Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Igunga kwenye mkutano wa kampeni za CCM zilizofanyika kwenye uwanja wa Barafu |
Wakazi wa Igunga wakimsikiliza mgombea wa urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa kampeni ulioanyika kwenye viwanja vya Barafu. |
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akimnadi mgombea udiwani wa kata ya Maganzo |
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kishapu Ndugu Suleiman Masoud Nchambi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kishapu |
NA SELINA WILSON, KISHAPU
MGOMBEA Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema serikali yake
itatoa kipaumbele kikubwa kwa wafugaji na wakulima, ikiwemo kushusha bei za
pembejeo na dawa za mifugo ili kuondokana na umasikini.
Alitoa ahadi hizo zenye neema kwa wakulima na wafugaji kwa nyakati
tofauti jana, wakati akihutubia mikutano ya kampeni katika wilaya za Kishapu,
Maswa na Igunga.
Alisema anatambua changamoto zinazowakabili wafugaji na wakulima kutokana
na bei kubwa za dawa za mifugo na pembejeo pamoja na malisho.
“Tunataka mifugo itunufaishe kiuchumi, serikali yangu itaweka
mazingira mazuri kwa kuboresha upatikanaji wa dawa za mifugo ili wafugaji nao
wanufaike,” alisema.
Alisema pia anakusudia kuwekeza katika viwanda vya mazao ya
mifugo, ikiwemo viwanda vikubwa vya nyama, ngozi, viatu, mikoba na mikanda
itengenezwe hapa nchini kwa ngozi.
“Tukitengeneza viatu vya wanafunzi, viatu vya askari na kuviuza
hapa nchini na nje, tutapiga hatua kubwa kimaendeleo. Ethiopia imepiga hatua
kubwa kwa viwanda vya ngozi, kwa nini sisi tushindwe,” alisema.
Dk. Magufuli alisema pia kupitia ufugaji , serikali yake
itashirikiana na wawekezaji wa ndani kuanzisha viwanda vya kusindika maziwa ili
yauzwe nje ya nchi.
Akiwa Igunga mkoani Tabora, Dk. Magufuli alihutubia maelfu ya
wananchi waliofurika katika uwanja wa Barafu mjini Igunga, ambapo aliwatangazia
neema ya kutatua kero kubwa ya maji.
Alisema wanapotengeneza barabara, wanajenga madaraja, serikali
yake itakachofanya ni kuchimba mabwawa makubwa na kuhifadhi maji kwa ajili ya
matumizi ya wananchi.
Dk. Magufuli alisema miradi ya barabara na madaraja ndio
inayotumia fedha nyingi zaidi kuliko miradi ya maji, hivyo kama aliweza
kutengeneza mtandao wa barabara za lami kilomita 17,666, hawezi kushindwa.
“Kama niliahidi kujenga daraja la Mbutu hapa Igunga na likajengwa
na hili la maji niacheni, sitashindwa, ni mambo rahisi yanayohitaji mtu kama Dk.
Magufuli, nichagueni niwe rais ili niwafanyie kazi. Mimi Magufuli ni kazi tu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliahidi kujenga kilometa nne
za barabara za lami katika mji wa Igunga, ili kuuweka katika hali bora zaidi.
Aliwataka wananchi wa Igunga wamchague Dk. Peter Kafumu, awe
mbunge kwa kuwa yapo mambo mengi kwenye ilani yanayotakiwa kutekelezwa kwenye
jimbo hilo, hivyo wakimpatia Kafumu yatatekelezwa kirahisi.
Msichague
wabunge wasusaji
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwataka wananchi kutochagua wabunge
wenye tabia ya kususia vikao vya Bunge wakati mipango muhimu kuhusiana na
maendeleo ikijadiliwa.
Alikuwa akizungumza na wananchi wa majimbo ya Maswa Mashariki na
Magharibi, katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu.
Alisema kutokana na kuchagua wabunge wenye tabia hiyo, ndio maana
Wilaya ya Maswa licha ya kuwa kongwe, bado imeendelea kubaki nyuma kimaendeleo.
Alisema wabunge wa upinzani mara nyingi ndio wamekuwa wakisusia
vikao vya Bunge na kutoka nje wakati wenzao wakijadili mipango muhimu ya maendeleo.
“Kwenye vikao vya bajeti ndio mahali ambapo wabunge wanawabana
mawaziri ili wapitishe miradi ya maendeleo katika maeneo yao. Lakini wao
wanatoka nje na kuacha wenzao wanapigania majimbo yao,” alisema.
Alisema Maswa inapitwa na Wilaya ya Chato, ambayo ni mpya na haijafikisha
hata miaka 10, lakini imepiga hatua kubwa kimaendeleo, hivyo kuwataka wananchi
kutumia uchaguzi huu kufanya marekebisho kwa kuchagua wabunge bora wa CCM.
Dk Magufuli alisema maendeleo yanakuja kwa mipango inayoanzia
kwenye vikao mbalimbali, ikiwemo vikao vya Bunge la Bajeti, ambavyo ndivyo
vinapitisha bajeti za miradi yote ya maendeleo.
Awali, mgombea ubunge wa Maswa Mashariki kwa tiketi ya CCM,
Stanslaus Nyongo, alimuomba Dk. Magufuli awasaidie kutatua changamoto kubwa za
jimbo hilo, ambazo ni maji, barabara,umeme na elimu.
Nyongo alisema Mwaswa ndio wilaya iliyozaa Wilaya za Bariadi
na Meatu, lakini yenyewe imeendelea kubaki nyuma kimaendeleo hivyo alimuomba Dk
Magufuli akiingia Ikulu, aingalie wilaya hiyo kwa namna tofauti.
Akizungumza katika jimbo la Maswa Magharibi, Mjumbe wa NEC,
Stephen Wassira, aliwataka wananchi wasikubali kufanya majaribio wakachagua
viongozi kwa ushabiki.
“Mmewachagua wapinzani mmeona wanachofanya bungeni, msifanye
ushabiki, angalieni viongozi watakaowaletea maendeleo. Awamu ya tano itaongozwa
na Rais Dk. Magufuli, anataka watu wachapa kazi mtapata maendeleo,” alisema.
Msafara wa Dk. Magufuli, ukitokea Maswa kwenda Igunga mkoa wa
Tabora, ulilazimika kusimama katika maeneo ya Kishapu, Kolandoto na Maganzo
mkoani Shinyanga, kabla ya kuingia katika eneo la Igurubi, Igunga mkoani
Tabora.
No comments:
Post a Comment