Thursday, 24 August 2017

SAMIA AWATAKA DIASPORA KUCHANGIA MAENDELEO

WATANZANIA wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), wametakiwa kuwa raia wema na wazalendo kwa ajili ya kuchangia maendeleo nchini kwao, baada ya serikali kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji.

Hayo yalisemwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake, ambayo ilisomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba, katika Hoteli ya Sea Cliff, Fujoni, Mkoa wa Kaskazini B Unguja.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga vizuri kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa jamii ya wana-Diaspora ili kuchangia pato la taifa.

"Kwa mfano, juhudi kubwa zimechukuliwa katika kuleta maendeleo, ikiwemo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vya kati, ambapo sekta mbalimbali zinashirikishwa ikiwemo wananchi.

"Serikali ya awamu ya tano ipo katika hatua za kuleta maendeleo, ikiwemo ujenzi wa viwanda, ambapo ifikapo mwaka 2020-2025, imejipanga kuwa na uchumi wa kati katika sekta ya viwanda, kwa hivyo mchango wa Diaspora unahitajika kwa kiwango kikubwa,"alisema.

Pia, Samia aliwataka wana-Diaspora kuwa raia wema wakati wanapokuwa nje ya nchi na kuishi kwa utulivu.

Alisema utulivu utawafanya kufanya shughuli zao mbalimbali za maendeleo na uzalishaji na kutoa mchango wao nyumbani.

"Wito wangu nawaomba wana-Diaspora, wakati mnapokuwa nje ya nchi muwe raia wema, hatua ambayo itawafanya kutambuliwa na hivyo kusaidia maendeleo nchini mwenu," alisema.

Vilevile, alisema hivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya Muungano imefungua ofisi sita za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutoa fursa kwa Watanzania kuwasiliana nchini kwao bila ya matatizo.

"Tumefungua ofisi za ubalozi Israel, Korea Kusini pamoja na Algeria kwa ajili ya kutoa nafasi kubwa kwa Watanzania, kushirikiana na kuwasiliana na wenzao walioko nje ya nchi," alisema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefurahishwa na juhudi za wana-Diaspora katika kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Ussi alizitaja juhudi zinazochukuliwa kwa ajili ya kuwatambua Watanzania hao kuwa ni matayarisho ya Sera ya Diaspora.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua kwa kiasi kikubwa mchango wa Diaspora katika kuleta maendeleo na ndiyo maana tupo katika hatua za mwisho za matayarisho ya sera ya Diaspora," alisema.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Diaspora, Asha Maulid, alisema wamefurahishwa na juhudi za serikali, ambazo zimewafanya sasa kutambuliwa rasmi pamoja na mchango wao kwa taifa.

Asha, ambaye anaishi Uingereza, alisema wamefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na serikali zote mbili katika kujenga mazingira mazuri dhidi yao, hatua ambayo imewapa ari na moyo wa kusaidia maendeleo nchini.

Mkutano huo unawashirikisha wana-Diaspora 200, lengo kubwa likiwa kuwaunganisha na kufahamu fursa zinazopatikana nchini, ikiwemo uwekezaji.

No comments:

Post a Comment