Thursday, 3 September 2015
MAGUFULI AWAASA WATANZANIA KUWA MAKINI
MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli, amewataka Watanzania
kutafakari na kufanya uamuzi sahihi na kamwe wasichague kiongozi kwa
kigezo cha kutaka mabadiliko.
Amesema mabadiliko yanayopaswa kufanywa na Watanzania ni kumchagua
kiongozi bora na mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za
umasikini pamoja na kupambana na ubadhirifu serikalini.
Dk. Magufuli alifafanua kuwa kuna baadhi ya mataifa yameingia kwenye
machafuko yaliyosababisha kuzorota kwa uchumi na ustawi wa wananchi
baada ya kufanya mabadiliko mabaya ya kisiasa.
Akizungumza na wajumbe wa Jumuia ya Wazazi wa CCM, Dar es Salaam,
jana, Dk. Magufuli alisema, mabadiliko ya kukurupuka yamesababisha
nchi za Syria, Libya na Misri kujikuta katika machafuko.
“Wakati wa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar
Gaddaf, maisha ya wananchi wa Libya yalikuwa mazuri, lakini kwa
kufanya maamuzi ya kukurupuka kwa madai ya kutaka mabadiliko, hali ya
taifa hilo imekuwa mbaya.”
Alisema wananchi wanapaswa kusimamia amani na kufahamu kuwa mabadiliko
ya kweli yanaendana na ustawi wa amani.
Alisema Watanzania hususan vijana wanapaswa kuelimishwa kufahamu
historia ya nchi.
Aliongeza kuwa CCM ni miongoni mwa vyama vilivyojitolea kufanikisha
harakati za ukombozi kwenye nchi za Kusini mwa Afrika.
Alisema licha ya baadhi ya mataifa yaliyokuwa yakitawala nchi za
Afrika kutopendezewa na kazi hiyo ya CCM, lakini Chama kimeendelea
kubaki kuwa imara.
Alisema kuna nchi zilizofanikisha kufanya mabadiliko ya kweli kwa
kuimarisha uchumi na maendeleo yenye kupigiwa mfano.
Dk. Magufuli alisema China imefanikiwa kuimarisha uchumi wake baada ya
kufanya mabadiliko ambayo yalisimamiwa na chama tawala cha
Kikomunisti.
Mgombea huyo wa urais wa CCM, alisema katika utumishi wake amekuwa
akimtanguliza Mungu kwa sababu, ndiye mwenye njia ya haki.
Alisema endapo atashika madaraka ya nchi, atazingatia utumishi bora
kwa maslahi ya taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment