Wednesday, 30 August 2017
MAMBOSASA: NATAKA DAR ISIYO NA UHALIFU
KAMISHNA Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema hataki kuona jiji hilo likiwa ni sehemu ya maficho kwa wahalifu kukimbilia na kujiona wako salama.
Pia, amewataka wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa polisi ili kuibua matukio ya kiuhalifu yanayozuia maendeleo yao.
Alitoa tamko hilo Dar es Salaam, jana, wakati alipokuwa akijitambulisha kwa waandishi wa habari na kuelezea mikakati yake baada ya kuteuliwa kuiongoza kanda hiyo.
Mambosasa alisema yupo kwa ajili ya kupambana na uhalifu na kutengeneza mazingira rafiki kwa wananchi kwa ajili ya kuondoa kero zinazozuia maendeleo kutokana na usumbufu wa wahalifu.
"Taarifa za uhalifu kwangu ni mtaji na ndizo zinazoniwezesha kufanyakazi vizuri. Hatutaki kuona Dar es Salaam, inakuwa maficho yao kwani tutawakamata kabla hawajafika waendako na wahakikishe wanatafuta
mkoa mwingine wa kwendakufanya uhalifu, siyo hapa," alisema.
Kamishna huyo, aliitaja mikakati aliyonayo katika kupambana na kudhibiti uhalifu kuwa ni kuhakikisha kila mwananchi anafanya shughuli za maendeleo pasipo kusumbuliwa .
Pia, alisema amepanga kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia kamati za mitaa, kata na hadi mkoa.
Aliwataka wananchi kuhakikisha kila mtu anakuwa mlinzi kwa mwenzake, kutokukubali kukaa na wahalifu na kutokuwa sehemu ya uhalifu.
Katika hatua nyingine, Mambosasa alisema hayuko tayari kuona uhuru wa mtu ukichezewa na askari kwa kuwanyanyasa wananchi.
"Mara nyingi polisi wamekuwa wakikamata mtu na kusema ni amri kutoka juu. Kwangu mimi ukisikia hivyo, kata rufani kwa sababu polisi huwa anafanyakazi kwa kufuata sheria," alisema.
Wakati huo huo, Kamishna huyo alizungumzia kuhusiana na tukio la kuungua kwa kampuni ya mawakili na kusema kuwa, polisi bado wanaendelea kufanya upelelezi.
Alisema tatizo ni baadhi ya watu kuchukulia tatizo hilo na kuliingiza katika masuala ya kisiasa.
"Tambueni matukio kama hayo, hasa yanayoashiria kuwepo na mlipuko wa bomu, lazima tufanye uchunguzi wa kikemikali ili kubaini aina ya mlipuko na kuja kuutolea ufafanuzi, siyo jambo la haraka haraka," alisema.
Aliwataka wananchi kutokurupuka kutoa taarifa za masuala ya uchunguzi, bali waviachie vyombo sahihi, hasa vya usalama kufanyakazi yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment