa umoja wenu mlitanguliza maslahi ya Taifa na kumpa kura mtu ambaye atalisaidia Taifa.

"Na mimi nitafanyakazi kwa nguvu zangu zote na kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu ili Watanzania wote, hasa wanyonge, ambao siku zote walikuwa wakionewa," alisema.

Baadhi ya juhudi alizozitaja kufanyika tangu aingie madarakani ni pamoja na kuondoa ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka sh. bilioni 371, hadi kufikia sh. bilioni 483, kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kulinda mali za umma hasa madini.

Vilevile, Rais Magufuli aliipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kwa kuzuia udahili wa wanafunzi wote wa mwaka kwanza katika vyuo vikuu 19 na kuzuia udahili wa wanafunzi wa kozi 75, katika vyuo vikuu 22, kutokana na dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa ubora vyuo hivyo uliofanyika Oktoba, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment