Sunday 30 July 2017

NEC YATEUA WABUNGE WANANE WAPYA CUF



TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeteua majina ya wabunge wanane wa viti maalumu wa Chama cha CUF.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima, alisema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Kailima alisema NEC katika kikao chake cha jana, ilipitisha majina na wabunge wateule wa viti maalumu, ambao ni Rukia Ahmed Kassim,  Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainab Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.

Alisema uteuzi huo umefanyika baada ya NEC kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, aliitaarifu tume kuwepo nafasi wazi nane za wabunge wa viti maalumu kupitia CUF.

"Hii imetokea baada ya waliokuwa wabunge wa viti maalumu kupitia Chama cha CUF, kuvuliwa uanachama na uongozi wa chama hicho, hivyo kupoteza sifa za kuwa wabunge kwa mujibu wa Ibara 67(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997," alisema Kailima.

Mkurugenzi huyo pia alisema kufuatia uteuzi huo, wabunge wanane waliotajwa kwenye barua ya Spika Job Ndugai, hawana sifa tena za kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kikatiba.

Wabunge hao wa viti maalumu waliotajwa kwenye barua ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyoiandika kwa Spika Ndugai ni Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Khadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed.

Kufuatia barua hiyo, iliyokuwa imepitishwa na Kaimu Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, Spika alisema alilazimika kwa mujibu wa sheria kuwafikiria wabunge hao ili kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi.

Baada ya kauli hiyo, juzi, Spika huyo alitamka rasmi kuwa, kwa mamlaka aliyonayo kwa kuzingatia kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kuwaondoa kwenye orodha ya wabunge wa bunge lake.

Spika huyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, aliyoitoa Julai 26, mwaka huu, alisema uamuzi huo ulizingatia pia kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343 kama ilivyojadidiwa Mwaka 2015.

Alisema kutokana na uamuzi huo, alimwandikia Mwenyekiti wa Tume ili aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa sheria.

Wakati hayo yakitokea, Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akidai kuwa, serikali inakichezea 'rafu' chama chake na kwamba, wabunge waliofukuzwa uanachama na CUF ya Profesa Lipumba, wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga maamuzi hayo.

Alidai uamuzi wa kuwafukuza uanachama wabunge hao wanane na madiwani wawili, ulikuwa feki huku ukitolewa na Baraza Kuu feki, hivyo kuitaka Mahakama Kuu itamke kwamba, wao bado ni wanachama halali wa CUF na wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Mbali na hilo, Maalim Seif kwenye taarifa hiyo alizishambulia taasisi za serikali, ikiwemo Ofisi ya Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na baadhi ya wakuu wa wilaya kwamba, wanahusika kwa namna moja au nyingine katika kutekeleza suala hilo.

Alisema kwa kuanzia, wanakwenda mahakamani kupinga uamuzi huo wa Spika huku hatua nyingine zitakazochukuliwa na chama hicho kwa upande wa watu wanaomuunga mkono, zikisubiri maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi aliloliita halali la Chama, ambalo linakutana leo, katika kikao cha dharura.

Hata hivyo, muda mchache kabla ya maamuzi hayo ya NEC na wabunge hao kufungua kesi mahakamani, kwa niaba ya wenzake, Riziki Shahali Ngwali, alisema lengo lao ni kwenda mahakamani punde watakapopokea barua rasmi za kuvuliwa uanachama.

Alisema endapo watazipata, watakwenda mahakamani kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa, baraza hilo la Lipumba halina mamlaka ya kufanya maamuzi ya chama, kutokana na kwamba, Lipumba sio mwanachama wa CUF.  

“Sisi tutakwenda kutafuta haki katika chombo cha kutoa haki, ambacho ni mahakama. Tutakwenda mahakamani, kila ngazi ina maamuzi yake, lakini kwa Lipumba tunakwenda mahakamani kusema yeye hana mamlaka ya hicho alichokifanya, sababu alishavuliwa uanachama.

"Huwezi ukawa mwenyekiti wakati ulishavuliwa uanachama, na kama sio mwanachama, huwezi kufanya maamuzi ya chama, hayakuhusu,” alisema.

Pamoja na hayo, Riziki alidai kuwa, endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yenye mamlaka ya kuthibitisha wabunge viti wa maalumu baada ya chama husika kuteua, itawapa barua za utenguzi wa uteuzi wao, pia wataenda mahakamani kupinga maamuzi hayo.

“Ndio, tunatafuta ushauri wa wanasheria ili watuambie la kufanya, lazima tuhangaike kesho au keshokutwa, sababu na sisi wenyewe hatujapata barua rasmi ya kutuambia hayo maamuzi ya jana, tunayasoma tu kwenye mtandao.

"Kwa namna yoyote ile tulipewa uteuzi kwenye chama kwa barua, kwa hiyo anayetengua uteuzi wetu atupe barua ya kututengeua, kitu ambacho hakijafanyika,” alisema.

Aliongeza kuwa kama tume ya uchaguzi, inayopitisha wabunge wa viti maalumu baada ya chama kuteua, itawapa barua ya kutengua na sababu zake, watatafuta ushauri wa kisheria kukabiliana na hilo.

Naye, Savelina Mwijage, alidai kuwa Profesa Lipumba amekurupuka katika kufanya maamuzi hayo, aliyodai kuwa yamekiuka katiba ya chama hicho kwa lengo la kuendeleza mgogoro ulioko ndani ya chama hicho.

"Na mimi nimesikia hivyo hivyo. Kwa kawaida, ukitenguliwa au kusimamishwa, unapata barua lakini tunasikia kwenye vyombo vya habari na sijapata barua na kwa mujibu wa katiba yetu, huwezi kuchukuliwa hatua ya kuvuliwa uanachama kabla ya vikao kufanyika. Kuna vikao vinakaa vya baraza kuu, kamati tendaji, vinakuita mara ya kwanza ya pili mara ya tatu unavuliwa, lengo la kukurupuka, anaendelea na migogoro," alisema.

Baadhi ya wasomi waliozungumza na Uhuru kuhusu sakata hilo, walisema pande mbili za CUF zinapaswa kukutana na kuzungumza, badala ya kuendesha chama kama wanavyofanya sasa, jambo linalotishia uhai wake.

Dk. Chrispin Haule wa Chuo Kikuu cha Jordan, alisema hali ilivyo ndani ya CUF, inavuruga utendaji na utoaji wa maamuzi kwenye ofisi na taasisi zingine zinazohusika na siasa, hivyo CUF haipaswi kulalamika kwa vyovyote kuhusu uamuzi uliofanywa na Ofisi ya Spika na NEC.

Kwa upande wake, Paul Dau, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Siasa, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema siasa haziko kama zinavyofanywa na CUF, hivyo yanayotokea ndani ya chama hicho ni matokeo ya kukosekana kwa umoja wao.

Alisema tofauti na miaka mingine, serikali iliyoko madarakani inafanyakazi kwa ufanisi, hivyo mazoea ya kukorofishana na kukimbilia mahakamani wakati ofisi ya Spika ikiendelea kutengeneza mazingira ya kusubiri, hayapo hivyo kila chama kijifunze kulingana na uhalisia wa mambo.

No comments:

Post a Comment