Thursday 31 August 2017

RC AAGIZA KUKAMATWA BOSI BODI YA KOROSHO



KAMANDA mpya wa Polisi mkoani Mtwara, Lucas Mkondya,  ameanza kazi kwa kuagizwa na mkuu wake wa mkoa, Halima Dendego, kumkamata na kumuhoji  Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Hassan Jaruff.

Mkurugenzi huyo na wenzake sita, kati yao watatu tayari wametiwa mbaroni tangu juzi, watahojiwa na kufikishwa mahakamani kwa  kupokea, kutunza na kusambaza  dawa za korosho, ambazo muda wake wa matumizi umepita na siyo sahihi.

Hadi jana, waliokuwa wamekamatwa ni watunza ghala la pembejeo watatu, ambao ni  watumishi wa nyadhifa nyingine katika Bodi ya Korosho, Katibu Mukhtasi wa Mkurugenzi Mkuu, Felista Onestina, Emiliana Salia na Husna Rajabu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Halima  alimwagiza Mkondya, kuwakamata mara moja, Mkurugezi Mkuu Jaruff  na  Mkurugenzi wa Kilimo na Ubanguaji, Luseshelo Silomba.

Wengine aliotaka wakamatwe kwa tuhuma hizo ni Meneja Rasimali Watu, Shauri Mokiwa na Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi inayolinda ghala hilo, ambae jina lake halikupatikana.

Mkuu wa mkoa  alikemea hujuma hizo, alizodai kufanywa na Bodi ya Korosho Tanzania na kuonya kuwa, ofisi yake haitafumbia macho tukio lolote la kutia doa azma ya serikali kuwainua wakulima.

“Ninakuagiza kamanda wa polisi wa mkoa, kuwafikisha mahakamani wahusika wote wa matukio mawili, la awali na hili la jana na kuwafikisha mahakamani,” alisema Halima.

Akifafanua tukio la juzi, Halima alisema ofisi yake ilipata taarifa ya kusambazwa pembejeo kwa wakulima, ambazo muda wake wa matumizi umemalizika.

Halima alisema walifanya ziara fupi ya kushutukiza katika ghala hilo na kukuta dawa za maji lita 414.5, zilizokwisha muda wake, zikiwa tayari kusambazwa kwa wakulima.

Alisema kati ya hizo, nyingine katika kasha ziliandikwa tofauti na dawa iliyopo ndani.

Halima alifafanua kuwa, katika makasha hayo, kuliandikwa dawa hizo zimetengenezwa mwaka 2017, lakini zenyewe ndani  zilionyesha kuwa ni za mwaka 2012 na muda wa matumizi ni miaka mitatu.

Hili ni tukio la pili la kukamatwa dawa zilizopita muda wake. Juni 30, mwaka huu, alikamata dawa ya unga aina ya salfa tani 20, zilizopita muda wake wa matumizi.

No comments:

Post a Comment