Thursday 31 August 2017

SHAHIDI: MANJI AMEWEKEWA VYUMA KWENYE MOYO



MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, amepanda katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiwa shahidi wa mfanyabiashara Yussuf Manji.

Profesa Janabi alidai jana, kuwa Manji amewekewa vyuma kwenye moyo, tiba ambayo anakumbuka alipatiwa katika mji wa Florida, Marekani, ambapo baada ya kurudi, alihudhuria kliniki kwenye taasisi yao na kulazwa. 

Janabi alifika mahakamani hapo na kupanda kwenye kizimba mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, ambapo alitoa ushahidi katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, inayomkabili mfanyabiashara huyo.

Manji, alipanda kizimbani mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi kwa upande wake, baada ya mahakama hiyo kumuona ana kesi ya kujibu juu ya tuhuma hizo, kutokana na kuridhika na ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa jamhuri.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Hajra Mungula, kutoa ushahidi  kwa kuulizwa maswali, Profesa Janabi (51), ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alidai anamfahamu Manji kwa kuwa aliwahi kulazwa katika taasisi yao ya JKCI, Februari na Julai, mwaka huu.

Shahidi huyo alidai kabla ya hapo, Manji aliwahi kuhudhuria kliniki kwenye taasisi hiyo, ambapo mara ya kwanza alipata matibabu ya moyo nje ya nchi na alifika kwao kama mgonjwa wa moyo aliyetibiwa.

"Tulitizama kumbukumbu zake na kumtibu kama mgonjwa wa moyo. Februari, mwaka huu, alirudi tena tukamchunguza kama vile vyuma vimeziba ama la, ambapo tuliingiza mipira hadi kwenye moyo na kugundua unafanya kazi vizuri," alidai.

Shahidi alidai Julai, mwaka huu, Manji alirudi tena kwenye taasisi hiyo, akiwa na tatizo hilo na maumivu upande wa kushoto katika moyo wake.

Alidai mshitakiwa huyo alipofika kwenye taasisi hiyo, Februari na Julai, mwaka huu, hakumpokea yeye moja kwa moja, ila anakumbuka alikuwa anatokea polisi.

Alidai katika magonjwa ya moyo, walimpatia dawa za aina tatu na alikuwa na matatizo ya mgongo na kutolala vizuri, ambapo alikuwa na dawa zake binafsi.

Shahidi huyo alidai kwa upande wa maumivu, walimpatia dripu ya paracetamol na kuna wakati alipewa sindano ya tramadol. Alidai kipindi cha maumivu, walimpatia matibabu, lakini kabla ya hapo, alilazwa Hospitali ya Aga Khan.

Profesa Janabi alipewa kielelezo namba mbili, ambacho ni ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu matokeo ya uchunguzi wa sampuli ya mkojo wa Manji, ambayo aliisoma na kisha kuulizwa maswali.

Alidai grupu la daiwa aina ya benzodiazepines, lina dawa nyingi ambazo kama grupu, kuna zile zinazopatikana hospitalini.

Aidha, alidai kabla ya mgonjwa wa moyo hajawekewa vyuma, kuna vitu ukivitumia vinaathiri mishipa ya moyo, vikiwemo sigara na dawa za kulevya na baada ya kuwekewa, kuna vitu anaambiwa asivitumie, lakini uamuzi wa kutumia ama la siyo wa daktari.

Shahidi huyo alidai kwa mgonjwa wa moyo, ambaye ana vyuma kwenye moyo, iwapo atatumia dawa za kulevya aina ya heroin, kuna athari kubwa, kwa kuwa kazi ya vyuma ni kuzibua mishipa ya moyo ili damu iweze kutembea.

Alidai athari yake ni kwamba, vyuma vinaweza kuziba tena na mgonjwa anaweza kwenda kwenye oparesheni kubwa zaidi na kwamba, Manji alipofika kwenye taasisi yao, vyuma vilikuwa havijaziba.

Baada ya kumaliza kuulizwa maswali na Wakili Hajra, ambaye alikuwa akishirikiana na Wakili Hudson Ndusyepo, shahidi huyo aliendelea kutoa ushahidi kwa kuulizwa maswali na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis. Shahidi huyo alidai matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kusababisha matatizo ya moyo.

Pia, alidai Manji alipewa dawa za aina tatu na kweli katika dawa hizo hakuna yenye metabolite ya morphin.

Shahidi huyo alimalizia kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi kwa kumuuliza maswali, ambapo aliieleza mahakama kuwa, visababishi vya matatizo ya moyo vipo vingi, mbali ya matumizi ya dawa za kulevya na kwamba, Manji alikuwa anatibiwa matatizo ya kutolala vizuri na maumivu katika Hospitali ya Aga Khan.

Shauri hilo litaendelea leo, ambapo Manji atapanda kwenye kizimba kujitetea.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Manji, ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga, anadaiwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu, eneo la Upanga Sea View, wilayani Ilala, Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Mshitakiwa huyo kwa sasa yupo mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi, ambayo Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana yake na washitakiwa wenzake.

No comments:

Post a Comment