Sunday, 20 August 2017
MENO YA TEMBO 28 YAKAMATWA DAR
Waziri wa Maliasli na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema serikali imefanikiwa kukamata jumla ya meno ya tembo 28 katika ghala moja lililopo Mbezi Beach jijini Dar es salaam, yenye uzito wa takribani kilo 376.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Maghembe amesema meno hayo yaliyokamatwa tarehe 13 na 14 mwezi wa nane mwaka huu yanaonekana ni ya tembo waliouawa miaka ya nyuma ikikadiriwa kuuawa miaka ya 2013 au 2014 na wahalifu hao kuyaweka majumbani mwao huku wakiendelea kutafuta masoko.
Waziri Maghembe amesema tayari hadi hivi sasa watuhumiwa sita wa ujangili wameshakamtwa akiwemo Mohamedi Yahya Mohamed, almaarufu Mpemba, Aboubakar Zuberi Seguni mkazi wa Mbezi Beach ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali za mtaa na imamu wa msikiti wa Huda uliopo Mbezi, Juma Saleh Jebo mkazi wa Manzese jijini Dar es salaam, Hamisi Rashid Omary mkazi wa Mbezi, Amir Bakari Shelukindo Mkazi wa Gairo Morogoro na Ahmed Shabani Bakari mkazi wa Mkuranga.
Wakati akiwataja watuhumiwa hao, Waziri Maghembe alisema vita dhidi ya ujangili ni ngumu kwa vile hata baadhi ya watu wasiotegemewa katika jamii kujihusisha nayo nao wamo, akitolea mfano wa mtuhumiwa, Bakari Zuberi Seguni mkazi wa Mbezi Beach ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali za mtaa na imamu wa msikiti wa Huda uliopo Mbezi kuwa yeye ni mfano katika jamii kwa kuwa ni kiongozi wa kiserikali lakini pia ni mtu wa Mungu ambaye ni ngumu kufikiria ni miongoni mwa washirika wa biashara hiyo haramu.
Aliongeza kuwa, Tanzania kupitia Wizara yake inataka kufuta kabisa biashara ya meno ya tembo kama China walivyofanya licha ya kuwa uuzaji wa meno ya tembo kwa sasa mara baada ya kufuta soko la wazi imekuwa ikiendelea kwa njia ya mtandao.
Katika hatua nyingine , Waziri Maghemba alipaza sauti kwa mataifa kama vile Vietnam na Thailand kuacha kujihusisha na biashara hiyo na kuiomba jumuiya ya Kimataifa kuingilia ili tembo waendelee kuwepo kwa faida ya kizazi kijacho na badae na dunia kwa ujumla.
Aidha, Waziri Maghembe amesema Tanzania na Dunia kwa ujumla imepata pigo kubwa baada ya kutokea kwa mauaji ya Mkurugenzi wa Palm Foundation, Wayne Lotter raia wa Afrika Kusini yaliyotokea usiku wa jana Masaki jijini Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele katika kuisaidia serikali katika vita dhidi ya Ujangili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment