Na Khadija Mussa, Mkinga
WANANCHI wametakiwa kuendelea kuichagua CCM na kuachana
na vyama ambavyo havijajipanga kwa ajili ya kuwaongoza na havina mfumo wa
uongozi.
Hayo yalisemwa jana na mgombea mwenza wa urais wa CCM ,
Samia Suluhu Hassan, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja
vya Duga wilayani hapa.
Samia alisema wananchi wamchague Dk John Magufuli kuwa
rais ili waweze kupata maendeleo na wasithubutu kuchagua wapinzani wanaojiita
UKAWA kwa kuwa hawajajipanga kuongoza nchi na hawana mfumo wa uongozi.
"Kwanza mgombea wao urais ni CCM maslahi, amekodi
chama kwa pesa nyingi na hajapitia mchakato wowote, hivyo hajajipanga kuongoza
nchi," alisema.
Samia aliongeza kuwa hakuna sababu ya kuichagua UKAWA
kwani umoja huo haujasajiliwa sehemu yoyote, hivyo aliwaomba kuendelea
kuichagua CCM kwa kuwa ndicho chama chenye kuwaletea maendeleo.
Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu,
aliwaomba wananchi hao kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura
na kuchagua wagombea wa CCM.
Alisema wakimchagua Dk Magufuli, watamuwezesha Samia
kuwa makamu wa rais, hivyo kuliwezesha taifa kusonga mbele kimaendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Tanga,
Henry Shekifu, alisema CCM kazi yake kubwa ni kuwaletea maendeleo wananchi na
kuboresha amani, hivyo aliomba wananchi waichague.
Awali, akiwa njiani kwenda Mkinga, Samia alilazimika
kusimamisha msafara katika eneo la Mtimbwani wilayani hapa ili kuzungumza na
wananchi waliozuia msafara wake.
Akizungumza na wananchi hao, alisema serikali ijayo
itahakikisha umeme unapatikana katika vijiji vyote nchini katika muda wa miaka
miwili, hivyo aliwaomba wamchague Dk. Magufuli kuwa rais.
No comments:
Post a Comment