NA SELINA WILSON, KWELA
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema akichaguliwa kuwa rais, atarejesha heshima ya Jeshi la Polisi kwa kuwapa mamlaka ya kushughulikia matatizo yao haraka.
Amesema ataboresha maslahi ya polisi ili wasichukue rushwa ndogondogo zinazosababisha kero kwa wananchi, lakini anatambua wapo askari wengine wema ambao hawachukui rushwa.
Dk. Magufuli aliyasema hayo, alipozungumza na wananchi katika Kata ya Laela katika jimbo la Kwela, katika mkutano wa kampeni ambapo, alisema anahitaji kurejesha heshima ya jeshi.
“Najua kuna matatizo mbalimbali ikiwemo maslahi. Maslahi nitayazingatia ili wasichukue rushwa ndogondogo kwa wananchi. Wapo wachache wanaochukua rushwa, lakini wengine ni wema,”alisema.
Alitoa mfano wa askari mmoja aliyekuwepo kwenye eneo hilo,” Mnamuona huyo askari wangu, amekonda kwa sababu ya kufanya kazi. Huyo hachukui rushwa, anafanya kazi yake vizuri, hivyo inabidi tuboreshe maslahi yao,”.
Hata hivyo, alisema pia kwamba atalishughulikia suala la watu kuchezea jeshi la polisi, badala yake atawapa mamlaka makubwa ili waweze kufanya kazi zao vizuri.
“Mambo ya mtu jambazi anakuja, unasubiri polisi jamii, nitahakikisha mnachukua hatua. Haya ndio yanapunguza nidhamu ya jeshi la polisi.
“Wewe unakwenda kumchokoza mtu ana SMG, halafu aache kukushughulikia, tutakuwa na jeshi lenye nidhamu, halitaonea mtu, lakini litimize wajibu wake,” alisema.
Alisema anataka kujenga Tanzania iwe nchi ya amani, lakini polisi wafanye kazi yao vizuri na kurejesha heshima na nidhamu.
Dk. Magufuli alisema ataboresha mishahara ya wafanyakazi wote, lakini kila mmoja atimize wajibu wake, aliyepo juu atimize wajibu wake na aliye chini atimize wajibu wake.
Kiboko ya mafisadi
Alisema anajua kuna changamoto nyingi ikiwemo migogoro ya mashamba, lakini hakutakuwa na watu kudhulumiwa, bali anataka kila mtu afanye kazi na apate haki yake.
Alisema wapo wakubwa wenye tabia hizo wanamtambua misimamo yake, hivyo atahakikisha analala nao mbele kwa mbele na kuwashughulikia.
“Mimi ni kiboko yao. Wananifahamu ndio maana waliposikia nimeteuliwa kuwania urais wamekimbia. Si mmeona wamekimbia wenyewe jamani. Nitalala nao mbele kwa mbele nitawapandia huko huko juu,”alisema.
Katika hatua nyingine, Magufuli alisema katika eneo hilo la Laela, kuna tatizo la maji ambalo limekaa muda mrefu bila kukamilishwa, hivyo alionya wahandisi kuhakikisha mradi huo unakamilishwa mara moja.
Dk. Magufuli alisema katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ya wananchi, hatakuwa na utani na kwamba yeye ni msema kweli, hivyo Mhandisi wa Maji wa eneo hilo ajiandae.
Alisema akiwa wizara ya ujenzi, amefukuza makandarasi 3,200 kutokana na sababu mbalimbali, hivyo akiwa rais hatashindwa kusimamia na kuhakikisha wananchi wanapata huduma na maisha bora.
Sijawahi kufukuzwa, kujiuzulu
Katika hatua nyingine, akizungumza katika mikutano mbalimbali, Dk. Magufuli alisema amekuwa katika utendaji serikalini kwa miaka 20, akiwa waziri na hajawahi kukemewa, kufukuzwa au kujiuzulu.
“Mimi ni kiongozi niliyefanya kazi kwa uadilifu na uaminifu. Nimekuwa kwenye uongozi miaka 20, nilikuwa nawaheshimu viongozi wangu, wananituma kazi, nazifanya kwa uadilifu.
“Sikuwahi kukemewa, sikuwahi kufukuzwa wala sijawahi kujiuzulu kwa sababu zozote zile. Miaka 10 mfululizo nimepita bila kupingwa kwenye ubunge, watu wote wamekuwa na imani na mimi bila kujali itikadi, waliniamini,” alisema.
Alisema baada ya miaka 20 ameona anatosha kuwa rais na anawashukuru viongozi waliomtangulia kwa kumpa maelekezo ambayo yamemfanya aweze kufanya kazi kwa mafanikio makubwa.
“Ndugu zangu nawaahidi sitaruhusu watendaji wabovu. Nitahakikisha nakuwa rais wa Watanzania wote. Nitawabana watendaji ili mradi wafanye kazi za wananchi,” alisema.
Dk. Magufuli alisisitiza kukomesha wizi wa dawa na kuwaonya kwamba hatawaacha waendelee kufaidika na magonjwa ya watu.
“Watu wasifaidike na magonjwa ya watu. Nitahakikisha dawa zinapatikana hospitalini badala ya kwenye maduka yaliyoko karibu na vituo vya huduma,” alisema Dk. Magufuli.
Ashusha gharika Tunduma
UMATI mkubwa wa maelfu ya wanachama na wananchi wamejitokeza kumlaki Dk. Magufuli katika mkutano wa hadahara uliofanyika katika uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Tunduma.
Vijana waliovalia sare za CCM walionekana kupagawa kwa furaha na kulazimika kuzunguka kwenye uwanja huo huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kusema ‘Tunamtaka Dk. Magufuli awe Rais wetu’.
Wakati wote wa mkutano huo, walikuwa wakizunguka uwanja huo na kupeperusha bendera za CCM hadi Dk. Magufuli alipomaliza kuhutubia.
Shamra shamra hizo ziliwakuwasanya wanawake kwa wanaume, ambao wakati wote walikuwa wakicheza nyimbo za Chama na kutangaza kwamba wana akili timamu na Dk, Magufuli ndiye rais wao.


No comments:
Post a Comment