WATUMISHI wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wamefikishwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kutafuna sh. milioni 68, ambazo ni mishahara hewa.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Abdalla Marela, mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Kati ya fedha hizo, Marela alisema hadi sasa zilizorejeshwa ni sh. milioni 20 wakati fedha zingine sh. milioni 48 bado hazijarejeshwa.
Alisema kubainika kwa watumishi hao kutafuna fedha hizo, kumetokana na halmashauri hiyo kuwa na mtandao wake, ulioiwezesha kuwapata watumishi wote waliohusika kutafuna fedha hizo.
Alipohojiwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota, kuhusu hatua walizochukua baada ya kubainika kwa ubadhirifu huo wa fedha za halmashauri, mkurugenzi huyo alisema ni baada ya kufanyika kwa uhakiki.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini alisema kutokana na kubainika kuwepo kwa malipo hayo hewa ya mishahara, wamewaagiza viongozi wa halmashauri husika wavuliwe madaraka.
"Tulichofanya ni kuwaagiza walimu wakuu na wasimamizi wa maeneo ya kazi, ambako watumishi hao hewa walikuwa wakifanyakazi, wavuliwe madaraka,"alisema.
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Abdallah Malera kuhakikisha kitengo cha ukaguzi wa ndani kinapewa vifaa na fedha zake kwa wakati kama zilivyopitishwa katika bajeti.
Agizo hilo lilikuja baada ya kamati hiyo kubaini udhaifu katika kitengo cha ukaguzi wa ndani cha Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, hivyo kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Agizo hilo lilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Abdallah Chikota, baada ya kuhoji hesabu za Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Chikota alisema kitengo hicho kinapaswa kuwa huru katika utendaji wake wa kazi kulingana na umuhimu wake.
"Uhakikishe kuwa kitengo hiki kinapewa vifaa na fedha zake kama zilivyopitishwa katika bajeti tena kwa wakati,"alisisitiza makamu mwenyekiti huyo.
Alitolea mfano wa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16, ambayo ilipitishwa, ambapo
kulikuwa na sh.milioni 22, lakini kitengo hicho kilipewa sh.milioni 2, jambo ambalo haikubaliki na kwamba, kamati haitaki kusikia jambo hilo likijurudia.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Ndani wa halmashauri hiyo, Jonais Shayo, alisema katika mwaka huo wa fedha, alipewa sh. milioni mbili zilizotokana na fedha za ndani.
Aidha, kamati hiyo ilibaini kuwepo kwa bakaa ya fedha nyingi za miradi, ambazo hazikutumika katika utekelezaji wa bajeti katika mwaka huo wa fedha na kufanya miradi hiyo kuchelewa.
“Kwa mfano, kuna shilingi milioni 19.9, ambazo zilikuwa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji zimekaa hadi mwaka huu, ndipo mmeanza utekelezaji,”alisema.
Kufuatia hali hiyo, kamati ilimuagiza Sagini kuhakikisha anafuatilia fedha hizo kwa karibu ili mradi huo uanze utekelezaji kwa lengo la kutowakatisha tamaa wafadhili wa mradi huo ambao ni JICA.
Sagini alisema kuwa mradi huo ulichelewa kuanza kazi kutokana na serikali ya mkoa kuingilia kati ili kuangalia uwezekano wa fedha hizo kutumika kwa manufaa zaidi ya umma.
No comments:
Post a Comment