Tuesday, 5 January 2016

MABALOZI WATATU WAJITAMBULISHA KWA RAIS MAGUFULI




RAIS Dk. John Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, jana, ilisema hafla hiyo ilifanyika Ikulu, mjini Dar es Salaam.

Msigwa alisema mabalozi waliokabidhi hati zao za utambulisho ni Balozi wa Jamhuri ya Korea, Song Geum-young, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland Van de Greer na Balozi wa Palestina, Hazem Shabat.

Akizungumza na mabalozi hao kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli aliwapongeza kwa kuteuliwa kuja kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewaahidi kuwa serikali yake itatoa ushirikiano kwao ili shughuli zao ziweze kufanikiwa.

Aidha, Rais Magufuli alisema Tanzania inatambua matokeo ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi hizo na amewahakikishia mabalozi hao kuwa ushirikiano huo utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wao, mabalozi waliokabidhi hati zao za utambulisho walimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri alioanza nao tangu alipoapishwa kuwa rais na kwamba, wapo tayari kutoa ushirikiano hususan katika
shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment