NA MOHAMMED ISSA, MKOANI
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ameweka
historia ya kipekee kisiwani Pemba, baada ya kupeleka umeme kwenye visiwa
viwili, kikiwemo cha Kisiwa Panza na Makoongwe, ambavyo havikuwahi kupata
huduma hiyo, tokea kuumbwa kwa dunia.
Aidha, wananchi mbalimbali wameendelea kumshukuru na
kumpongeza Dk. Shein kwa kufanyakazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa
Zanzibar.
Hata hivyo, serikali imesema inafanya utafiti kwa ajili
ya kutafuta umeme mbadala badala ya kutegemea ule unaotoka Tanzania Bara.
Mbali na hilo, Dk. Shein ameliagiza Shirika la Umeme la
Zanzibar (ZECO), kuwafungia umeme wananchi ambao hawana fedha taslimu za
kuunganishiwa huduma hiyo na kwamba watalipa taratibu.
Dk. Shein alisema hayo jana kwa nyakati tofauti,
alipokuwa akizindua miradi ya umeme Kisiwa Panza na Makoongwe, wilaya ya
Mkoani, Kusini Pemba.
Alisema mwaka 2010, katika kampeni zake za urais,
aliwaahidi wananchi wa visiwa hivyo kuwapelekea umeme ambapo ahadi hiyo
ameitekeleza.
Dk. Shein alisema lengo na dhamira yake ni kuwatumikia
wananchi kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuwasambazia huduma muhimu, ikiwemo
umeme, maji safi na salama, shule, barabara na hospitali.
Alisema awamu ya kwanza ya utawala wake, amejitahidi
kutekeleza ahadi zake kwa asilimia kubwa na kwamba lengo lake ni kuibadilisha
Zanzibar na kuwa yenye maendeleo ya haraka.
Kwa mujibu wa Dk. Shein, umeme wa Pemba ukubwa wake ni
megawati 20, ambapo hivi sasa wanatumia megawati saba na Unguja umeme uliopo ni
megawati 100, lakini wanatumia megawati 53.
Dk. Shein alisema kulingana na mahitaji ya huduma hiyo
pamoja na dhamira ya serikali ya kuifanya Zanzibar, kuwa eneo huru la uwekezaji
na viwanda, umeme uliopo utakuwa mdogo, hivyo wanafanya utafiti kuangalia namna
ya kuzalisha umeme wake.
Alisema tayari wataalamu wanafanya utafiti na kwamba
baada ya miezi minane, watamaliza utafiti huo ili kubaini ni umeme gani unafaa
kuzalishwa.
“Ndugu wananchi nia yetu ni kuzalisha umeme wetu wenyewe,
hivyo kuna timu ya waatalamu wanafanyakazi hiyo na itakapokamilika, itatuelekeza
tuzalishe umeme wa jua, upepo au maji,” alisema.
Aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Makoongwe, kutumia
nishati kwa maendeleo yao wenyewe.
Akiwa Kisiwa Panza, Dk. Shein aliwataka wananchi kulipa
bili za umeme ili waweze kupatiwa huduma zilizo bora na kwa wakati muafaka.
Dk. Shein, alisema mradi wa umeme katika kisiwa hicho
umegharimu sh. bilioni 1.28, ambapo mafanikio hayo yanatokana na azma yake ya
kuwapelekea maendeleo wananchi wa Kisiwa Panza na maeneo mengine.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha anakibadilisha kisiwa
hicho kuwa kama maeneo mengine ambayo hayana visiwa ili kukuza uchumi wa
wananchi na kwamba anafikiria kuweka usafiri wa uhakika.
Dk. Shein alisema katika kisiwa hicho, huduma mbalimbali
za kijamii zimepelekwa ikiwa ni pamoja na maji, shule na pia atajenga barabara
kutoka Mtondooni mpaka Panza.
Waziri wa Ardhi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah
Shaabani, alisema kazi ya kusambaza umeme katika kisiwa cha Makoongwe
imegharimu sh. milioni 855.2.
Alisema upelekaji umeme kwenye visiwa vidogo vidogo ni
sera ya serikali ya kuwapatia huduma wananchi.
Shaabani alisema umeme kwenye visiwa hivyo umepelekwa
ikiwa ni ahadi za Dk. Shein alizotoa wakati wa kampeni mwaka 2010.
Siha Juma Ali, mkazi wa Kisiwa Panza, alisema
wanamshukuru Dk. Shein kwa kuwapelekea huduma ya umeme na kwamba ameweka
historia ya kipekee katika kisiwa hicho.
Alisema Dk. Shein ni kiongozi mahiri anayefanyakazi kwa
vitendo na sio maneno kama walivyo viongozi wengine.
Nasoro Jabu Nasoro, mkazi wa Makoongwe, alisema Dk.
Shein amefanyakazi kubwa ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar, kwa moyo mmoja
bila ya kuwabagua.
Alisema katika maisha yao hawakufikiria kuwa kisiwa
hicho kingepata umeme, lakini juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Dk. Shein,
imetimiza ndoto yao.
Mbali na visiwa hivyo, pia seriali imefunga umeme katika
kisiwa cha Kojani na hivi sasa kimebaki kisiwa cha Fundo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), uniti
moja ya umeme mpaka 50, inauzwa kwa sh. 66, ambapo zaidi ya uniti 50, inauzwa
kwa sh. 222 na uniti moja mpaka 1,500, inauzwa kwa sh. 222.
No comments:
Post a Comment