Wednesday, 30 August 2017

MAKONDA ATANGAZA NEEMA DAR



MKUU wa Mkoawa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameshusha neema baada ya kutangaza kuwa, kila mtumishi katika sekta ya afya, polisi, Jeshi la Magereza na walimu Dar es Salaam, watapatiwa viwanja kwa gharama nafuu.

Neema nyingine ni wananchi kupimwa afya zao bure kuanzia wiki ijayo.

Makonda alisema hayo jana, Dar es Salaam, wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali  ya kisasa  ya Koika Chanika, itakayokuwa inatoa huduma za mama na mtoto, wilayani Ilala.

Hospitali hiyo inayotajwa kuwa ni ya kwanza nchini kumilikiwa na serikali, ikitoa huduma ya mama na mtoto, inatarajiwa kuanza kutoa huduma bure Agosti 4, mwaka huu.

Makonda alisema serikali itaendelea kuboresha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi.

Alisema uboreshaji huo utakwenda sambamba na uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa sekta hiyo, kuwapa motisha na mahitaji muhimu.

“Walimu nimewatafutia viwanja na zaidi ya 700, wamekwishakatiwa viwanja hivyo. Pia nitagawa viwanja kwa wahudumu wa afya katika hospitali zetu, polisi na magereza, watapewa viwanja kwa gharama nafuu kabisa,  katika eneo zuri, ambalo litakuwa na mitaa yao,” alisema Makonda.

Alifafanua kuwa nia ni kuhakikisha Dar es Salaam, inaongoza katika kutoa huduma bora, hasa za afya huku watumishi wake wakiishi maisha bora.

“Wiki ijayo, tutaanza upimaji wa afya bure kwa wananchi wote Dar es Salaam. Hata kama hatutakuwa na fedha, tutahakikisha kila atakayejitokeza anapimwa afya yake,”alisema.

Makonda aliwataka watumishi katika hospitali hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuamini kuwa kazi hiyo ni wito.

“Kazi ya udaktari na uuguzi ina uhusiano mzuri na Mungu. Mmepewa nafasi ya kukaa katikati. Najua kinamama mnawafahamu, wapo watakaokuja  wana hali mbaya, wahudumieni wote bila kuangalia rangi, sura hali ya kipato au itikadi,”alibainisha mkuu huyo wa mkoa.

Aliongeza: “Fanyenikazi kama wito. Mtumishi ambaye nia yake ni kupata mshahara tu, hafai kuwa mfanyakazi. Umuhimu wa  mtumishi ni kufanyakazi iliyo bora." 

Awali, Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Maghembe, aliwataka watumishi hao kufanyakazi kwa bidii kwa kuhakikisha  wanafuata  miiko na wajibu wao, badala ya kutoa lugha chafu au kuchelewa kuhudumia mteja.

Akitoa ripoti fupi ya hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala,   Victoria Ludovick, alisema  tayari vitanda 160, vimefungwa na watumishi 78, wanatarajiwa kutoa huduma katika hospitali hiyo.

“Watumishi watakaotoa huduma hapa wamepewa mafunzo maalumu na kwa asilimia kubwa wameripoti kazini. Hospitali itaanza kutoa huduma Septemba 4, mwaka huu. Vifaa vyote vipo,”alisema Dk. Victoria

Dk. Vitoria alisema halmashauri imetenga sh. milioni 600, kati ya sh. bilioni 1.6, zinazohitajika

No comments:

Post a Comment