Thursday, 7 September 2017

WIZARA YA ARDHI YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA JPM



WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imesema imeanza rasmi kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kubadilisha ridhii za Dodoma, kutoka miaka 33 kwenda miaka 99, alilolitoa baada ya kuivunja Mamlaka ya Uatawishaji Makao Makuu(CDA).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri wa wizara hiyo, Williamn Lukuvi, alisema mpaka sasa wanazo nakala za hati 250,000, ambazo zote watazibadilisha bure bila gharama yeyote.

Alisema madhara makubwa ya ridhii hiyo ilikuwa mmiliki kutokuwa na uwezo wa kumpatia mwekezaji kutoka nje ridhii hiyo kwa asili ya shughuli za uwekezaji.

Lukuvi alizitaka taasisi za benki nchini, ambazo zina hati za aina hiyo na wamiliki kuzitumia kukopa, kuzirejesha katika wizara hiyo ili zibadilishwe na baadaye zitarejeshwa kwao badala ya wakopaji, ambao ndio wamiliki.

“Wizara yangu leo (jana), imeanza rasmi kutekeleza agizo la rais kubadilisha hati zote zilizokuwa zimetolewa na CDA na sasa tupo tayari kutoa hati za miaka 99,”alisema.

Aliwasihi Watanzania wote kufika kwenye jengo la Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili waweze kubadilishiwa.

Waziri Lukuvi alibainisha kuwa, mkoa wa Dodoma ndio pekee, uliokuwa ukimilikisha ridhii hiyo kwa  miaka 33.

“Ubadilisjhaji wote sasa utafanywa na serikali bila gharama yoyote, mtu yeyote Tanzania apeleke ridhii hiyo kwa msajili wa hati kanda ya Dodoma ili abadilishiwe,”alisema

Alisema baada ya kubadilishiwa, ataweza kuingia ubia kupitia hati hizo kwani zitakuwa za muda mrefu.

Waziri Lukuvi alisema, wanachopaswa ni kuhakikisha kuwa hawadaiwi ada yeyote ya ardhi kabla ya kwenda kubadilisha hati hizo.

Alisema hivi sasa wawekezaji wa nje wanaweza kuwekeza Dodoma kutokana na mabadiliko hayo.

Awali, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ilikuwa inapangisha watu kutokana na hati moja aliyopewa, ambayo hivi sasa imefutwa na kwa wale wapya, watakaokuwa wakichukua hati mpya, watapata moja kwa moja hati hiyo ya miaka 99.

Lukuvi alisema mikopo mingi duniani inakopesha watu wenye hati ya muda mrefu,
hivyo wakazi wa Dodoma walikuwa wakishindwa kupewa mikopo kutokana kuwa na ridhii ya miaka 33.

No comments:

Post a Comment