Thursday, 7 September 2017

SPIKA NDUGAI AWAVUNJA MBAVU WABUNGE



SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, jana aliwavunja mbavu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kusema ataomba iandaliwe semina ya kujifunza lugha ya kiswahili kwa wabunge wanaotoka mikoa ya kanda ya ziwa.

Ndugai alitoa kibomu hicho baada ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, kusema kuwa yupo tayari kutembea na mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya kwenda kwenye maeneo ya jimbo lake kushughulikia kero ya miradi ya umeme.

"Nilipokuja jimboni kwako, nilitembea sana na wewe na ninaomba nikija tena, niendelee kutembea na wewe,"alisema Dk. Kalemani alipokuwa akijibu swali la Magdalena.

Majibu hayo yaliwavunja mbavu wabunge, ndipo Spika Ndugai alipoingilia kati na kusema,
"Wewe msukuma, tumia lugha ya kibunge."

Mbali na kumtaka Dk. Kalemani atumie lugha ya kibunge, pia alisema atafanya mpango kupitia Wizara ya Elimu, ili wabunge kutoka kanda ya ziwa, waandaliwe semina kwa ajili ya kujifunza matumizi ya kiswahili fasaha bungeni.

"Kwa kuwa waziri wa elimu yupo hapa, nitazungumza naye ili wabunge kutoka kanda hiyo wandaliwe semina,"alisema Spika Ndugai na kuzidi kuwavunja mbavu wabunge.

Katika swali lake, Magdalena alitaka kujua ni lini serikali itajenga kituo cha umeme katika jimbo la Kaliua kutokana na kuwepo kwa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Spika Ndugai pia aliwavunja mbavu wabunge pale aliposema, atafanya mpango ili utaratibu  wa kuhakiki vyeti feki ufanyike kwa wabunge, kauli iliyopokelewa kwa shangwe na baadhi ya wabunge.

"Mnashangilia eeh? Nitamuagiza katibu wa bunge afanye mpango huo,"alisema Ndugai na kuongeza: Lakini kwa kuwa baadhi ya wabunge naona mmenuna na hilo halitekelezeki, halitafanyika."

Spika Ndugai pia alitoa ombi kwa Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa, kuliangalia upya suala la kuwaruhusu mabinti wa Tanzania, kwenda kufanyakazi Arabuni kwa kuwa wamekuwa wakinyanyasika.

Alisema kuwaruhusu mabinti hao kwenda kufanyakazi nje, kinyume na zile walizoahidiwa, ni sawa na utumwa, hivyo ni vyema serikali ilitazame jambo hilo kwa makini.

No comments:

Post a Comment