Tuesday 15 August 2017

MISRI KUWEKEZA MIRADI MIKUBWA YA KIBIASHARA


TANZANIA na Misri zimekubaliana kuhuisha ushirikiano wake kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kibiashara, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha nyama na dawa.

Pia, zimekubaliana kuiwezesha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kufanya upasuaji wa figo ifikapo mwaka 2020.

Haya yalielezwa jana na Rais Dk. John Magufuli, katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Ikulu mjini Dar es Salaam, akiwa na mgeni wake, Rais Abdel Fattah Al Sisi, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku mbili.

Rais Magufuli alisema viongozi hao pia wamekubaliana kufufua tume za ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, ili kusukuma mbele juhudi za kimaendeleo baina ya mataifa hayo mawili.

Maeneo mengine ya ushirikiano, ambayo viongozi hao wameafikiana kushirikiana ni pamoja na kuongeza fursa ya mafunzo kwa Watanzania nchini Misri katika utaratibu wa kubadilishana, ambapo Tanzania, itapeleka walimu wa Kiswahili na Misri itaongeza nafasi za masomo ya Teknolojia ya Mawasiliano na Sayansi kwa Watanzania.

Pia, alisema Misri imekubali kuleta wataalamu wa masuala ya kilimo, hususan cha umwagiliaji na ujenzi wa kiwanda cha dawa za binadamu.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Misri yenye watu wanaofikia milioni 93, inatumia asilimia tano ya ardhi yake katika kilimo, ikilinganishwa na Tanzania yenye watu wanaofikia  milioni 50, inayotumia asilimia 95 ya ardhi yake katika kilimo.

Alisema licha ya Misri kuwa na eneo kubwa la jangwa, uzalishaji wake katika sekta ya kilimo uko juu, ikilinganishwa na Tanzania, kutokana na matumizi mazuri ya kilimo cha umwagiliaji.

Rais Magufuli pia alisema katika mazunguzo yao, wamekubaliana na kufanya mazungumzo zaidi ya namna bora ya matumizi ya maji kutoka Mto Nile, ambao chanzo chake ni Tanzania, kwa faida ya mataifa yote mawili.

Kwa upande wake, Rais Al Sisi alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi bora, huku akipambana vilivyo na rushwa na ufisadi.

Pia, alipomngeza katika kuendeleza juhudi za kudumisha amani katika nchi za maziwa makuu, ikiwemo Burundi.

Kiongozi huyo pia aliipongeza Tanzania kwa kuhudumia wakimbizi kutoka mataifa yenye wakimbizi, juhudi alizosema zinapaswa kuungwa mkono na mataifa mengine Afrika.

Alisema katika mazungumzo yao, wameafikiana kuongeza kasi ya ushirikiano kutokana na historia ndefu ya mataifa hayo, tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser, ambao umekuwa nguzo ya ushirikiano uliopo.

Hadi sasa biashara baina ya Misri na Tanzania imefikia thamani ya dola milioni 78.02 huku uwekezaji uliofanywa na Kampuni za Misri nchini ukifikia dola milioni 887.07.

No comments:

Post a Comment