Thursday, 31 August 2017
SERIKALI KUUZA MALI ZA WADAIWA SUGU KODI YA ARDHI
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabulla, ameziagiza halmashauri zote nchini kuwafikisha mahakamani na kuuza mali zao, wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi wenye madeni ya muda mrefu.
Dk. Mabulla alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya makusanyo ya kodi ya ardhi mkoani Geita, baada ya kukuta majina 100 ya wadaiwa wa kodi ya ardhi, ambao hawajalipa kwa zaidi ya miaka 10.
Naibu Waziri alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, kuhakikisha wadaiwa hao wa muda mrefu wanaandikiwa notisi ya siku 14 na kwamba, wasipolipa ndani ya muda huo, wafikishwe mahakamani bila kuchelewa na kama wasipolipa, mali zao zipigwe mnada.
Baada ya kubaini hayo, Angelina alifanya upekuzi wa nyaraka za umiliki wa ardhi katika masijala ya ardhi ya Halmashauri ya Mji wa Geita na kugundua uhifadhi mbovu wa hati na ucheleweshwaji utoaji hati za wamiliki kwa muda mrefu.
Naibu waziri alimuagiza mkurugenzi huyo kutembelea mara kwa mara katika ofisi na masijala za ardhi ili kuhakikisha maofisa wa idara ya ardhi wanatoa hati kwa wakati na kwa mpangilio mzuri bila kuleta migogoro.
Aidha, Naibu Waziri alitembelea eneo lenye viwanja vilivyowekwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, ambavyo vimepangwa kujengwa ofisi za serikali, shule, hospitali, makazi, maeneo ya kuzikia na huduma nyingine za kijamii.
Alimtaka mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, kuhakikisha mji huo unapangwa vizuri na kuwekwa miundombinu ya barabara, maji safi na taka na umeme ili kuepusha migogoro ya ardhi, ambayo mara nyingi huibuka kutokana na wilaya kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Dk. Angelina alitembelea eneo la Bombambili mkoani Geita, lililojengwa nyumba 48 za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambapo nyumba 14 tayari zimenunuliwa na Halmashauri ya Mji wa Geita.
Dk. Angelina alizitaka halmashauri nyingine nchini, kuiga mfano wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwashirikisha NHC katika kujenga nyumba bora, badala ya kutumia wakandarasi wa nje wakati Shirika la Nyumba la Taifa lipo na linajenga nyumba nzuri na kwa gharama nafuu.
Meneja wa NHC mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu, Injinia Benedict Kilimba,aliishukuru Halmashauri ya Mji wa Geita, kwa kuwa ya kwanza kununua nyumba hizo 14, katika hatua ya awali.
Naibu Waziri anaendelea na ziara yake ya mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo anataria kutembelea mkoa wa Shinyanga, katika wilaya ya Kahama na Shinyanga Mjini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment