Thursday, 3 September 2015

JK: TUMEJIPANGA KWA USHINDI MZITO; AMPIGA DONGO SUMAYE, AWASHANGAA WALIOKATWA URAIS KUWA NA NONGWA, AWAPONDA WALIODHANI WANA NGUVU KULIKO CCM



NA RABIA BAKARI

MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amesema amekipanga Chama vizuri na ushindi ni wa uhakika na wa lazima katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Pia, ameeleza sifa kubwa iliyosababisha Dk. John Magufuli kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, ambayo ni uadilifu na utendaji kazi wake uliotukuka na kuwashangaa wanasiasa wanaoendekeza nongwa na wengine kuhama Chama.

Amesema hata yeye alikatwa kwenye mbio za kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM mwaka 1995, lakini hakuwa na nongwa, badala yake aliendelea kuwa mtiifu kwa CCM na Mungu akamuwezesha kuliongoza taifa muda mwafaka ulipofika.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, jana, wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa Jumuia ya Wazazi katika ukumbi wa Karimjee, na kusisitiza ushindi kwa Dk. Magufuli ni wa uhakika pamoja na wagombea wengine kuanzia wa udiwani hadi ubunge.

Rais Kikwete alisema wameboresha zaidi ufanyaji wa kampeni ambapo kwa sasa zitafanyika mtu kwa mtu na ushindi utakuwa mkubwa kuanzia kwa madiwani, wabunge, wawakilishi na urais kwa Zanzibar na Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

"Kuna watu walijiona wana nguvu sana, wakadhani CCM haipo tena, lakini kumbe nguvu yao ni moto wa mabua, unawaka haraka, unazimika ndani ya muda mfupi na hautoi hata mkaa," aliongeza.

Alisema baada ya uzinduzi wa kampeni ndipo wapinzani walipoona nguvu ya CCM na wamejaribu kujipima, lakini bado hawajafikia kiwango na kukiri kwamba hakuna Chama chenye mtandao imara kama CCM.

"Sina wasiwasi tutashinda, tuna wagombea wazuri na wenye sifa waliotakiwa na  wananchi na safari hii tumejitahidi kuwawekea wanaowataka wao. Sijui kuna kampeni za Movement nini huko na harakati za mitandaoni, nawaambia hazifui dafu," alisisitiza  Rais Kikwete.

Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, Abdallah Bulembo, alimueleza Rais Kikwete kwamba wameunda kikosi kazi chenye wajumbe 33 kutoka nchi nzima kwa ajili ya kuhakikisha Chama kinapata ushindi, ambacho kitafanya kazi kuanzia ngazi ya taifa hadi kata.

Rais Kikwete alisema amefurahishwa na hatua hiyo na inaonyesha jumuia imefufuka na inafanya yale ambayo ni madhumuni ya kuundwa kwake.

Kwa upande wa uteuzi wa Dk. Magufuli, alisema tangu hapo awali hakuwa na mgombea yeyote na zaidi alikuwa hajui vigezo gani hasa vilitumika na waliopita kupata wagombea.

"Ubaya wa kazi ya uteuzi, unaifanya unapoondoka, na si utafanya kisha utarudia wakati mwingine, hivyo nilikuwa sielewi chochote.

"Niliamua kumfuata Mzee Mwinyi (Ali Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili) na Mkapa (Benjamini, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu), nikawauliza walifanyaje, walinijibu kwamba wanafuata muongozo wa Nyerere (Julius, Hayati Baba wa Taifa)," aliongeza.

Aliutaja muongozo huo kuwa sharti la kwanza ni kuteua mtu ambaye ana umri mdogo kuliko Rais anayestaafu kwa sababu ya muundo wa kizazi kwa kuwa akiteuliwa mtu sawa na anayestaafu ama aliyezidi umri, kuna vizazi havitaingia katika uongozi.

"Jambo lingine kubwa ni uadilifu, na hilo halina mjadala.  Kuna watu wanasema ooh alikuja na majina yake mfukoni, mara ooh kuna watu walilazimishwa kupigia majina ya tano bora kura, si kweli kila mmoja alipiga kwa hiyari yake na hata huyo Lowassa alipiga kura," aliongeza.

Alimsifu Bulembo kwa kazi kubwa ya kufufua jumuia hiyo, ikiwemo kurudisha shule ambazo zilitaifishwa na watu waliojibinafsisha mali za jumuia.

Alisema Bulembo ana sifa kubwa ya kutoona haya wala kigugumizi kuitetea CCM, huku akilinganisha kwamba kuna watu wana uwoga hadi hutamani kuvua mashati ya Chama wanapoona hali ngumu.

Aliwataka kutafuta nafasi ya kukutana na jumuia zote za Chama ili kuongeza mikakati hasa ya kampeni za mtu kwa mtu, kwa kuwa watu wanaokwenda kukutana nao ndio haohao.

Katika hatua nyingine, Bulembo alimuomba Rais Kikwete awe mlezi wa jumuiya hiyo kwa sababu yeye ndiye aliyefanya juhudi kubwa ya kuiokoa isizame.

Akijibu hoja hiyo, alisema atawafikiria akishastaafu kwa kuwa sasa hawezi kusema atakuwa mlezi, ilihali yeye ni mtendaji wa jumuia zote ndani ya Chama.

Pia, Bulembo alimueleza Rais Kikwete hapo awali kupitia vyanzo vyake vya mapato, jumuia ilikuwa ikikusanya sh. milioni 50 tu kwa mwaka, lakini sasa wanakusanya zaidi ya sh. bilioni 1.3, kutoka vyanzo vilevile na kwa watendaji wale wale waliokuwepo mwanzoni.

Kikwete ampiga dongo Sumaye

RAIS Jakaya Kikwete amesema kiongozi anapokuwa amemaliza muda wake wa uongozi na kustaafu, kamwe  hawezi tena kuanza kudai kwa nini hasikilizwi, ama kuombwa ushauri wa uongozi mpya.

Bila kumtaja jina, Rais Kikwete alieleza kushangazwa na kiongozi mmoja mkubwa katika serikali iliyopita, ambaye amehamia upinzani, kulalamika kuwa moja ya sababu za kuhama ndani ya CCM ni kutoombwa ushauri.

“Nilisikia mtu mmoja analalamika majuzi kuwa anahama chama kimoja kwenda kingine kwa sababu haombwi ushauri. Sasa wewe ulikwishakuwa waziri mkuu, umemaliza ngwe yako ya uongozi, unalazimisha kuombwa ushauri kwa nini? Huwezi kulalamika kuwa huombwi ushauri,” alisema.

 Rais Kikwete alionge kusema: “Mimi namaliza ngwe yangu ya uongozi. Nastaafu, naondoka. Kama rais anayekuja ataona ni jambo mwafaka kutaka ushauri wangu, nitachangia kwa kadri ya uwezo wangu, lakini kiongozi aliyestaafu hawezi kulazimisha kuombwa ushauri.”

Rais Kikwete alikuwa akizungumza katika hafla ya kumuaga ambayo iliandaliwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania, mjini Dar es Salaam, ambapo alisema kamwe  hatalazimisha hilo hadi atakapoombwa.

Alisema rais yeyote anakuwa amekamilika kwa maana ya washauri na masuala yote ya usalama hufanywa na vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wengine.

“Rais anakuwa amekamilika kila idara, kuhusu usalama mpo ninyi, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimekamilika. Mtampa ushauri rais anayekuja kama mlivyokuwa mnanipa miye.

“Na wala siombi  mje kwangu kuomba ushauri kwangu.  Nendeni kwa rais na Amiri Jeshi Mkuu wetu. Vinginevyo mtanitengenezea fitina na kiongozi wangu. Sitalazimisha wala kulalamika kuwa sijaombwa ushauri,” aliwaambia maofisa hao.

“Ninyi ndio mlikuwa nguzo yangu na washauri wangu mahiri, ndiyo maana tumeifikisha nchi yetu hapa ikiwa tulivu na salama. Kama mlivyonifanyia mimi, ushauri huo na nguvu zenu zote sasa zielekezeni kwa rais wetu mpya na nchi yetu itaendelea kuwa tulivu na salama,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment