Wednesday, 30 August 2017
MAWAKILI WAMGOMEA TUNDU LISSU
MAWAKILI katika maeneo mbalimbali nchini, jana waliendelea na kazi zao kama kawaida, hivyo kupuuzia wito wa mgomo uliotolewa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu.
Wiki iliyopita, Lissu aliwataka mawakili kugoma kufanyakazi jana na leo, kwa lengo la kulaani tukio la kushambuliwa kwa bomu ofisi za mawakili za Kampuni ya IMMMA, zilizoko Upanga, Dar es Salaam.
Katika maeneo ya Mahakama ya Rufani Tanzania, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, Mahakama ya Kisutu na kwingineko, gazeti hili lilishuhudia mawakili hao wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, kulishuhudiwa baadhi ya mawakili wakiendelea kutimiza majukumu yao kana kwamba hakuna wito wowote uliotolewa.
Akizungumzia kuhusu wito huo wa mgomo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, Augustine Rwizile, alisema mawakili walikuwa wakiendelea na majukumu yao kama kawaida.
“Mwenyewe umeona, mimi niseme nini tena, kwangu sijaona kama kuna kitu kama hicho, wala kitu kipya hapa, shughuli zinakwenda kama kawaida,”alisema Rwizile.
Aliongeza kuwa, mawakili waliokuwa na kesi za wateja wao, walifika kama kawaida na wasio na kesi hawakufika, hivyo haiwezi kuchukuliwa hawajafika kwa sababu ya mgomo huo.
Katika Mahakama ya Rufani Tanzania, mawakili walishuhudiwa wakiingia katika vyumba vya mahakama kwa ajili ya kuwatetea wateja wao, huku wengine wakibadilishana mawazo baada ya kutoka kwenye kesi.
Mmoja wa wanasheria waandamizi wa serikali, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji, alisema hakuna harufu yoyote ya mgomo huo na mawakili walifika mahakamani hapo kuwatetea wateja wao.
“Kesi zinaendelea kama kawaida, mawakili wamefika kama kawaida, hawawezi kufuata tamko la mtu mmoja na matakwa yake,"alisema.
Pia, katika Mahakama Kuu, mawakili walikuwa wakiendelea na shughuli zao.
Baadhi ya mawakili hao walisema Lissu amekuwa akichanganya mambo ya kisiasa na yale ya kisheria, jambo ambalo halikubaliki.
"Kwanza aliamua kuitisha mgomo Jumanne na Jumatano na kuacha kuitisha Jumatatu, siku ambayo mwenyewe alikuwa na kesi nzuri za kusimamia. Hatuwezi kuchanganya mambo haya," alisema mmoja wa mawakili hao.
Kwa upande wake, wakili maarufu Jerome Msemwa, ambaye alifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuhudhuria kesi za wateja wake, alisema hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuwafanya mawakili wagome.
Pia, alisema hakuna sheria wala kifungu cha sheria kinachowaruhusu wao kufanya hivyo.
"Hakuna sheria wala kifungu acha sheria kilichotajwa, ambacho kinaturuhusu kufanya hivyo," alisema.
Naye wakili Manzi, alisema wana mikataba binafsi na wateja wao wakati wakili Fredrick Jonathan, alisema kama mawakili, wanasikitika juu ya tukio hilo, lakini jambo hilo kwa sasa lipo katika mamlaka za uchunguzi.
Alisema hawaoni iwapo ni busara kugoma kufanyakazi kwa kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wateja wao.
"Hili ni tukio la uhalifu, nina mteja wangu yupo mahabusu na nina mkataba, nisipoingia mahakamani, nitamuumiza mteja," alisema.
Wakili huyo alisema linapotokea tukio la uhalifu, halafu ukanyoosha kidole kwa taasisi moja, hata mhalifu anapata nafasi ya kukimbia na kujificha.
Wakili mwingine, ambaye jina lake hakutaka kutajwa gazetini, alisema kufanya mgomo kuhudhuria mahakamani ni sawa na kumuadhibu mteja kwa kosa ambalo halijui na wala halimuhusu.
Alisema ni mapema kuchukua hatua na wao wakiwa maofisa wa mahakama, unapogoma unakuwa unamgomea nani huku mteja wako yupo mahabusu. Alisema analaani kulipuliwa kwa ofisi za kampuni hizo, lakini haungi mkono mgomo.
Katika Mahakama ya Kisutu, mawakili wanaohudhuria kesi za jinai na za madai, walionekana wakifika mahakamani hapo kuendelea na shughuli zao.
Katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, mmoja wa mawakili alisema wanaendelea na kazi kama kawaida.
"Ni kweli Lissu alitangaza mgomo wa siku mbili kwa mawakili kutokana na tukio la mlipuko, lakini sisi hatuoni sababu ya msingi ya kufanya mgomo kwani sio suluhisho la matatizo,"alidai wakili huyo.
Alisema linapotokea jambo linalohusu masuala ya kiusalama, hawapaswi kukurupuka, badala yake wanatakiwa kuwa na utulivu kusubiri uchunguzi ufanyike na kubaini chanzo na hatua zitakazochukuliwa.
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Benedicto Kitalika, aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi wa tukio hilo ili kuwabaini wahalifu.
Pia, alitoa rai kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia katika upelelezi, waziwasilishe ili zifanyiwe kazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment