Sunday 30 August 2015

REKODI YA DK. MAGUFULI YAMSHINDA LOWASSA, ATUMIA DAKIKA NANE KUZUNGUMZA, ILANI YA UKAWA YAKOSEKANA





NA WAANDISHI WETU

MGOMBEA urais wa CHADEMA na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, jana alishindwa kuhimili mikiki ya kampeni, hivyo kutumia dakika 11 kuhutubia wafuasi wao katika mkutano wake wa uzinduzi wa kampeni.

Lowassa ambaye alipanda jukwaani saa 11:40 jioni alishuka saa 11:52 na muda mwingi tangu kuingia katika Viwanja vya Jangwani mahali walipozindulia kampeni alionekana mnyonge huku akitembea kwa kuburuza miguu hali iliyozua hofu kwa wananchi.

Wakati akizindua kampeni zake za urais wiki iliyopita, mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, alitumia dakika 58.

Aidha, aliwasikitisha zaidi wafuasi wake kushindwa kutumia muda wake kunadi ilani ya chama chao na badala yake aliwataka wananchi wakavisome katika tovuti ya chama chao ambayo hata hivyo alishindwa kuitamka kwa ufasaha na hata wananchi walipomuomba kurudia kuitaja hakufanya hivyo.

CHADEMA na UKAWA ambao walizindua kampeni zao, watu waliofika walilalamika kukosekana kwa utaratibu.

Pia, licha ya kushindwa kuzungumzia mipango ya Ilani ya chama chake, Lowassa alizidisha machungu kwa wakulima baada ya kusisitiza serikali yake atakayoiunda itaendelea kukopa mazao yao.

Alisema wataendelea kukopa mazao ya wakulima na kulipa kwa riba, kitendo ambacho serikali ya CCM kupitia  mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli, kusisitiza kuwa hakitakuwepo.

Katika mipango ya utekelezaji wa ilani ya CCM, Dk Magufuli, alisema suala ya wakulima kukopwa mazao yao  halitakuwepo.

Kupitia serikali itakayoundwa na CCM, mkulima atalipwa fedha zake kwa wakati na kwa bei nzuri.

Licha ya kupeleka kilio kwa wakulima, Lowassa alionyesha wazi kuwa serikali yake itaingilia uhuru wa mahakama baada ya kutangaza kuwatoa gerezani viongozi wa kundi la Uamsho wanaoshikiliwa kwa tuhuma za uchochezi.

Kesi dhidi ya viongozi hao tayari iko mahakamani, muhimili ambao huendesha mambo yake kwa misingi ya haki pasipo kuingiliwa na mtu au serikali.

Katika hali iliyoonyesha kuwa Lowassa na chama chake hawakujipanga kuwaelezea wananchi namna gani watavyowasaidia, alisema serikali itamtoa gerezani mwanamuziki Nguza Viking Babu Seya’ na mwanawe Johnson Nguza ‘Papi Kocha na ‘kumrejesha duniani’ aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), marehemu Daudi Balali. Balali alifariki dunia Mei 20, 2008 nchini Marekani.

“Nimesikia nitamtoa Babu Seya na kumrejesha  Balali”, alisema Lowassa.

Kauli hiyo ilizua maswali kutoka kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza, waliosikika wakidai kuwa mgombea huyo anawafanyia maigizo ya kisiasa badala ya kuwaelezea namna atakavyoweza kutatua kero za wananchi.

“Sasa hii kali ya kumfufua marehemu, hivi Watanzania tuna mahitaji hayo ya Balali na Babu Seya. Hatuwezi tukaendeshwa na serikali ya maigizo,” alisema mmoja ya wananchi hao.

Wakati Lowassa akiendelea na hotuba yake, watu walianza kuondoka kana kwamba mkutano wake ulikuwa umemalizika.

Wananchi hao  walisema, uwezo wa Lowassa kuzungumza na kueleweka bado mdogo, huku wakidai udhaifu wa afya yake unachangia.

Mara kadhaa mgombea huyo alijikuta akikumbushwa na baadhi ya maofisa wa chama chake kwa kunong’onezwa na kupewa vijikaratasi kutoka meza kuu baada ya  kuonekana kugusia baadhi ya masuala ambayo yameahidiwa katika Ilani ya CCM.

Kwa mujibu wa Lowassa miongoni mwa vitu atakavyofanya ni kuboresha hospitali na ujenzi wa reli ya kati, jambo ambalo limeshatiliwa mkazo na CCM katika utekelezaji wake.

SUMAYE NAYE

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alijitosa kumtetea Lowassa ilhali  alipotangaza kuomba ridhaa ya CCM awanie urais, ndiye aliyetamka hawezi kumuunga mkono kwa kuwa ni mgonjwa na hayuko tayari nchi iongozwe na rais asiye na afya njema iwapo CCM ingemteua.

Katika hali ya kushangaza Sumaye ambaye ndiye aliyeeleza juu ya hofu ya afya ya Lowassa na hatima ya urais, jana aliendelea kukiri kuwa Lowassa ni mgonjwa, lakini akimtetea kuwa atatibiwa Ikulu akiwa rais.

Sumaye alidai Lowassa kuwa mgonjwa si hoja kwa kuwa marais hutibiwa nje ya nchi wakiwa madarakani, hivyo achaguliwe pamoja na hali yake kutokuwa nzuri kwa kuwa atatibiwa akiwa Ikulu.

WAFUASI WAHOJI

Wafuasi wa vyama hivyo walisikitishwa zaidi na hali ya mgombea wao kushindwa kusimama na  kuhutubia kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.

“Kwa kweli hali ya mgombea wetu ni mbaya afya sio nzuri  anaumwa na amechoka tuombe mungu amtie nguvu asije kudondoka maana hata kuinua miguu hawezi lakini tupo pamoja naye,” alisema.

Licha ya dosari hiyo, walilamikia kukaa muda mrefu katika viwanja hivyo bila kuwepo kwa utaratibu na viongozi wao kufika jioni huku wakiwa hawana sera inayoeleweka ya kile walichokitaja kuwa matumaini  wanayoyasema.

VIBAKA WAIBA, POMBE NJE NJE
Katika hatua nyingine mkutano huo ulikuwa na vurugu nyingi, hali iliyosababisha kinamama kupoteza watoto.

Aidha vurugu hizo zilisababisha watu waibiwe simu na kufikia hatua ya kuomba uongozi uliopo mbele kutoa  msaada ambapo hata matangazo yalipotolewa hakuna aliyepata mali yake.

Vurugu hizo zilisababisha baadhi ya wafuasi hao waliokuwepo katika mkutano kurushiwa chupa za maji.

Kamera za gazeti hili pia zilifanikiwa kunasa matukio ya unywaji pombe na watoto wadogo waliokuwa wamevalishwa nguo za CHADEMA, lakini walioonekana kana kwamba walilazimishwa.

Hali ya usalama ilikuwa mbaya kiasi cha watu mbalimbali kupoteza mali zao zikiwemo simu na mikoba kwa kinamama.

DK. SLAA, PROF. LIPUMBA WAYEYUKA

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim wameendelea kukacha hafla zinazomhusisha Lowassa kugombea urais.

Wanasiasa hao hawakuonekana katika kampeni za CHADEMA na UKAWA kama ilivyokuwa ikienezwa na baadhi ya viongozi wa umoja huo ambao walitamba kuwa wangekuwa nao.

Dk. Slaa ambaye alijiuzulu baada ya Mbowe kumuingiza Lowassa ndani ya chama hicho hajulikani aliko mpaka sasa.

Aidha viongozi wa CHADEMA walishindwa kumzungumzia mwanasiasa huyo wala wale wa CUF kuzungumzia aliko Profesa Lipumba.

VIONGOZI WA DINI
Viongozi wa dini waliohudhuria na kuhudumu kwenye uzinduzi huo, walionyesha dhahiri kununuliwa kutokana na sala zao kujaa vijembe, maneno ya dharau na kuyaelekeza kwa viongozi wa chama tawala (CCM) na serikali.

Hali hiyo iliwashangaza wananchi ambao si wafuasi wa vyama hivyo vinavyounda Ukawa, waliofika kwenye viwanja hivyo kusikiliza ilani ambayo ilisemekana ingetolewa, ambapo walisema sala imefanyiwa mzaha.

“Hawa wanaigiza, sala gani ile sasa? Wanacheza na Mungu hawa! Utamwombeaje mwenzako ubaya wa namna hiyo kisa tuu hayuko pamoja na unachokiamini? Lazima watakuwa wamelipwa, inashangaza sana haya ni maigizo,” walisema.

Katika sala hizo zilizotolewa na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo ambayo kwa niaba, ilitolewa na kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, zilikuwa na maneno ya kejeli yaliyoonesha ni ya kipambe.

Mojawapo wa maneno hayo ni kuombea watu wasio pamoja na vyama hivyo hasa Chadema kuwa wapate saratani ya damu na ugonjwa wa viziba mkojo ili UKAWA iendelee na harakati zake za kuelekea ikulu - maneno ambayo yaliwaacha watu midomo wazi.


POLEPOLE AMNANGA

Akizungumza juzi usiku kupitia kipindi cha Mada Moto cha kituo cha televisheni cha Channel Ten, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polelepole, aliendelea kusisitiza kuwa uadilifu wa Lowassa unatia shaka na kwamba, hastahili kuwa kiongozi wa taifa hili.

Polepole alisema kuwa, Tanzania inastahili kuongozwa na rais muadilifu asiyekuwa na makandokando ya ‘uchafu’ unaotokana na utumishi wake kwa umma.

Alisema pamoja na hayo, Watanzania wanapaswa kuwa mikononi mwa rais aliyeingia kwa siasa za maendeleo na sio anayeng’ang’ana kuingia madarakani kwa kutumia siasa za nguvu.

“Hawa ni watu wawili tofauti, huyu wa kwanza (wa siasa za maendeleo) anafanya siasa zake kwa nia ya kuwanufaisha wengi, lakini huyu wa pili anafanya hivyo kwa manufaa yake na watu waliomzunguka,” alisema.


CHADEMA BUNDA

Aliyekuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni za ubunge wa CHADEMA kwenye Jimbo la Bunda Mjini, Pius Masuruli ambaye nafasi yake alipewa Ester Bulaya, amekihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Ester alikuwa mbunge wa viti Maalumu (UVCCM) kupitia Vijana mkoani Mara ambapo alihama CCM na kujiunga CHADEMA.

Mbali na Masuruli, wengine waliokihama chama hicho ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa jimbo  hilo, Emmanuel Malibwa na walinzi waliorudisha kadi na kujiunga na CCM, juzi, kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM, Stephen Wassira.

Uzunduzi huo ulifanyika katika Viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Bunda na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Alisema ameamua kuhama CHADEMA kwa sababu ni cha ubinafsi, majungu na ni cha ukanda, hivyo anakiunga mkono Chama na wagombea wake akiwemo Wassira.

Masuruli alisema chama hicho kimeshindwa kutambua mchango  alioufanya na kibaya zaidi, uongozi wa juu ulikata jina lake wakati ndiye aliyekuwa ameongoza katika kura za maoni na alitangaza rasmi kumuunga mkono mgombea wa CCM.

Kwa upande wake, Malibwa alisema mbinu walizokuwa wanatumia  kukijenga chama hicho katika Wilaya ya Bunda ndizo watakazotumia kukiua na kuijenga CCM.

Wassira alisema viongozi hao wa CHADEMA wamechukua uamuzi sahihi kuihama na kuhamia katika chama makini cha CCM na kwamba, kumchukua Ester ni sawa kutwaa kapi ambalo haliwezi kushinda katika jimbo hilo.

VIJANA NA VURUGU

USIKU wa kuamkia jana, vikundi vya vijana wanaosemekana kuwa wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakizunguka kwenye kaya za maeneo mbalimbali Dar es Salaam, kuwashurutisha watu kuhudhuria uzinduzi huo.

Kitendo hicho kilisababisha usumbufu kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo yakiwemo ya Gongo la Mboto na Chanika katika Manispaa ya Ilala kutokana na kelele na vurugu zilizofanywa na vijana hao miongoni mwao walikuwa wamelewa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema vijana wengi wanaoshabikia chama hicho hawajielewi kutokana na kufuata mkumbo na kusahau wajibu kama raia kwa taifa lao, ikiwemo kudumisha amani ina utulivu.

Walisema vijana wanatumiwa vibaya na wanasiasa wenye uchu wa madaraka na wakipewa fedha kidogo wanatumika kama ngazi ya wanasiasa husika kutimiza azma yao.

Mmoja wa wafanyabiashara eneo la Pugu Stesheni, Idd Masoud, alisema alilazimika kufunga duka mapema kuhofia kuvamiwa na vijana hao waliokuwa wametawanyika maeneo mbalimbali wakiimba na kupiga kelele kwenye makazi ya watu.

Alivitaka vyombo vya usalama kuendelea kutimiza wajibu ili kudhibiti vikundi vinavyotishia usalama wa raia.


No comments:

Post a Comment