NA CHRISTOPHER LISSA
KWANZA nilipongeze Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam chini ya
Kamishna shupavu Suleiman Kova kwa uamuzi
makini wa kukemea ‘rafu’ inayoonekana kuanza kuchezwa na baadhi ya wagombea wa urais,
hasa mgombea wa CHADEMA, Waziri
Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa chafu ya Richmond, Edward Lowassa.
Tunajua wenye midomo wataongea sana, hasa wale ambao
kazi yao ni kupinga kila jambo linaloamriwa na serikali na vyombo vyake vya dola, hata kama ni jema
na lipo kwa ajili ya maslahi yao wenyewe.
Hii ndiyo hulka iliyojengeka katika vichwa vya wengi.
Kukinzana na maamuzi ya serikali na vyombo vyake, kushindwa kutii mamlaka ,
sheria, taratibu, kanuni na hata tamaduni za kimazoea zilizopo.
Lakini ni wepesi wa kulaumu na kulaani vyombo vya dola
na serikali pindi kasoro ndogo inapojitokeza. Kwa lugha nyingine wagumu wa kuelewa wepesi
wa kusahau.
Tunaamini kuwa Jeshi la Polisi hapa nchi liko makini na
maamuzi yake kama haya ambayo kwa wengine wanachukulia kwa wepesi wepesi.
Ametajwa Lowassa
kama mfano tu wa waasisi wa
kampeni za ‘rafu’ kwa sababu ndiye aliyeonekana kuwa ‘wasanii’ kuliko wagombea
wengine ambao wako makini na timamu.
Tunajua kuwa hatua hii ya Jeshi la Polisi si ya
kukurupuka kwa sababu Lowassa, juzi
alionekana akirandaranda katika vituo na
ndani ya mabasi ya dadalada.
Pia Jeshi la
Polisi mkoa maalumu wa Ilala, juzi lilimzua kufanya ziara holela baada ya kuingia katika mtaa wa Swahili na wapambe wake na kutaka kuingia Soko la Kariakoo, akitokea soko la Tandale,
Kinondoni.
Hata hivyo, Lowassa alipigana chenga na Polisi na
kuonekana wilayani Temeke akiendeleza utaratibu wake wa kampeni. Hili
linastahili kulaaniwa.
Kisingizio chake kikubwa ni kuzungumza na wafanyabishara
na wananchi ili kujua matatizo yao, wakati anaelewa fika kuwa ratiba ya kampeni
aliyonayo mkononi haionyeshi kwamba
atapita maeneo hayo kwa kipindi hicho. Kufanya hivyo ni kinyume cha utaratibu.
Nasema hivyo kwa sababu najua kuwa Lowassa na wapambe
wake ni watu wenye akili timamu. Watu
wanaoelewa kanuni zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), juu ya
utaratibu wa kampeni pamoja na kukabidhiwa
ratiba rasmi, ambayo wanatakiwa kuifuata, hawawezi kufanya vitu kama
hivyo.
Inashangaza kuona
kuwa Lowassa anaanza kwenda kinyume kwa kudandia
daladala na kufanya kampeni zisizo na msingi pasipo kufuata ratiba aliyonayo
mkononi.
Kwa nini anafanya mchezo huu wa kuchepuka? Kwanini
asibaki njia kuu ambayo inamuelekeza
afuate ratiba?
Inashangaza mtu kama Lowassa ambaye aliwahi kushika
nyadhifa za juu hapa nchini ukiwemo
Uwaziri Mkuu na anajua masuala ya itifaki na usalama aanze
kupanda daladala kiholela na kutengeneza picha zisizo na msingi.
Katika miaka yote
ambayo Lowassa tumemfahamu sijawahi
kumuona akipanda Daladala. Au
ndiyo kutafuta adidu za rejea
katika Ilani ya Ukawa? Waswahili
wanasema kutafuta ‘Kiki’.
Kitendo cha Lowassa kuonekana kunywa maziwa kwa
mamantilie Tandale, hasa wakati huu
ambapo Serikali inapambana na
mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu
huku Tandale likiwa ni eneo ambalo limetajwa kuongoza kwa maambukizi ya
ugonjwa huo ni upotofu wa mawazo
yakinifu.
Kwa lugha ya mtaani
unaweza kusema huu ni usanii wa wazi ambao au kiini macho ambacho kiukweli kinaonesha ni jinsi
gani mgombea huyo anavyojaribu
kulaghai watanzania kwa uchu wa kuingia
Ikulu kwa kutumia upanga wake wa fedha.
Hizi ni kampeni
za kejeri. Kampeni za kiini macho kwa wananchi. Kampeni holela. Kampeni chafu.
Kampeni zisizo na mashiko.
Ni kwa miaka mingapi Lowassa aliwahi kuonekana Sokoni na
kapu au kuwasabahi wafanyabishara na kujua matatizo yao? Leo
huyu Lowassa anaonekana akigalagala
na kina Mama ntilie, makondakta na watu
wanaobangaiza akijifanya Malaika mtakatifu na mwokozi wao.
Uamuzi huu wa kampeni holela, unatia hofu juu ya uwezo
wa kufikiri na wa kimaamuzi wa inayojiita ‘Timu Lowassa’. Potelea mbali ‘Timu Ukawa’ ambayo tunajua inaburuzwa kimaamuzi. Haina sauti.
Imetulizwa kama siyo kufumbwa mdomo.
Nasema inaburuzwa kwa sababu haingii akilini kama wangeweza kukubaliana na kampeni kama hizi
zisizo na mashiko.
Nazijua kampeni za CHADEMA zilivokuwa zikifanyika wakati
alipokuwepo Katibu Mkuu wao
Willybroad Slaa, aliyejiuzuru kutokana
na kutokukubaliana na hatua ya chama
hicho kumpokea mtu kama Lowassa.
Zilikuwa ni
kampeni za uhakika na za kuheshimu mamlaka husika.
Lakini pia sina shaka kwamba kwa jinsi ninavyomfahamu
Lowassa sitashangaa sana kama nikiambiwa
kuwa maamuzi ya kulandalanda mitaani, kuonjaonja maziwa na visheti, yametoka katika kichwa chake mwenyewe. Kwa hilo sina wasiwasi kwa sababu namjua kwa
maamuzi yake.
Nakumbuka kipindi akiwa Waziri Mkuu kabla ya kushambuliwa kuhusika na kashfa
chafu ya Richmond, aliwahi kuja na wazo
la moango wa kutengeneza mvua baada ya nchi kukumbwa na
ukame. Eti mvua ya kutengenezwa Tanzania.
Kwanini tusiamini hii leo kuwa Lowassa anaweza kushauri
apande Daladala na kukaa vijiweni kuonja
maziwa kama sehemu ya kampeni? Au aende
kutalii sokoni ? Kwa uwezo wake wa kufikiri hili linawezekana kuwa ni wazo lake
la kiubunifu haswaa.
Hii ndiyo athari ya kuitikiwa ya waliokuwa viongozi wa Chadema na Ukawa
kufanyangwa kifikra na kuwa waitikiaji wa ‘Ndiyo Mzee’ kwa kila atakalotamka.
Ndiyo! Nafahamu kwamba kama si wazo la ubunifu lililotoka katika kichwa chake na kuitikiwa
‘Ndiyo Mzee’ basi angelikataa kwa
sababu anaelewa fika kuwa si utaratibu,
haifai na ni kinyume cha ratiba.
Ninaamini kuwa
Lowassa ndiye aliyekabidhiwa kanuni
na taratibu za kampeni, hivyo
asingiweza kukiuka mapema namna hii hata
kabla ya CHADEMA kuzindua kampeni zake.
Nasema haya kwa
sababu, kwanza ni hatari kwa
mgombea kama Lowassa kuzurula mitaani na kufanya kampeni holela pasipo ulinzi makini.
Nilipongeze tena jeshi la Polisi kwa uamuzi huu makini
kwa sababu wao ndiyo wabeba lawama pindi majanga yanapotokea.
Lakini si kwa Lowassa tu, bali hata
wagombea wengine ambao wanawaza
kufuata nyendo hizo chafu, kutii taratibu zilizopo na kuheshimu maagizo yanayotolewa na vyombo vya dola.
Pia kufuata ratiba ya kampeni inayotambulika na NEC,
vyama vyao na vyombo vingine likiwemo Jeshi la Polisi. Nimalizie kwa kumuasa Lowassa ‘michepuko ya kampeni siyo dili, afuate njia kuu ambayo
ni ratiba ya kampeni.’
No comments:
Post a Comment