MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumanne Kishimba, amewataka wananchi kumuunga mkono
ili aweze kusimamia kikamilifu rasilimali zilizopo wilayani humo na pia kuharakisha
maendeleo.
Kishimba, amesema licha ya kuwa na rasilimali nyingi,
bado jimbo hilo liko nyuma kimaendeleo na kwamba, dhamira yake ya kuwania
nafasi hiyo ni kuwainua wananchi.
Alikuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika juzi mjini hapa, ambapo alisema wananchi wanatakiwa kuwa
makini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Kishimba alisema wapinzani wamejipanga kuwarubuni wakati
hawana sera wala dhamira ya kweli ya kuwatumikia.
Awali, akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Kishimba
alisema kuna mambo mengi yaliyofanyika katika kuleta maendeleo kwa wananchi na
kwamba, serikali imejipanga kuyaendeleza kikamilifu.
Alisema atahakikisha tatizo la umeme kukatika mara kwa
mara linapungua kama wananchi watampa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, kwani
linazidi kurudisha nyuma shughuli za maendeleo.
“Mimi kama mgombea ubunge wa jimbo hili kupitia CCM,
nawaomba wananchi kunipa ridhaa ya kuliongoza ili tuweze kushirikiana kwa
pamoja katika kulinda raslimali zetu
tulizonazo, ikiwemo migodi ya dhahabu kama vile Buzwagi, Bulyanhulu na viwanda
mbalimbali, vikiwemo vya pamba, tumbaku pamoja na kuleta mikopo kwa vijana ili
waweze kuendelea kujiajili wenyewe,”alisema Kishimba.
No comments:
Post a Comment