Tuesday, 22 September 2015

MAGUFULI AWAAMBIA WANANCHI WA BUKOBA 'MMETISHA'







Na Charles Mganga, Bukoba
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amewaasa Watanzania kuwaogopa na kuwakataa wagombea wanaotoa ahadi za kitapeli, badala yake wamchague ili alete mabadiliko ya kweli kwa maendeleo ya taifa.

Amewaponda baadhi ya makada waliokihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukimbilia upinzani, akisema ni wachumia tumbo na hawapaswi kusikilizwa wanayoyazungumza hivyo, wapuuzwe.

Pia, ameonyesha kushangazwa na kauli za mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa kuwa atabadilisha maisha ya Watanzania ikiwemo kuondoa nyumba za nyasi, akisema ni ahadi za uongo na zisizo na tija mbele ya Watanzania wanyonge.

Dk. Magufuli, aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano mkubwa na wa kihistoria mjini Bukoba, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kuomba ridhaa ya Watanzania wamchague ifikapo Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema anatambua shida za Watanzania na daima amekuwa akitoa ahadi za kweli na zenye kutekelezeka hivyo, Watanzania wasiwe na hofu na wamuamini kwa kumpa kura za kutosha.

“Nimekubali mnanipenda ndugu zangu…huu umati ni mkubwa sana na inaonyesha imani yenu kwangu hivyo ninaomba urais kwa ajili ya kuwatumikia.

“Wapo wagombea wanasema watabadili mambo ndani ya siku 100, sijui 40, hawa jamani si wakweli…mimi nasema ukweli na daima niko hivyo, ahadi zangu na CCM zinatekelezeka kwa sababu tuna uzoefu wa kutosha,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema wapo watu wanaowarubuni Watanzania wakidai kuwa serikali haijafanya lolote wakati walipewa nafasi za juu za Waziri Mkuu wakati kazi kubwa iliyofanywa na serikali inaonekana hadharani.

“Kuna watu wanadai serikali haijafanya chochote wakati wanaona kipo na kimefanyika kwa mafanikio makubwa sana. Kama hakuna kilichofanyika na wenyewe walikuwepo tena kwenye nafasi za juu, hawa ndio maadui zetu waliotukwamisha.

“Kama walikuwa hawaoni kinachofanywa na serikali ni kwanini waliendelea kubaki? Wangejiuzulu wakaondoka ili wanaoweza kufanya chochote wakaingia kufanya kazi. Ndugu zangu mimi siwezi siasa za blah blah kama wenzetu, kwangu ni kazi tu,” alisema Dk. Magufuli na kushangiliwa na umati wa watu uliofurika Viwanja vya Gymkhana mjini hapa.

Dk. Magufuli aliwaahidi wakazi wa Bukoba na mikoa ya jirani kuwa akiingia madarakani, atahakikisha bei ya kahawa inapanda ili kuwainua wananchi kiuchumi.

Alisema kahawa ya Bukoba imekuwa ikiuzwa kwa bei ya chini kutokana na msururu wa makato na kwamba, akiingia hilo litakuwa jambo la kwanza.

Alisema serikali itahakikisha inajenga kiwanda cha kahawa ili hata ile inayolimwa nchi jirani ya Uganda, iuzwe mkoani Kagera na kwamba, hilo litatekelezwa ili kuongeza thamani ya kahawa ya Bukoba.

“Serikali yangu nataka watanzania wawe na sauti na wanufaike na kazi wanazofanya. Kahawa bei inakuwa chini kwa sababu ya msururu wa kodi, sasa nikiingia madarakani ndio itakuwa kazi ya kwanza. Huyu waziri wa kilimo na biashara wataanza na hili,” alisema.

Kuhusu usafiri katika Ziwa Victoria, Dk, Magufuli alisema tayari serikali inaendelea kuboresha na kuna meli kubwa inatengenezwa nchini Denmark, ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa Bukoba, Mwanza na visiwa vyake.

Pia, alisema uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami itapewa kipaumbele cha pekee ili kuondoa adha kwa Watanzania.

Tibaijuka apiga magoti jukwaani
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Muleba Kusini, jana alilazimika kumpigia magoti Dk. John Magufuli, akiomba barabara ya kutoka Muleba Kusini hadi hospitali teule ya Rubya, ijengwe kwa kiwango cha lami.
 
Akizungumza katika kampeni za Dk Magufuli, anayewania urais kupitia CCM, Profesa Anna Tibaijuka, alisema amelazimika kuwasilisha ombi hilo kwa magoti kutokana na umuhimu wake na kwa wananchi.
 
Alisema hana kawaida ya kupiga magoti, lakini ameamua kufanya hivyo ili kuonyesha barabara hiyo ni moja ya vipaumbele vya Muleba.
 
"Kwa hiyo tunakuomba mgombea urais utujengee barabara hiyo kwa lami, " alisema.
 
Katika majibu yake, Dk. Magufuli alisema serikali yake itakamilisha yote yaliyoanzishwa na awamu zilizotangulia na kuahidi kujenga barabara hiyo ili wananchi waondokane na adha wanazopata.

Kabla ya kwenda uwanja wa David Zimbihile, kulikofanyika mkutano huo, Dk. Magufuli alikwenda kutoa pole kwenye msiba wa aliyekuwa mgombea udiwani, Oswald Rwakaba, aliyefariki kwa ajali.

Aidha, kabla ya kufika Jimbo la Muleba Kusini akitokea Chato, Dk. Magufuli alisimama maeneo matano ya Bwoyongera, Suyakatenga, Kyamunyora, Runazi na Rulanda, ambako aliahidi kutatua changamoto za maji, umeme na bei ya kahawa.
 
Akiwa njiani kwenda Jimbo la Muleba Kaskazini, mgombea huyo wa urais alisimama mara kadhaa na kuwahimiza wananchi kuichagua CCM iwaletee maendeleo.

"Jamani mimi sina ubaguzi, maendeleo hayana vyama, wala kabila, kwangu mie ni kazi tu," alisema.

Alisema wanapaswa kuwachagua viongozi wa CCM na kuachana na ahadi hewa wanazotoa wapinzani.
 
Alipowasili Jimbo la Muleba Kaskazini, Dk Magufuli alikuta umati wa watu ukimsubiri katika uwanja wa polisi.
Kagasheki amlipua Amani
Naye mgombea ubunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Balozi Khamis Kagasheki, amemlipua aliyekuwa Meya wa Halmashauri hiyo, Dk. Anatory Amani na watendaji wengine kuwa wamesababisha umasikini kwa wananchi wa manispaa hiyo.

Alisema kuna vitendo vingi vya wizi na ufisadi ambavyo wananchi wamefanyiwa, ikiwemo kuporwa ardhi na kulipwa fedha kiduchu huku watendaji hao wakiuza kwa bei ya juu, jambo alilosema halikubali na kumuomba Dk. Magufuli kuwashughulikia.

Balozi Kagasheki alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa mgombea urais Dk. John Magufuli uliofanyika mjini Bukoba na kuhudhuriwa na maelfu ya watu.

Alisema wananchi wengi wanyonge wameporwa ardhi zao na ‘majambazi hayo’ baada ya kujiuzia viwanja vya halmashauri na kisha kuwauzia wananchi kwa bei kubwa.

"Mheshimiwa Magufuli ukiingia ziangalie sana halmashauri maana zina changamoto kubwa, aliingia jambazi amewaibia wananchi viwanja na kisha amekimbilia huko kwingine.

"Walikuwa wakiwalipa wananchi sh. 300 kwa mita moja ya ardhi huku wenyewe wakiuza tena kwa sh. 4,500 hadi 7,000 kwa mita moja za mraba," alisema Balozi Kagasheki.

Alimuomba Dk. Magufuli akiingia madarakani aanze na halmashauri ya Bukoba Mjini ili kuondoa kero zilizoachwa na meya aliyetimuliwa pamoja na ubovu wa barabara na huduma nyingine.

Dk. Amani ameihama CCM na kujiunga na NCCR – Mageuzi baada ya juhudi za kujiunga CHADEMA kushindikana, ambapo kutapatapa huko kulitokana na uchu wa madaraka.

Katika hatua nyingine, Balozi Kagasheki alimuahidi Dk. Magufuli kura za kutosha ambapo watafanya kampeni za nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu ili kuhakikisha anashinda.

Alimwambia Dk. Magufuli kwamba wote wanaowania nafasi ya urais ni  kama watoto wake, na hakuna mwenye kuweza kuvaa saizi ya kiatu chake hivyo asiwe na wasiwasi na ushindi.

Mwijage aomba kanda maalumu
Mgombea ubunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, aliomba kuimarishwa kwa amani kama Ilani ya CCM inavyoelekeza

Alisema kutokana na vitendo vya ukatwaji makoromeo, ameomba Kagera iwe Kanda Maalumu ya Kipolisi kama zilivyo Dar es Salaam na Tarime/Rorya.

Pia alimuomba Dk. Magufuli kusaidia wananchi kujenga shule za sekondari tatu za kidato cha sita.

"Tunaomba utusaidie ujenzi wa shule tatu za sekondari kidato cha sita, "alisema Mwijage.

Hata hivyo, alisema ana uhakika chini ya utawala wa Dk. Magufuli, suala la umeme litakwisha.

Akizungumza na wananchi wa Kamachumu, Dk Magufuli alisema mji wa Kamachumu una historia hivyo, unapaswa kuendelezwa.

RANCHI ZA TAIFA
Dk. Magufuli alisema hakuna jambo lililomuumiza kama ugawaji holela wa ranchi za taifa.

Alisema alipoingia Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, alikuta ranchi 52 za mifugo, zilibinafsishwa kiajabu na waziri wa wizara hiyo aliyemtangulia.

Bila kumtaja mtangulizi wake huyo, Dk. Magufuli alisema kitendo hicho hakikumuumiza peke yake, hata Rais Jakaya Kikwete.

"Hawa wanaopita na kutoa ahadi nyingi, mbona hawajawapa ranchi," alihoji Magufuli.

Alisema suala la ranchi ya Kagera linashughulikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela, ili sehemu ya eneo hilo, waweze kugawiwa wananchi.
 
Aidha, Dk. magufuli alishangazwa na wapinzani wanaobeza kwamba hakuna kilichofanywa na CCM.
 
"Jamani wengine walikuwa viongozi kwa miaka kumi, eti wanasema hakuna kilichofanyika kitendo cha kukosa kumbukumbu, nao ni ugonjwa, " alisema Dk. Magufuli.

Mgombea huyo aliwaahidi kukamilisha upatikanaji wa meli kutoka Bukoba hadi Mwanza.
Kwa jana pekee, Dk. Magufuli alifanya mikutano kwenye majimbo ya Muleba Kusini na Kaskazini, pia alifanya kampeni katika majimbo ya Bukoba Vijijini na Bukoba mjini.

BULEMBO APASUKA TENA
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Abdalla Bulembo, amesema kama kuna mtu ana mapenzi na mgombea wa UKAWA, ruksa kuondoka CCM na kwamba, vikao vya uteuzi vya CCM vilishamaliza kazi yake na Dk. Magufuli ndio kila kitu.
 
Aidha, alimponda mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa, kuwa ameshindwa kuonyesha heshima mbele ya Watanzania wanaokwenda kumsikiliza katika mikutano yake, badala yake amekuwa akihutubia kwa dakika tatu, jambo ambalo ni kinyume na kanuni
 

No comments:

Post a Comment