Sunday, 30 July 2017

MARAIS WASTAAFU WAUFAGILIA UONGOZI WA JPM


RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amesema viongozi wastaafu wanauthamini uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, kutokana na utendaji kazi wake uliorejesha heshima na maadili ya nchi na Watanzania kwa ujumla.

Mwinyi, ambaye ni mlezi mstaafu wa Chama cha Skauti Tanzania, alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 100 ya Skauti Tanzania, yaliyoambatana na utoaji wa tuzo kwa viongozi wastaafu, ambao ni waasisi na walezi wa chama hicho, wakiwemo marais kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema wote wameshuhudia tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano, uadilifu unarudi kwa kasi na nidhamu inajengeka katika Taifa.

"Sina shaka hayo ndiyo mliyokuwa mkifundishwa ninyi skauti wetu na mnaibukia kwa kujifunza nidhamu hiyo, jambo ambalo ni bahati kubwa kwenu, nawapeni hongera, kama tunavyotoa hongera kwa awamu ya tano, pia nashukuru kwa tuzo mlizotutunuku leo,"alisema Mwinyi.

Pia, aliwaasa kuyashika mafunzo hayo, kuyatekeleza na kuyafanyia kazi ili taifa lijue lina skauti wenye mwenendo wa nidhamu iliyotukuka na uadilifu mkubwa.

Naye, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alitoa rai kwa vijana hao kuongeza juhudi za kupambana na dawa za kulevya, kuimarisha maadili, uzalendo na tabia njema, mambo ambayo wamefundishwa.

Alishukuru kwa tuzo ambazo wametunukiwa kama walezi wastaafu na kwamba, alipokea kijiti hicho kutoka kwa kaka yake, ambaye ni Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa, ambaye naye amekabidhi kwa mdogo wake, Rais Dk. John Magufuli, ili aendeleze gurudumu la kukilea chama hicho baada ya yeye kustaafu.

"Nimepokea barua ya kualikwa kuhudhuria mkutano mkuu wa skauti duniani, ambapo wameniteua kuwa msemaji mkuu. Nimekubali, naamini heshima hii nimeipata kwa niaba yenu, nawaahidi nitajitahidi kutafuta maneno mazuri ili nisiwaangushe walionialika na Skauti wa Tanzania waliosababisha nipate mwaliko huo.

"Unajua ukialikwa unatoka 'OUT', vinginevyo ningebaki Msoga kuangalia ng'ombe,"alisema.

Naye, Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, aliwataka skauti kujiepusha na masuala ya siasa, kwa kuwa jukumu lao ni kuimarisha mshikamano wa taifa na kwamba, skauti na siasa ni vitu tofauti.

Alisema binafsi maisha yake yote aliyatumia ndani ya skauti, ambapo alipata malezi yaliyomsaidia katika maisha yake kwa kuwa alipata uelewa, udugu na uzalendo.

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alisema wakati Skauti Tanzania wanatimiza miaka 100, Skauti Zanzibar wanatimiza miaka 105, ambazo zote ni historia.

Aliwataka vijana hao kuyashika na kuyaenzi yote waliyofundishwa ili kuendeleza amani na mshikamano, kwani kuna msemo usemao 'asiyesikia la mkuu huvunjika guu'.

No comments:

Post a Comment