Thursday, 24 August 2017
MAGAZETI, MACHAPISHO KUSAJILIWA UPYA
SERIKALI imesema magazeti na machapisho yote yataanza kusajiliwa upya kuanzia jana hadi Oktoba 15, mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbasi, alipozungumza na waandishi wa habari.
Dk. Abbasi alisema ili kukidhi matakwa ya kanuni ya 7 ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2017, serikali kupitia MAELEZO, itaanza kutoa leseni za machapisho mbalimbali, ikiwemo magazeti na majarida yote nchini.
Pia, alisema kwa mujibu wa sheria, utaratibu wa sasa unafuta mfumo wa awali wa utoaji wa hati za usajili wa magazeti na majarida, uliokuwa ukitumika kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ambayo kwa sasa imefutwa.
Vilevile, alisema utaratibu huo mpya utawahusu wamiliki wote wa magazeti, majarida na wamiliki wapya, ambao hawakuwa wameyasajili machapisho yao,
ambapo leseni hizo zitahusishwa kila mwaka kwa mujibu wa Kanuni ya 8(3) na 12 (1 na 2) cha Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2007.
"’Fomu za maombi na akaunti ya kulipia na orodha ya nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya usajili, vinapatikana kuanzia leo katika ofisi za MAELEZO, Dar es Salaam na Dodoma au kwenye tovuti ya maelezo www.maelezo.go.tz,’’ alisema.
Aliwataka wamiliki wa magazeti na majarida wenye usajili wa zamani, wawe wamekamilisha taratibu za kupatiwa leseni mpya za uendeshaji na uchapishaji wa majarida na magazeti ifikapo Oktoba 15, mwaka huu, vinginevyo hawataruhusiwa kuyachapisha kwa kuwa watakuwa wametenda kosa kisheria.
Mkurugenzi Msaidizi anayehusika na usajili, Patrick Kupangula, alisema ili kupata usajili mpya, mmiliki anapaswa kuwa na cheti cha usajili wa kampuni kwa wenye kampuni, sera ya gazeti, ada na mchoro wa gazeti litakavyokuwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment