RAIS Dk. John Magufuli amepiga marufuku operesheni ya ubomoaji wa nyumba zaidi ya 20,000 mkoani Dar es Salaam.
Operesheni hiyo ni ya ubomoaji wa nyumba zaidi ya 300, zilizoko katika Mtaa wa Masaki na Kata ya Toangoma, wilayani Temeke, iliyokuwa ifanyike chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Operesheni nyingine, ambayo Rais Dk. Magufuli ameagiza ifutwe ni ile ya nyumba 17,000, ambayo ilitangazwa Agosti 28, mwaka huu na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambayo ingehusisha nyumba zilizojengwa katika Bonde la Mto Msimbazi na Jangwani, wilayani Kinondoni.
Akihutubia kwa nyakati tofauti wananchi wa Toangoma na Bonde la Msimbazi, jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema ni marufuku operesheni bomoa bomoa zaidi ya ile ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro, inayoendeshwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na ujenzi wa reli ya treni ya kisasa ‘Standard Gauge’.
Alimuagiza Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kumkamata mtu yeyote, ambaye atathubutu kubomoa nyumba yoyote ya mwananchi kinyume cha utaratibu.
Makonda alisema taarifa za operesheni hizo hazikufuata utaratibu wa kimamlaka, ambapo zimekuwa zikitolewa kupitia vyombo vya habari pekee.
Alifafanua kuwa, baada ya taarifa za operesheni hizo kutangazwa kupitia vyombo vya habari, alipiga hesabu na kubaini kuwa, iwapo nyumba 17,000, zitavunjwa, wananchi zaidi ya 100,000, watakosa mahali pa kuishi.
“Hii ni idadi kubwa sana. Nikamuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa (Theresia Mbando) kumtafuta aliyetoa agizo hili ni nani?” Alisema Makonda.
Aliongeza: “Nilitaka kufahamu kama mimi mkuu wa mkoa ninazo taarifa? Ofisi yangu haikuwa na taarifa. Nikawa bado nahangaika ni nani huyu aliyeingia kwenye nyumba yangu bila mimi mwenye nyumba kujua?”
Makonda alisema utaratibu ulivyo serikalini, kama kuna maamuzi yanachukuliwa na serikali kuu, lazima mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wajulishwe.
“Nikaangalia na wakuu wangu wa wilaya na wakurugenzi, hakuna aliyekuwa na taarifa. Kama maamuzi hayo yalitolewa na wizara, serikali huwa inawasiliana kwa maandishi, siyo kwa magazeti, lakini hakuna maandishi,”alisema Makonda.
SIMU YA JPM
Makonda alisema juzi, saa tatu usiku, alipigiwa simu na Rais Dk. Magufuli, kuhusu undani wa sakata la bomoa bomoa zinazotangazwa jijini Dar es Salaam.
“Wakati nahangaika kutafuta majibu, saa tatu nikaona simu ya mwanaume wa Tanzania inaingia (Rais Dk. Magufuli). Aliniuliza Makonda, wewe ndiye mkuu wa mkoa, unazo taarifa za bomoa bomoa?” Alieleza Makonda.
Aliongeza: “Nikamjibu taarifa niliyo nayo ni ile ya bomoa bomoa ya upanuzi wa barabara ya Morogoro na wa reli, taarifa ya bomo bomoa nyingine sina.”
Makonda alisema katika mazungumzo hayo, alimuomba Rais kama anazo taarifa ampe maelekezo.
“Rais akaniambia hana taarifa. Alivyoniambia hizo taarifa hana na mimi sina, tukabaki tunaulizana. Nikasema wewe ni mkuu wa nchi na mimi umenimegea hiki kipande, hapa katikati nani kapenya penya,”alibainisha Makonda.
Aliongeza: “Wote tukasema tumtafute. Rais akaniambia mimi nilichaguliwa ili kuwaletea wananchi maendeleo, sikuchaguliwa kuwabomolea nyumba zao. Akaniuliza umesoma Ilani ya Chama?"
“Nikamjibu mzee nilivyokuja serikalini, nilitokea kwenye Chama. Akaniambia Ilani ya CCM ukiisoma, inasema tutaboresha makazi, hatukusema tunabomoa makazi,”alizidi kubainisha Makonda.
Makonda aliendelea kusema mazungumzo baina yake na Rais Dk. Magufuli,
yalikwenda mbali zaidi, kiasi cha kuelekezwa awaambie wananchi walio kwenye maeneo, ambayo ni hatarishi, kuhakikisha usalama wa familia zao.
“Mimi kama mkuu wa mkoa na rais, wote tumehuzunika na kufedheheka na kauli hizo za bomoa bomoa, kwa sababu ofisi za serikali zinafuata utaratibu, mamlaka ya mkoa, wilaya mpaka mtaa,”alieleza mkuu huyo wa mkoa.
“Kwa sababu hawajataka, hawajaniambia sababu, hawajaniambia wananchi wangu zaidi ya 100,000, watakwenda kuishi wapi, ninasitisha ubomoaji nyumba kuanzia sasa,” alisema Makonda.
“Tufuate taratibu. Utawala bora ni kufuata taratibu na sheria. Kama kuna jambo limekiukwa kwa watu waliovamia maeneo, ziko taratibu,”alisisitiza Makonda.
"Ninazo taarifa kuwa, kuna wananchi wanazo hati za makazi, wengine tuliwapimia tukawapa na hati, leo tunataka kuwafukuza katika maeneo yao,"aliongeza.
Alisema inawezekana kuna baadhi ya watu walikuwa na mkakati wa kubomoa nyumba za mabondeni ili kuwagombanisha wananchi na serikali yao.
“Watu wanakwenda nje ya utaratibu, wanakwenda hata kubomoa nyumba zisizo husika, wanawaacha watu wanahangaika. Wanaacha wananchi wanalia na wengine wanania ovu,"alisema.
Kufuatia tamko hilo, wakazi wa Toangoma na Bonde la Mto Msimbazi, ambao nyumba zao ziliwekwa alama ili kubomolewa, walilipuka kwa furaha na kuimba nyimbo za kumsifu Rais Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment