Tuesday 8 September 2015

BAKWATA YASISITIZA AMANI UCHAGUZI MKUU, MUFTI AWATAKA WATANZANIA WABADILIKE




Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), mkoani hapa limefanya dua ya kuliombea taifa ili kuliepusha na changamoto zinazojitokeza nyakati za uchaguzi ikiwemo vurugu na uvunjifu wa amani.
Aidha, limevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuepuka vurugu kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika maombi maalumu ya kuliombea taifa yaliyofanyika Mailmoja Kibaha, Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi alisema ni lazima Watanzania wabadilike kwa kutambua uchaguzi sio lazima kuwepo kwa vurugu na uvunjifu wa amani.
Aliwataka wanasiasa na wafuasi kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo pasipo kufanya jazba ambazo zinasababisha migogoro baina ya vyama.
Sheikh Zuberi alisema wanasiasa wanaokosa nafasi za uongozi wasiwe chanzo cha kuvunja amani ya nchi kutokana na kutokubali kushindwa.

“Ni vyema kila mmoja akamuomba Mungu atuvushe kwenye mabalaa ili uchaguzi mkuu ufanyike kwa haki na uhuru na ndio maana tumeona ni vyema tukafanya maombi haya kwa ajili ya kumwomba Mungu atunusuru na hali hiyo,” alisema.

Alisema Tanzania ni nchi inayosifika kwa amani ambapo ikiendelezwa itaendeleza utulivu uliopo hivyo ni vyema Watanzania wakaendelea kuilinda amani iliyopo ili nchi isiingie kwenye machafuko kama ilivyo kwa baadhi ya nchi ambazo watu wake wanapata tabu.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba, ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani, alisema tayari serikali imejipanga kufanya uchaguzi kwa njia ya amani na utulivu.
Halima alisema viongozi wa dini wanapaswa kuhakikisha amani inaendelea kudumu na watakaokwenda kinyume cha sheria, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kadhi wa mkoa wa Pwani, Abbas Mtupa, alisema tayari wametoa maagizo kwa maimamu na masheikh wa misikiti yote kufanya maombi maalumu kila Ijumaa ili kuiombea nchi amani ya uchaguzi ufanyike kwa amani.
Mtupa alisema kuwa maombi hayo maalumu ya kumwomba Mungu kwa wale wenye nia mbaya ya kuleta vurugu washindwe na kwamba yatakuwa endelevu hadi uchaguzi mkuu utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment