Thursday, 27 August 2015

SAMIA AWATIKISA MBOWE, LEMA




Na Epson Luhwago, Arusha

JIJI la Arusha jana lilizizima kutokana na maelfu ya watu kufurika
katika viwanja vya Samunge, vilivyoko katika eneo la Ngarenaro wakati mgombea mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipohutubia mkutano wa kampeni.

Mafuriko hayo ya watu yalidhihirisha wazi kuwa mbunge wa Arusha Mjini, aliyemaliza muda wake, Godbless Lema (CHADEMA) hana nafasi ya kurejea katika nafasi hiyo.

Aidha, kabla ya kutikisa ngome ya Lema, Samia alianza kuisambaratisha ngome ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wakati alipopata mapokezi makubwa na ya kihistoria wilayani Hai kabla ya kuhutubia umati wa watu kwenye mkutano wa hadhara.

Kujaa kwa watu hao ndani ya jiji la Arusha kuliwafanya hata viongozi wa kitaifa walioandamana na mgombea mwenza kupatwa na mshangao, kiasi cha kumfanya Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi, kutamka kwamba umati huo haujapata kutokea.

Watu hao hawakuletwa na mabasi wala malori kutoka sehemu mbalimbali za jiji hilo na vitongoji vyake, tofauti na watu wengine ambao wamekuwa wakifanya hivyo.

Maelfu ya watu hao walikuwa wakiburudika na kushangilia kila kiongozi aliyeko kwenye timu ya kampeni alipokuwa akisimama na kutoa neno.

SAMIA AFUNIKA
Hatimaye ulifika wakati wa Samia kuhutubia kuomba kura na kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambapo walikuwa wakishangilia kila hoja aliyokuwa akiitoa kutokana na kuwa na mashiko na kuwagusa wananchi wa kawaida.

Katika hotuba yake, Samia alisema serikali ijayo ya CCM itahakikisha inatatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Arusha Mjini na kuwaletea maendeleo.

Alisema serikali imeshaanza kulishughulikia tatizo la kiwanda cha
magurudumu cha General Tyre kilichoko Arusha.

Katika kufanya hivyo, alisema serikali imesharejesha umiliki wa kiwanda hicho mikononi mwake kwa kununua hisa alizokuwa nazo mwekezaji.

Neema nyingine aliyoitangaza ni  ujenzi wa kiwanda cha kuchakata
madini ya Tanzanite ili wafanyabiashara waache kuuza madini mithili ya nyama kwenye bucha.

“Haiwezekani Tanzanite ichimbwe Arusha, lakini ikatengenezwe Kenya au Afrika Kusini. Tutakikisha kiwanda kinajengwa Arusha ili kiweze kuwanufaisha Watanzania kwa kuchakata madini na pia kutoa ajira kwa vijana wa Arusha na Tanzania kwa ujumla,” alisema.

Kuhusu ajira, alisema hilo ni suala la kipaumbele na kwa upande wa
Arusha, serikali ijayo itahakikisha madereva wa magari makubwa na
madogo wanapata mikataba ya kudumu.
AWATIKISA MBOWE, LEMA
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameitikisa ngome ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kuwataka wananchi wa Jimbo la Hai kutomchagua kwa kuwa ni kikwazo kwa maendeleo.   
Mbowe, ambaye alikuwa Mbunge wa Hai kupitia chama hicho, amedaiwa kutoonekana mara kwa mara katika jimbo hilo tangu alipochaguliwa miaka mitano iliyopita, hivyo kutojali shida za wananchi.
Akihutubia katika mikutano ya kampeni iliyofanyika Machame na Masama jana, Samia alisema wananchi wa Hai hawana budi kujifunza na kutorudia makosa kwa kuchagua upinzani kwa kuwa umeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi.
“Miaka mitano iliyopita mlikuwa na huyu kaka (Mbowe), lakini hakuna alichofanya. Sasa chagueni huyu kaka kutoka CCM, Danstan Mallya, ili awe mbunge wenu na hatimaye ashirikiane na Dk. John Magufuli (mgombea urais wa CCM) na mimi katika kuleta maendeleo.
“Kamwe ndugu zangu wa Hai msifanye makosa kama yale ya nyuma kwa kuuchagua upinzani na matokeo yake huduma muhimu za maendeleo zimesimama,” alisema alipokuwa katika mkutano wa kwanza uliofanyika kwenye kijiji cha Kialia, Machame.
Kabla ya Samia kuhutubia, kada wa CCM, Sajenti mstaafu Seif Mkambala, aliimba shairi ambalo miongoni mwa beti zake lilisema;
Mbowe katika vijiji, lini kawatembelea,
Akafika kuwahoji, shida zinazotokea,
Mitano wajibikaji, nini alitufanyia,
Chagueni Sisiemu, mafiga yote matatu.

Kila siku mpitaji, chini hataki kutua,
Mtu ukimhitaji, simu anakufungia,
Kahamia kwenye jiji, kazi yake kutanua,
Chagueni Sisiemu, Mafiga yote matatu.

Shairi hilo liliwafanya viongozi na wanachama wa CCM waliofika katika mkutano huo kulipuka kwa furaha huku kinamama wakipiga vegelegele kuonyesha kukolewa na ujumbe uliotolewa.  
Samia alisema kwa kuichagua CCM, wananchi wa Hai watapata maendeleo kwa kuwa mbunge na madiwani wake watashirikiana na halmashauri ya wilaya na serikali kuu katika kupeleka huduma muhimu.
Katika kijiji cha Massama Mula, alikofanya mkutano wa pili, aliwasimamisha waliokuwa wakigombea ubunge kwenye jimbo hilo, Fuya Kimbita na Menrad Swai, ambao walivunja makundi kwa lengo la kuirejesha hai mikononi mwa CCM.
Hatua ya kuwakutanisha makada hao ambao walisababisha mpasuko baada ya kura za maoni, imesababisha CCM kuwa imara na walikiri kuwa wataunganisha nguvu zao kuhakikisha Chama kinapata ushindi.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Samia alisema serikali ijayo ya CCM itahakikisha inatatua kero ikiwemo ya barabara ya Machame hadi Masama na ile ya Masama hadi lango la Mlima Kilimanjaro.
Alisema ujenzi wa barabara hizo utasaidia kukuza uchumi wa wananchi pamoja na kuongeza pato litokanalo na utalii kwa kuwa wageni hao wanapokwenda Mlima Kilimanjaro, watakuwa wakipitia geti la Masama.
Pia alisema geti hilo litafunguliwa baada ya kufungwa miaka kadhaa iliyopita hivyo kusababisha uchumi wa wananchi wa Masama kushuka.
Sambamba na hilo, alisema tatizo la huduma duni za afya katika Hospitali Teule ya Machame litapatiwa ufumbuzi kwa kuwa amepata malalamiko kwamba huduma zinazotolewa ni za kiwango cha chini.
“Pia nimeambiwa kuwa kuna tatizo la vocha za pembejeo katika wilaya ya Hai. Tutahakikisha zinapatikana kwa wingi ili kuwawezesha wananchi kulima kwa wingi na kuinua kipato chao,” alisema.
Tatizo lingine ambalo aliahidi kulifanyia kazi ni uhaba wa mabweni katika shule za sekondari. Katika kulipatia ufumbuzi suala hilo, alisema mkazo mkubwa utakuwa katika ujenzi wa mabweni ili kuwaepusha watoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni.
Alisema watoto wengi wamekuwa wakishindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni na kurudi. Kutokana na hali hiyo, alisema atahakikisha serikali ijayo inafanya kila jitihada kujenga mabweni.
AHITIMISHA ZIARA SIHA
Samia jana alihitimisha kampeni kwa mkoa wa Kilimanjaro kwa kufanya mkutano kwenye jimbo la Siha, ambapo alisema utekelezaji wa Ilani umefanyika kwa asilimia 80 kwa kutatua kero mbalimbali za afya, elimu na maji.
Kutokana na mafanikio hayo, aliomba wananchi wa Siha kuichagua CCM ili kumalizia kazi iliyobaki ya kujenga mabweni, kusambaza umeme, ambao umeshaanza kusambaza maji na kuwawezesha wafugaji.
Pia alisema barabara ya Ngaranairobi itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo kuongeza kasi ya maendeleo.
Samia jana aliingia mkoani Arusha kuanza kampeni ambapo atatembelea majimbo yote. Jana jioni alifanya mkutano mkubwa katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwenye viwanja vya Majengo eneo la Usa River.
Wanachama 500 wahama CHADEMA
WANACHAMA zaidi ya 500 kutoka CHADEMA wamehama chama chao na kuhamia CCM mkoa wa Morogoro, huku wakieleza kuwa wana imani na Dk. Magufuli.
Wamesema migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji chini ya uongozi wa Dk. Magufuli itapatiwa ufumbuzi wa haraka hivyo, hawana sababu ya kuendelea kuwepo CHADEMA.
Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Rojas Romuli alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Alisema wanachama hao waliamua kuhama vyama vyao baada ya kusikia kauli ya Magufuli alipopita mkoani hapa mwishoni mwa mwezi uliopita na kuahidi kushughulikia kero hiyo ambayo ni kubwa kwa mkoa wa Morogoro.
Alisema wanachama hao wengi wao ni kutoka wilaya ya Ulanga katika jimbo la Ulanga Magharibi ambapo ni jamii ya wafugaji.
Hata hivyo, katibu huyo alisema wanachama na wananchi hao kwa ujumla wanaimani na CCM kutokana na utekelezaji wa ilani yake sambamba na ahadi wanazotoa zinatekelezeka kwa asilimia kubwa.
Alisema sababu kubwa ambayo itakiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi ni pamoja na kuteua wagombea bora, ambao wanauzika kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuwarudisha wagombea asilimia kubwa waliochaguliwa katika kura za maoni na jamii husika.
Alisema hadi sasa zaidi ya kata tano katika mkoa wa Morogoro wagombea wake wamepita bila kupingwa na kwamba bado pingamizi zingine zinaendelea kushughulikiwa.

No comments:

Post a Comment