Thursday, 31 August 2017

VIGOGO 56 WAAMRIWA KUREJESHA HATI ZA KUSAFIRIA ZA KIDIPLOMASIA


VIGOGO 56 wamerejesha pasi za kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia, baada ya Idara ya Uhamiaji kuwataka kuacha kuzitumia kwa kuwa zimefikia ukomo wa matumizi yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya idara hiyo kutangaza Agosti 14, mwaka huu, kuwa viongozi wote wanaotumia pasi hizo, kuzirejesha mara moja ndani ya siku 30.

Idara hiyo imeeleza kuwa, endapo wahusika watakaidi agizo hilo, idara hiyo itachukua hatua za kuzifungia pasi hizo na vigogo hao watashindwa kuzitumia popote pale duniani.

Uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alilolitoa Julai 28, mwaka huu, ambapo aliiagiza Idara ya Uhamiaji, kudhibiti kitengo cha utoaji hati za kusafiria za kibalozi na wanaomaliza muda wasipewe tena.

Pia, Waziri Mkuu aliagiza kukaguliwa kwa hati hizo katika mipaka yote na maeneo yote ya usafiri, ili kujua kama anayeitumia bado ana hadhi ya kidiplomasia na endapo Uhamiaji itabaini mtumiaji hana hadhi hiyo, ichukue pasi husika kwani baadhi ya watu wanazitumia vibaya.

Akizungumza jana, katika mahojiano maalumu na Uhuru, ofisini kwake, Dar es Salaam, Mrakibu Ali Mtanda, ambaye ni Msemaji Mkuu wa idara hiyo, alisema vigogo hao wamezirejesha pasi hizo Makao Makuu ya Uhamiaji, yaliyoko Kurasini.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, kutoa tamko mwanzoni mwa mwezi huu kuwa,  walianza kuendesha zoezi hilo kwa njia za kidiplomasia, kwa kuwataka wahusika wazirejeshe kwenye ofisi za Uhamiaji.

"Mwanzo tulianza kuchukua hatua za kidiplomasia. Kuna watu walikuwa wanamiliki pasi za kidiplomasia, lakini hadhi yao imekoma baada ya kumaliza kazi zao. Tumewaomba wazirudishe, lakini kama hawataweza kufanya hivyo, tutachukua hatua," alieleza.

Kamishna Jenerali alieleza kuwa, miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa na idara hiyo ni kuzizuia pasi hizo kutotumika popote pale, endapo muhusika atakaidi kuzirejesha kama ilivyoagizwa.

Mrakibu Mtanda alisema pasi ya kusafiria ni mali ya serikali na anayepatiwa ni Mtanzania pekee, hivyo ikibainika yeyote amepatiwa pasi hiyo kwa udanganyifu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

"Wamerudisha viongozi 56, lakini kwa sasa siwezi kuwataja majina yao.
Tunashukuru kwa vile wameonyesha uungwana, lakini tunawaomba wengine wenye pasi hizo, wazirudishe mara moja kabla hatujachukua hatua,"alisema Mtanda.

Aliongeza kuwa, viongozi hao wanatakiwa kurejesha pasi hizo hata kama wapo mikoani, katika ofisi za idara hiyo kabla ya muda huo.

"Tunawaomba viongozi wenye pasi hizo, wanatakiwa kuzipeleka katika idara zetu zilizoko mikoani, lengo usipite muda huo,"alisisitiza Mtanda.

Alisema viongozi wanaotakiwa kubakia na pasi hizo ni marais wastaafu, makamu wa rais wastaafu, marais wastaafu wa Zanzibar na mawaziri wakuu wastaafu.

Viongozi wengine, ambao wanatakiwa kuwa na pasi hizo hata kama wamestaafu ni waziri kiongozi, maspika wa bunge wastaafu na baraza la wawakilishi.

Wengine ni manaibu spika, jaji mkuu mstaafu, makatibu wakuu viongozi, wanasheria wakuu wastaafu, wakuu wa jeshi la ulinzi, Inspekta Jenerali wa Polisi na wakuu wa Jeshi la Magereza.

Pia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS).

Mrakibu huyo alieleza kuwa, idara hiyo inaendelea kufanya doria kwenye maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wimbi la wahamiaji haramu linadhibitiwa.

Alieleza kuwa msako dhidi ya wahamiaji haramu hauwalengi raia wa baadhi ya nchi, bali ni kwa wote wanaoingia nchini bila kufuata sheria na taratibu za uhamiaji.

No comments:

Post a Comment