Thursday 27 August 2015

RED BRIGADE YATISHIA USALAMA WA UCHAGUZI

KAMISHNA Paul Chagonja
JAJI Francis Mutungi

NA MWANDISHI WETU
KIKUNDI cha ulinzi cha Red Bridged cha CHADEMA, kimetakiwa kudhibitiwa haraka ili kuepusha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa raia.
Imeelezwa kuwa iwapo hakitachukuliwa hatua za haraka, kinaweza kuingilia shughuli za vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Hivi karibuni, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA wanaounda kikosi hicho mjini Mbeya, waliingilia kazi za polisi wakati wa mkutano wa mgombea urais wa chama hicho uliofanyika mjini humo.

Katika mkutano huo, wana kikundi wa Red Bridged walionekana wakiranda huku na kule kwa kutumia gari linalofanana na yale yanayotumiwa na polisi wakati wa doria.

Akiwasilisha mada kwenye mdahalo wa kujadili amani na usalama wakati wa kampeni na uchaguzi mkuu, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, James Jesse, alisema shughuli za vikundi vya ulinzi vinavyotumiwa na vyama vya siasa zinapaswa kutazamwa upya.

Mhadhiri huyo bila ya kukitaja kikundi hicho, alisema baadhi ya vikundi vinapaswa kutazamwa vyema kwa kuwa vinaweza kutishia amani na usalama wa nchi.

Alisema kikundi hicho kimekuwa kikijihusisha na shughuli ambazo ni wazi zinakiuka lengo la uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi.

"Kila mmoja anakumbuka kilichotokea hivi karibuni wakati baadhi ya wanasiasa wakiwa kwenye matukio ya kisiasa, walionekana wanakikundi cha ulinzi wakitumia sare na mavazi kama ni moja ya vikundi rasmi vya ulinzi wa nchi.

"Ni vema hatua zikachukuliwa kwani kwa taarifa zilizopo, vikundi hivyo vimekuwa vikitoa mafunzo mfano wa yale yanayotolewa kwa vikundi rasmi vya ulinzi wa nchi.

"Iwapo haya hayatashughulikiwa sasa, huko tuendako tunaweza kuingia kwenye matatizo," alisema.

Wakichangia mada hiyo, baadhi ya washiriki wa mdahalo, walisema ni vyema vikundi kama vya ulinzi hususan Blue Gurd, vinapaswa kupewa mwongozo maalumu wa kisheria na si kuendeshwa kienyeji.

Jaji John Mkwawa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), aliyekuwa akimwakilisha mwenyekiti wa tume hiyo, alisema ni vyema hatua mahsusi za kisheria zikachukuliwa kuzuia uvunjifu wa amani unaoweza kufanywa na vikundi hivyo.

Jaji Mkwawa alisema hata vyama vwa siasa ambavyo asili yake vilitokana na wapiganaji wakati wa kudai uhuru, hivi sasa havina vikundi vya ulinzi mfano wa hivyo vinavyolalamikiwa.

Alisema ikiwa kutatungwa sheria maalumu kuhusu vikundi hivyo, itasaidia kubainisha kazi zake na mipaka ambayo vinapaswa kuifuata na kuizingatia.

Kwa mujibu wa Jaji Mkwawa, ili kuendeleza utulivu ni vyema vikundi hivyo vikaundiwa utaratibu mahsusi.

Akizungumza kuhusu vikundi hivyo, Mkuu wa Operesheni na Mafunzi wa Jeshi la Polisi,  Kamishana wa Paul Chagonja, alisema vikundi hivyo vinapaswa kujisajili na kujipambanua ili viweze kutambulika rasmi.

Hata hivyo, alisema vitapaswa kuwa na mipaka ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa yapo baadhi ya mambo, ambayo havipaswi kuyaamua au kuyachukulia hatua.

"Bila shaka umefika wakati kwa vikundi hivi sasa kujisajili kama ambavyo zinafanya kampuni za ulinzi.

"Hata baada ya kufanya hivyo yapo baadhi ya mambo ambayo havipaswi kuyafanyia kazi bali inapaswa kuviachia vyombo husika ikiwemo polisi.

"Hata askari wa kampuni za ulinzi wana mipaka yao, kuna baadhi ya mambo ambayo tunawaambia kwamba hilo hawaruhusiwi kulifanya waliache mikononi mwa polisi," alisema.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Alhad Mussa Salum, alisema ni vyema suala la kukabiliana na vikundi hivyo likafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Alisema hakuna kitu bora na cha muhimu kuliko amani ya nchi, hivyo chombo au kikundi chochote kinachoashiria kuvunja amani kinapaswa kukabiliwa.

Akichangia hoja hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema hakuna haki isiyo na wajibu.

Alisema kila taasisi vikiwemo vyama vya siasa vinapaswa kuzingatia kuwa hakuna haki isiyo na wajibu.

"Kila chama kitimize wajibu wake kabla ya kudai haki," alisema.

Katika hatua nyingine, Kamishna Chagonja alisema jeshi hilo linawataka viongozi wote hususan wagombea wa nafasi mbalimbali kuzingatia ratiba ya kampeni  waliyoiwasilisha polisi.

Alisema polisi haiwezi kukaa kimya endapo mgombea yeyote hususan wa urais ataacha ratiba iliyowasilishwa kwenye vyombo vya ulinzi na kwenda maeneo mbalimbali kienyeji.

"Wako wagombe leo hii wanatoka na kwenda mitaani ambako wanaonja uji na mambo mengine wakiwa hawana ulinzi wetu, lakini jambo lolote likitokea huko ni sisi ndio tutakaolaumiwa, hivyo hatuwezi kuliacha jambo hilo litokee," alisema.

Kauli ya Chagonja inakwenda sawa na taarifa ya NEC, ambayo imevitaka vyama vyote kuacha kufanya mikusanyiko ambayo haipo katika ratiba ya kampeni ya rais.

Kauli ya NEC imekuja siku chache baada ya mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa kuonekana kwenye maeneo mbalimbali ambako inadaiwa alikwenda kuona maisha mbalimbali ya wana-Dar es Salaam.

ACT YAIKATAA
Katika hatua nyingine, Chama cha ACT Wazalendo kimesema kwa sasa CHADEMA si chama cha upinzani bali ni CCM B inayokusanya makapi kuua upinzani nchini.

Imeitaka CHADEMA kuacha ufinyu wa kufikiri kwa  kuwarubuni Watanzania na pia imetangaza kuzindua kampeni zake Jumapili hii katika viwanja vya Zakiem Mbagala, Dar es Salaam ambapo viongozi wa kitaifa akiwemo Zito Kabwe, Samson Mwigamba, Anna Mghirwa na wagombea ubunge wote watahudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mipango na Mikakati wa ACT, Habibu Mchange, alisema katika kampeni zake, chamahicho kitahakikisha kinafanya siasa safi na kuinadi ilani ya uchaguzi na kauli mbiu ya utu, uzalendo na uadilifu.

Alidai CHADEMA imekuwa ikikihujumu chama chake kwa muda mrefu na kutumia makapi ya CCM kusema uongo ili kuhakikisha chama hicho kinakufa.

Alisema  kwa sasa chama hicho kimebuni mbinu mpya, ikiwemo kushambulia viongozi wa ACT katika mikutano, kushusha bendera, kuchana mabango na kuvunja matawi ya chama hicho.

Mchange alisema chama chake kinatoa siku saba na kutoa taarifa polisi ili ishughulikie vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyodaiwa kufanywa na CHADEMA.

Alidai hivi karibuni, chama hicho kilitumia vijana wa Red Brigade kumshambulia katibu Mwenezi wa ACT jimbo la Manonga, Juma Pius, aliyelazwa Hospitali ya Wila ya Igunga.

Alidai ACT inao ushahidi wa tukio hilo kufanywa na vijana hao, ikiwa ni maagizo kutoka kwa kiongozi mkubwa wa CHADEMA na matukio mengine ikiwemo kubomoa  tawi la Mtogole na kushambulia mikutano mbalimbali.

Alisema busara ni muhimu na kupambana kwa hoja katika siasa na kwamba CHADEMA hawana jipya zaidi ya kutawaliwa na hofu kwa kuwa wanajua wanafanya siasa za kitoto.

Kwa upande wake, Katibu wa Fedha na Rasilimali wa ACT, Peter Mwambuja, alisema CHADEMA wanatambua kuwa siasa za uongo wanazozifanya zimepitwa na wakati na wamekizushia vitu vingi ACT ikiwemo kufadhiliwa na mgombea urais, Edward Lowasa na Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, lakini sasa wanaona aibu kwa kuwa wameshindwa kuficha fedha za viongozi hao zinakwenda wapi.

Alisema walipiga kelele sana kuwa fedha ya Lowassa ni chafu na inatumika kuifadhili ACT, lakini sasa wanatumia nguvu nyingi kuficha ukweli kwa kuwa fedha ya Lowassa imekuwa safi kwao.

No comments:

Post a Comment